NAIROBI, KENYA
GAVANA wa Kaunti ya Nyeri nchini Kenya, Wahome Gakuru, amefariki mapema jana baada ya kupata ajali barabarani katika eneo la Kabati, barabara kuu ya Thika-Sagana, Kaunti ya Murang’a.
Alikimbizwa katika Hospitali ya Thika Level 5 kwa matibabu ya dharura, lakini akaaga dunia.
Kamishna wa Kaunti ya Murang’a, John Elungata, alithibitisha kifo hicho na kusema Kabati ni eneo hatari na madereva hukosa mwelekeo kila inaponyesha mvua.
Maofisa wa polisi walisema kuwa gari la gavana huyo lilikuwa na abiria wanne wakati wa ajali hiyo ,akiwamo msaidizi wake binafsi, dereva na mlinzi wake.
Mkono na mguu wa msaidizi wake binafsi ilivunjika, huku miguu ya mlinzi wake ikipata majeraha makubwa na dereva akielezwa yu katika hali nzuri.
Mapema siku ya Jumatatu alipiga picha na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Alliance Boys wanaofanya mtihani wa kidato cha nne.                                                                                                                   Polisi walisema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gurudumu moja la gari hilo kupasuka wakati mvua kubwa ikinyesha.
Mwili wa gavana huyo umesafirishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee jijini Nairobi.
Inadaiwa kuwa gavana huyo alikuwa akielekea kuhudhuria kipindi kimoja cha redio na runinga wakati gari lake lilipokumbwa na ajali hiyo.
Dk. Gakuru ni gavana wa pili wa Nyeri kufariki dunia akiwa madarakani baada ya Nderitu Gachagua kufariki Februari, mwaka huu.