27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI YAPANDIKIZA BETRI KWA MTOTO MWENYE MOYO UPANDE WA KULIA

NA VERONICA ROMWALD–DAR ES SALAAM

MTOTO mwenye umri wa miezi tisa (jina linahifadhiwa) ambaye moyo wake umekutwa upo upande wa kulia tofauti na hali ya kawaida, amefanyiwa upasuaji mkubwa kutibu tatizo lililomkabili.

Upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji moyo wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na wenzao kutoka Taasisi ya Open Heart International (OHI).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, alisema hii ni mara ya kwanza wanafanya upasuaji kwa mtoto ambaye moyo wake upo upande wa kulia.

“Kwa kawaida moyo wa binadamu huwa upo upande wa kushoto, kati ya watoto 2,000 wanaozaliwa duniani, mtoto mmoja anaweza kuzaliwa moyo wake ukiwa upande wa kulia kama huyu.

“Lakini moyo kuwa kulia si tatizo, tulimpokea kutoka Hospitali ya Bugando ambako walihofia huenda ikawa ni tatizo walipogundua moyo wake upo kulia.

“Tulimfanyia uchunguzi alipofika hapa tukabaini pamoja na kuwa na moyo kulia, alikuwa na tatizo kubwa kwa sababu vyumba vyake vya moyo vilikuwa vinafanana wakati vinapaswa kuwa tofauti.

“Kutokana na hali hiyo, damu chafu iliyokuwa ikiingia katika moyo ili kusafishwa ilikuwa ikichanganyika na ile safi ambayo husukumwa kwa pamoja ndani ya mwili, jambo lililokuwa linahatarisha maisha yake.

“Tukagundua tatizo jingine kwamba umeme wake wa moyo ulikuwa chini ya kiwango kiasi cha kushindwa kusukuma damu vema kwenda sehemu mbalimbali za mwili, hivyo tumemfanyia upasuaji mkubwa wa kurekebisha vyumba vyake na tumempandikiza betri,” alisema.

Alisema katika kambi hiyo ya matibabu iliyoanza Novemba 25, mwaka huu hadi Desemba Mosi, mwaka huu, wamewafanyia upasuaji wagonjwa 16.

“Kati yao, tisa walikuwa watoto waliokuwa na uzito wa kuanzia kilo nne hadi 12 ambao umri wao ni miezi minne hadi miaka minne,” alisema.

Alisema wagonjwa saba walikuwa watu wazima waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu katika moyo na kubadilisha milango ya moyo miwili hadi mitatu iliyokuwa imeziba au haikufunga vizuri.

Mkufunzi wa Wagonjwa Mahututi na Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa OHI, Dk. Russel Lee, alisema wataendelea kushirikiana kwa ukaribu na JKIC katika kutoa matibabu.

“Kila ninapokuja Tanzania naona JKCI inazidi kufanya matibabu kwa kiwango cha juu zaidi ya awali, hili ni jambo linalotia faraja kubwa, OHI tutaendelea kushirikiana nao pia kwa kuwapatia mafunzo wataalamu wake ili wazidi kufanya vizuri zaidi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles