SENETA wa zamani katika Bunge la Taifa la Nigeria mwenye umri wa miaka 87, Cyrus Nunieh ameamua kufunga ndoa katika umri wake huo mkubwa.
Seneta Nunieh, aliiteka mitandao ya jamii hivi karibuni baada ya picha zake za harusi kwa mkewe Rosemary Ijeoma kusambaa mno.
Anasema aliamua kuoa mke mwingine kwa sababu ya kuchoka kuishi mpweke kwa miaka mingi.
Kama ilivyo kwa wenzi wengi, walifunga ndoa mbele ya wanafamilia na marafiki na waliapa kiapo cha ndoa hadi kifo kitakapowachukua.
Hafla hiyo ya harusi ya Nunieh na mkewe mpya Rosemary Ijeoma anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka ya 40 ilifanyika katika Hoteli ya Kifahari ya Kirais katika Bandari Harcourt, Jimbo la Rivers.
Anasema amekuwa akiishi bila mwenzi baada ya mkewe wa zamani kufariki dunia mwaka 1991.
“Nisingeweza kukabiliana tena na upweke huu ukizingatia pia watoto wangu wote ni watu wazima na wana maisha yao wenyewe yaliyotawaliwa na shughuli nyingi.
Nunieh amemuelezea mkewe mpya Rosemary kama mwanamke mwenye akili, ambaye yuko daima kwa ajili yake.
Anasema: “Siwezi kuendeea kukaa peke yangu. Nampenda sana na yeye ananipenda, tunaelewana na ana akili sana.
“Katika ndoa kuna faida sehemu fulani na hasara maeneo mengine. Hakuna ukomo wa umri, baadhi wanaweza kusema ni mzee na utakufa muda si mrefu, lakini kumbuka wengine walikufa kabla hata hawajazaliwa.
“Baadhi walikuwa na mwaka mmoja au miwili na wakafa. Kifo hakitegemeani daima na umri wa mtu.”
Anaongeza: “Unajua kuwa waridi (rose) ni ua zuri kuliko yote na tuna Mary wawili katika Biblia; tuna Mary, mama wa Yesu na Mary Magdalene. Yeye pia (Rosemary) ni muumini wa Biblia.”
Senata huyo ambaye kwa sasa ni mfalme wa Ogoniland katika Jimbo la Rivers anawazodoa wale wanaoshangaa umri wa mkewe, kwamba kwanini wanaguswa na umri wake? Huku akisema yeye si kichanga na ni mwanamke mcheshi.