LONDON, England
MCHEZAJI wa zamani wa Chelsea, Frank Lampard, amesema angependa kushirikiana na klabu hiyo ikiwa ni pamoja na kuziba pengo lililoachwa wazi na Mnigeria, Michael Emenalo la Ukurugenzi wa Ufundi.
Jumatatu iliyopita Emenalo, alifanya uamuzi mgumu na kushangaza wengi baada ya kujiuzulu nafasi yake hiyo aliyodumu kwa miaka 10.
Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, Marina Granovskaia, alithibitisha kwamba kwa sasa wanapitia upya mfumo wao wa uongozi wa klabu hiyo.
Hata hivyo, inaonekana kwamba bado haijawekwa wazi kama Chelsea wana mpango wa kuajiri mkurugenzi mpya wa kufanya kile kilichokuwa kikifanywa na Emenalo, lakini Lampard ambaye alikuwa akifanya kazi BT Sport na kusoma mafunzo ya ukocha tangu atangaze kustaafu Februari mwaka huu, ametajwa kama mtu sahihi wa kurithi mikoba hiyo.
Lampard alipoulizwa kama yupo tayari kuacha kazi BT Sport na kujiunga na Chelsea alisema: “Nilifanya kazi na Michael kwa miaka saba au nane na kazi yake ilikuwa ya mafanikio katika historia ya Chelsea, nafikiri anastahili pongezi.
“Kila mmoja ndani ya Chelsea anamtakia mafanikio mema huko aendako, nikiwa mmoja wao, mimi ni mtu wa Chelsea, ningependa kuwa miongoni mwa jambo fulani la muda mrefu kwenye klabu hiyo, hata hivyo hilo litafahamika hapo baadaye,” alisema Lampard.
Lampard hakufanya siri kuhusu matamanio yake kuwa katika uongozi wa klabu hiyo ambapo yatamfanya siku moja kuwa kocha wa timu hiyo.
Mtandao wa ESPN ulieleza kuwa Chelsea ipo katika harakati za kutafuta wachezaji wao wote wa zamani ili kuziba pengo hilo.
“Nahitaji kusoma, nimecheza soka kwa miaka 20 hainifanyi kuwa kocha mzuri, natakiwa kujifunza lakini ningependa kutumia uzoefu wangu niliotumia katika soka nikiwa kama mchezaji. Ni kweli nimetumia muda mwingi Chelsea, hiyo inaweza kuwa sababu na kukamilisha ndoto zangu, hata hivyo si kazi nyepesi.
“Nimefanya kazi na makocha wengi, natakiwa kuchukua yaliyo mazuri na mabaya kutoka kwao na kutafuta njia yangu. Ningependa kufanya kazi na wachezaji chipukizi na kuwafanya kuwa bora,” alisema Lampard.