NA SALMA MPELI – ALIYEKUWA SINGIDA
NOVEMBA 4, mwaka huu, wapenzi wa soka wa mkoani Singida walifanikiwa kushuhudia pambano la Ligi Kuu Bara (VPL) kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 17.
Kukosekana kwa burudani hiyo kulitokana na timu ya Singida, iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, kushuka daraja, kabla ya kupanda tena msimu uliopita.
Mchezo huo, uliopigwa Novemba 4, ulizihusisha timu ya Singida United dhidi ya Yanga ya Dar es Salaam na ulipigwa kwenye Uwanja wa Namfua, uliopo Manispaa ya Singida na kumalizika kwa suluhu.
Kabla ya mchezo huo, Uwanja wa Namfua ulifungwa ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa ukarabati ambao ulikuwa wa takribani miezi minne.
Hatua hiyo iliilazimu Singida United kusaka uwanja mwingine ili kuutumia kama uwanja wake wa nyumbani katika michezo ya Ligi Kuu, ambapo ilifanikiwa kuupata wa Jamhuri, ulioko Manispaa ya Dodoma.
Hatua ya kukosa kushuhudia pambano la Ligi Kuu kwa kipindi kirefu ilisababisha wenyeji wa Mkoa wa Singida kuwa na shauku ya kwenda uwanjani kuziona Yanga na Singida United zikiumana.
Kabla ya mchezo huo, mashabiki wa mji wa Singida walikuwa na shamrashamra, huku mazungumzo katika vijiwe mbalimbali yakihusu pambano kati ya timu hizo.
Madereva wa bodaboda, bajaji na teksi walionekana wakijadili juu ya mchezo huo katika vijiwe vyao.
Hali iliyoonekana mjini hapo ni kama kulikuwa na matayarisho ya sikukuu za kidini kama Krismasi au Idd, ambazo zimekuwa zikisherehekewa kwa bashasha.
Kituko cha mwaka ni pale mashabiki wa soka walipovamia uwanja kwa lengo la kuishuhudia Yanga, lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa baada ya wachezaji wa timu hiyo kutumia muda mfupi kufanya mazoezi ya kupasha misuli, kisha wakaondoka zao.
Siku ya pambano, mashabiki walianza kuwasili uwanjani hapo kuanzia saa tatu asubuhi, hadi inafika saa saba mchana misururu mirefu ya watu ilionekana nje ya uwanja.
Hata hivyo, idadi ndogo tu ya mashabiki ndio walifanikiwa kuingia uwanjani, kutokana na kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki elfu 10 pekee.
Kutokana na uwezo mdogo wa uwanja katika kuingia watu, mashabiki wengi walishindwa kuingia uwanjani, hatua iliyosababisha baadhi yao kupanda juu ya miti na mawe makubwa yaliyoko kando ya Uwanja wa Namfua ili kushuhudia pambano hilo.
Wadau wa soka nchini wamezoeleka wakiingia uwanjani mapema zaidi katika mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga, lakini hii ya Singida na Yanga imekuwa ni mechi nyingine iliyobeba mashabiki wengi na kujaza uwanja mapema zaidi.
Wakati mchezo unaendelea, mashabiki wa Singida walionekana kugawanyika katika makundi matatu, la kwanza lilishangilia matukio ya kufurahisha yaliyofanywa na timu zote mbili, kama Yanga walishambulia lilishangilia na hivyo hivyo kwa Singida.
Kundi la pili na la tatu, haya yalikuwa yakipingana, moja lilionekana likiishangilia Singida United muda wote wa mchezo na jingine liliishangilia Yanga dakika zote 90 za mchezo huo.
Hivi ndivyo hali ilivyokuwa kabla na baada ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Singida United kupigwa mkoani Singida.