Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), amesema miradi mikubwa itaua uchumi wa taifa kutokana na uendeshaji ambao utaifanya serikali kutokopesheka.
Amesema sifa ya miradi hiyo mikubwa ambayo ina gharama kubwa ni mabilioni ya dola ambayo uwekezaji wake huchukua muda mrefu ambayo pia kulipia kwake huchukua muda mrefu sana.
Akichangia mjadala wa mpango wa maendeleo bungeni leo, Nape emesema miradi mingi yaa aina hiyo si ya kulipa hivi karibuni.
“Sipingi miradi hii isipokuwa ninapingana na mapendekezo ya serikali ya namna ya kuwekeza na kuendesha miradi hii kwa kutumia fedha za serikali kwenye miradi hii.
“Tafsiri ya uamuzi wa kutumia fedha za serikali kwenye miradi hii kwanza itailazimisha serikali kutumia pesa nyingi hivyo lazima serikali iende kukopa, na serikali ikikopa itaanza kulipa deni lililokopwa kabla ya miradi kuanza kulipa faida kwa nchi yetu, kwa hiyo tutachukua hela kwenye maeneo mengine tulipie deni kwenye miradi hii na kufunga mikanda muda mrefu,” amesema.
Aidha, amesema zikichukuliwa fedha za maeneo mengine maana yake utaathiri miradi ya huduma, elimu afya na itafika mahali hata fedha za wafanyakazi itashindikana kulipwa, kuna madhara makubwa kwa deni la Taifa kuchukua fedha za serikali ambazo ni lazima kukopa kuwekeza kwenye miradi hii.
Nape amesema alitegemea miradi hiyo ingeruhusu sekta binafsi kwa kutengeneza mazingira kwa sekta hiyo kuwekeza kwenye miradi hiyo badala ya kuchukua fedha za serikali na kupeleka kule.
“Miradi hii ni ya uzalishaji wa umeme Stigler’s Gorge, ujenzi wa reli, uboreshaji wa shirika la ndege, miradi ya bandari, barabara ni baadhi ya miradi ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara na ikajilipa. Sababu za kuchukua hela za serikali na kupeleka huko kwa kweli sijaiona,” amesema Nape.