DAMASCUS, SYRIA
RIPOTI iliyowasilishwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inayolaumu Syria kutumia gesi ya sumu aina ya Sarin wakati wa shambulizi lililotokea katika mji wa Khan Sheikhun, ambalo lilisababisha vifo vya watu wengi, wakiwamo watoto, imepingwa.
Naibu Balozi wa Urusi, Vladimir Safronkov, amesema kazi iliyofanywa na jopo la uchunguzi ni ya kukatisha tamaa na kwamba linatumiwa na Magharibi kuijengea taswira mbaya Serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Chombo cha uchunguzi wa pamoja (JIM), kilihitimisha katika ripoti hiyo mwezi uliopita kuwa, Serikali ya Syria ilihusika na mashambulizi ya gesi ya sumu ya Sarin ya Aprili 4, mwaka huu, katika eneo hilo.
Urusi, mshirika wa Syria na Marekani, wameweka miswada yao ya maazimio yenye kukinzana juu ya kurefusha shughuli za jopo hilo, itakayokamilika Novemba 16.
“Tuna hakika kuwa utaratibu huo, ulio na jukumu la juu, hauwezi kufanya kazi kwa njia hii,” Safronkov aliliambia baraza hilo. “Bila mabadiliko ya kina, litakuwa chombo cha kuvutana na Serikali ya Syria,” alisema.
Urusi inasisitiza ripoti hiyo haiaminiki, kwa sababu wataalamu hawakwenda eneo lililoathirika la Khan Sheikhun na badala yake walichunguza sampuli zisizo za kweli.
Awali akiwasilisha matokeo, Edmond Mulet, mkuu wa jopo hilo, alisema wataalamu wamegundua sumu ya gesi ya Sarin ilidondoshwa kutoka angani na ndege za Syria zilikuwa eneo hilo.
Mulet alisema uchambuzi wa gesi ya sarin iliyotumiwa Khan Sheikhun ilifanana na gesi inayoathiri neva inayopatikana katika hifadhi ya Syria na kwamba ni ngumu kuiiga.
Lakini Safronkov alijibu hilo kuwa, kemikali zinaweza kuzalishwa mahali popote na kuitupia lawama makusudi Serikali ya Syria.”