Na Walter Mguluchuma -MPANDA
TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Katavi, imewatia mbaroni watu wawili kwa tuhuma za kupokea rushwa.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi, John Minyenya aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Nicodemo Peter na Peter Mwaninsawa, wote ni wakazi wa Mtaa wa Nsemlwa Manispaa ya Mpanda.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakipokea rushwa ya Sh 400,000 nje ya jengo la Ikulu ndogo Mkoa wa Katavi, kwa kujifanya wao ni maofisa wa Takukuru.
Minyenya alisema watuhumiwa hao walikamatwa jana asubuhi baada ya kuwekewa mtego huo baada ya kupata taarifa kutoka kwa msiri wao juu ya watu hao waliokuwa wakijiita ni maofisa wa Takukuru Kitengo cha Uchunguzi.
Alisema kabla ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao walimpigia simu msiri wa Takukuru wakidai kuwa wana jalada la uchunguzi dhidi ya msiri huyo.
“Kutokana na hali hiyo watu hao walimtaka msiri wetu awape Sh 400,000 waweze kulifunga jalada kwa kufuta tuhuma zilizomkabili msiri huyo ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Vikonge wilayani Tanganyika.
“Walidai alikuwa akituhumiwa kupokea rushwa ya kutoka kwa wafugaji ambao alikamata mifugo yao na kuiachia baada ya kupokea rushwa ya Sh milioni 2.5.
“Msiri wetu huyo ambaye hapendi na anapinga rushwa alilazimika kufika ofisi ya Takukuru na kutoa taarifa juu ya maofisa hao bandia wa Takukuru na tulipowekewa mtego tulifanikiwa kuwatia mbaroni leo (jana),” alisema Minyenya.