Na MARK MWANDOSYA
TUNAENDELEA na historia ya Ufukwe wa Matema, ambao una mambo mbalimbali yenye kuvutia ambayo watu wengi hawayafahamu. Endelea kutoka pale tulipoishia jana…
Wavuvi waliozungumzia suala la huduma za ugani na mafunzo ya uvuvi bora wanathibitisha kutokuwapo kwa huduma za aina hiyo. Wanasema huwa wanaambiwa kama wanataka mafunzo inabidi waende Kyela. Hivyo basi, wao hutumia uzoefu wa asilia waliorithishwa na wazazi wao.
Wamekiri kukutana na baadhi ya maafisa wa uvuvi, lakini ni katika mazingira ya wataalamu hao kukagua leseni za uvuvi. Wavuvi wanashangaa kuhusu kutakiwa kuwa na leseni. Kwani kwao uvuvi ni kama kilimo. Maafisa hao wakiwakuta wavuvi na samaki katika mitumbwi na kama hawana leseni, basi huondoka na samaki hao na kusema, “mmetuvulia mboga”.
Tabia hiyo inaendelezwa na maafisa uvuvi wanapokagua nyavu. Kwa mujibu wa wavuvi hata kama nyavu zinazotumika ni halali, hunyag’anywa na kuuzwa sehemu nyingine bila kutolewa risiti za mauzo.
Uvuvi wa kisasa na wa kibiashara ni pale mitumbwi ya kisasa au meli ndogo za uvuvi zinazoweza kwenda mbali, zinapotumika. Wavuvi wadogo inabidi waungane katika vikundi ili waweze kukopeshwa na vyombo vya fedha ili wanunue vifaa vya uvuvi vya kisasa. Ni muhimu pia idara ya uvuvi ikawa na mitumbwi ya kisasa ili kutoa huduma za ugani na mafunzo ya uvuvi endelevu.
Ngunga (Lake Nyasa flies)
Ukikaa ufukweni Matema wakati Ziwa Nyasa likiwa limetulia, kwenye upeo, kwa mbali kabisa unaweza kuona umbile kama vile moshi unaobaki nyuma kama meli imepita.
Mara ya kwanza nilibishana na wenyeji wangu nikiwaambia meli ya MV Songea ilikuwa ikipita kwa mbali kutoka bandari ndogo zilizopo mwambao wa Ziwa. Wenyeji wakanicheka kama vile sijui kitu. Na hakika sikuwa najua.
Kwani ule ulikuwa si moshi bali makundi makubwa ya wadudu wenye umbo la mbu ambao huletwa mwambao na upepo mkali unaotoka ziwani.
Ngunga (Chaoburus edulis) hutokana na mabuu (larvae) ambao huzaliana juu ya maji. Baada ya kukua hubadilika kuwa kama mbu au inzi wazima na huelea katika makundi makubwa ambayo huonekana kwa mbali kama moshi.
Mabuu ni chakula cha muhimu cha samaki na ngunga wenyewe ni chakula cha ndege na binadamu. Makundi ya ngunga yanapofika ufukweni wenyeji hujitokeza na ndoo na vikapu ili kuwakusanya.
Kwa taarifa za wenyeji wa hapa, baada ya kuwatengeneza kama keki, Ngunga huwa chakula kitamu na chanzo muhimu cha protini kwa ajili ya mwili.
Wenyeji huku hawakosi maelezo kuhusu asili ya ngunga. Ukizungumza na baadhi yao watakwambia ngunga wanatoka kwenye miamba iliyo chini ya ziwa. Wakifika ufukweni, baada ya siku moja hurudi majini na hukua na kuwa samaki wadogo, dagaa au usipa, kama dagaa wanavyojulikana huku. Wengine watakwambia ngunga wanatokana na Nyifwila anapofuka moshi.
Nyifwila
Nyifwila ni tafsiri ya kinyakyusa ya neno la Kiingereza dragon, ambalo kwa mujibu wa Kamusi ya Ufafiti wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI) lina maana zimwi, au mnyama mtambaachi mkubwa mwenye mbawa na kucha, na daima hupumua moto. Ni myama wa kutisha mithili ya joka kubwa, lenye vichwa vingi na ambaye anaishi katika fikra tu akiwa ni kielelezo cha nguvu na uwezo mkubwa.
Mataifa mengi ya Asia ya Mashariki yanatumia zimwi hili kama alama ya kidini na kitaifa. Wachina wameupa mwaka mmoja kati ya mzunguko wa miaka 12, wa miaka ya wanyama 12, kuwa ni mwaka wa dragoni.
Kwa jamii ya Kichina, watoto wengi zaidi huzaliwa mwaka wa dragoni kwa sababu ya imani kwamba watoto hao huwa na bahati katika maisha. Kwa kalenda ya Wachina, mwaka wa 2012 ulikuwa ni wa dragoni na utafuatiwa na mwaka 2024.
Jamii nyingi zina hadithi au simulizi (anecdotes) zinazorithishwa kizazi hadi kizazi kuhusu uwapo wa matukio ya ajabu yanayohusisha matukio yanayotokana na nguvu za ajabu za mazimwi ya kila aina (mythical).
Wengi wetu tuliopata nafasi ya kupata elimu nchini Uingereza, au wale ambao wamesoma kuhusu mila na desturi za Waingereza hatuwezi kusahau simulizi za mara kwa mara za kuonekana au kutoonekana kwa Zimwi la Loch-ness (Loch-ness monster), zimwi ambalo inadaiwa ni la bahari linaloishi katika ziwa linalotokana na sehemu ndogo ya bahari kuzungukwa na ardhi. Loch maana yake ziwa kiskoti na kiirish. Zimwi liliotajwa awali linasimuliwa kuishi katika Ziwa Ness huko Uskoti, Uingereza ya Kaskazini.
Kwa maelezo ya jirani yangu, Mzee Abudile (85), Nyifwila anaishi chini kabisa ya Ziwa Nyasa. Haonekani na binadamu isipokuwa kwa miujiza. Ni zimwi kubwa lenye vichwa takriban kumi na mbili.
Nyifwila ana macho mengi kama nyota. Huko aliko akichukia basi Ziwa Nyasa linachafuka. Akilala, ziwa linatulia. Akitoka huko aliko na kuja mwambao basi huacha mawimbi makali na dhoruba ziwani na pwani. Mara chache anapofanya hivyo huelekea milimani, milima ya Livingstone.
Tunajua alikuwa huko pale anaporudi ziwani. Kwani huacha mawe yakiporomoka kutoka mlimani, na njia anayochukua hufuatiwa na mto. Anapopita huacha mafuta yanayowaka moto. Ukikanyaga mafuta hayo utadhurika.
Ni wazee wa kimila tu wanaoruhusiwa kuchukua mafuta yaliyo katika mapito ya Nyifwila kwa ajili ya shughuli zao za kijadi kama vile kutengenea dawa au kufanyia matambiko.
Kama ilivyo kwa zimwi la Loch-ness hakuna anayeweza kuthibitisha kuiona Nyifwila. Kama ilivyo kwa binamu ya Nyifwila aliyeko Uskoti, watu hushindana kuangalia ziwa kuona kama anaweza kuonekana. Mzee Abudile anaapa yeye amewahi kusindikizwa na Nyifwila usiku wa manane akitokea Malawi kuvuka Mto Songwe hadi karibu na Itungi akirejea Matema.
Ndugu zake hawaamini hadithi yake. Kwani wanasema kwa kuwa karibu tu na Nyifwila, leo hii Abudile angekuwa ametangulia mbele za haki.
Loch-ness ni kivutio kikubwa, kila mtalii akijaribu kuingia katika rekodi ya kuliona zimwi. Ni zoezi linaloendelea kwa zaidi ya miaka 1500 hadi sasa na utalii huo huiingizia halmashauri ya eneo hilo wastani wa Sh bilioni 90 kwa mwaka.
Pango la Matambiko la Pali-Kyala
Mila na desturi za jamii nyingi duniani kote zinahusu uwapo wa maeneo ambayo hutumika na kulindwa kijadi kwa ajili ya matambiko.
Kwa jamii za Kiafrika kusini mwa jangwa la Sahara, utamaduni huo unahusu kutoa matambiko kushukuru kwa kile jamii imetendewa na asili, maombi ya jamii kwa miungu wao kwa ajili ya mvua ili kuondokana na ukame, jamii kuepushwa na majanga asilia ikiwa ni pamoja na magonjwa na mambo mengine ambayo mtu mmoja mmoja, familia au ukoo wanashauriwa kutoa sadaka kwa sababu mbalimbali ambazo wanashauriwa na uongozi wa jadi.
Pango la Pali-Kyala, au kwa ufupi Likyala kama linavyojulikana na wenyeji wa huku, liko umbali wa km 2 hivi kusini mwa kitongoji cha Lyulilo mwambao mwa Ziwa Nyasa kuelekea kitongoji cha Ikombe. Pango la Likyala liko katika kitongoji cha Lyulilo, ambacho kiko katika kijiji cha Ikombe.
afu za Milima ya Livingstone zinaingia Ziwa Nyasa kuanzia Lyulilo na inaambaa kusini mpaka Manda na Mbamba Bay. Unaweza kufika pango la Likyala ama kwa kutembea kuambaa ufukweni kutoka Lyulilo au kwa mtumbwi kutoka mwalo wa Matema. Ni mwendo wa dakika 15 kwa mtumbwi unaotumia mota.
Umaarufu wa pango la Likyala unatokana na kwamba ni mahala pa matambiko ya kijadi. Linalindwa na wazee maalumu wa kimila wanaotoka Ikombe. Kihistoria ni mahala ambapo wazee walifanya matambiko ya kuombea mvua. Akisimulia umaarufu wa eneo hilo, Joseph (43) anaeleza kwamba wazee wa kimila walipokuja kufanya matambiko ya mvua, mara tu baada ya wao kumaliza matambiko, mvua zilinyesha.
Kwa maelezo ya Joseph na Charity (25) kuna maajabu ya kila aina hapo. Wakati mwingine unaweza ukakuta kuku wakizunguka zunguka maeneo hayo ingawa ni mbali kutoka kwenye makaazi ya watu. Anasisitiza Charity Ngalawa, ambaye ni nahodha wa boti iliyotupeleka, na mwenyeji wa Matema mwenye asili ya Manda, “ukimtamani kuku unayempata hapa na ukamchukua, ukamchinja na kumla, utadhulika.
Unaweza kupooza mwili au ukapata kichaa au hata kufa. Lazima watu watakaojua suala hilo mapema waharakishe kuwaona wazee wa kimila ili waweze kukuokoa.”
Inasemekana kuwa pango hilo ni refu na linafika mpaka Ukinga, Makete. Lakini kwa mujibu wa Joseph, ambaye amewahi kuingia kwenye pango hilo, pango ni kubwa mwanzoni lakini upenyo unakuwa mdogo baada ya mita zipatazo hamsini hivi.
Katika kumbukumbu zao kama zilivyokaririwa katika historia fupi ya kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Daosisi ya Konde 1891-1991, iliyohaririwa na mwaka 1991, Mwalimu Andalalisye Mwaihabi na wenzake wanaeleza jinsi ambavyo wamisionari wa kwanza walivyopata shida kupenyeza injili kwa sababu ya dini za kiasili ambazo zilikuwa zimejengeka katika jamii za wenyeji wa maeno haya. Pango la Pali-Kyala limeelezwa kama ni mahali ambapo Wakisi wa Ikombe walikuwa wakiabudu Mungu wao.
Umaarufu wa eneo hilo la pango unatokana pia na kuwepo kwa samaki wa mapambo katika kina kifupi cha ziwa. Hawa ni samaki wa rangi za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na; pundamilia, weusi, bluu, weusi na manjano. Hata bila ya uwa na mawani ya kuogelea majini, samaki hao wanaonekana.
Wageni wengi hufika eneo hilo li kuvua samaki wa mapambo. Wao na wavuvi wenyeji huwavua samaki hao bila udhibiti wowote na kuashiria kupungua kwa samaki wa aina hiyo. Ziwa Nyasa ni maarufu kwa samaki hao wenye rangi za kila aina na zinazovutia. Kama ilivyoelezwa awali, inakadiriwa kuwa kuna aina 700 hadi 1000 ya samaki wa aina ya cichlids katika ziwa, wengi wao hawapatikani duniani kote isipokuwa Ziwa Nyasa tu (endemic). Katika eneo la Matema samaki wa mapambo wanapatikana kwa wingi maeneo ya Likyala; kwa Katulemi, karibu na Lyulilo; na Isumba, kusini karibu na Ikombe. Wageni wengi huwatafuta samaki hao kwa ajili ya matankimaji yaliyotengenezwa kwa vioo kwa ajili ya maonesho (aquarium).
Maporomoko ya maji ya Mwalalo (Mwalalo Waterfalls)
Baada ya kukaa kwa muda, Matema kama mwanakijiji, nilipata kufahamu kwamba moja ya vivitio vya Matema ni maporomoko ya maji yaliyo katika Mto Mwalalo. Mwalalo ni moja ya mito inayoingiza maji katika Ziwa Nyasa karibu na Kitongoji maarufu cha Lyulilo.
Kuipata njia ya kuanza safari ya kwenda kwenye maporomoko ilitubidi, mimi na walioniongoza kwenda huko, Joseph Sinyangwe (43) na Mario Mwaitulo (25), twende kwa gari hadi lilipo tanki la maji la kijiji cha Matema, km 4 kutoka ufukwe wa Matema katika kitongoji cha Bulinda.
Ndipo safari inapoanza kupanda kupita kandokando ya Mto Mwalalo unaopita katika korongo kubwa katikati ya milima miwili. Kabla ya kuanza safari niliwauliza wenzangu ingechukua muda gani kufika kwenye maporomoko? “Sisi kawaida huchukua dakika 55.
Tukiwa na wewe inaweza ikachukua saa moja na nusu tu.” Nikawaelewa. Walikuwa na maana kutokana na umri wangu tungeenda polepole. Hawakunikatisha tamaa. Pamoja na kwamba waelekezi wangu hao walinitahadharisha ugumu wa safari, nilipigamoyo konde na kuwakumbusha kwamba umri ni namba tu!
Unaanza kuona ugumu wa safari mapema. Kwani ukiangalia huku na huko kingo zote mbili za mto ni miamba ya mawe iliyo wima. Kilichobaki ni kutafuta upenyo mahali unapoweza kuweka mguu huku ukishikilia mwamba ili usidondoke lakini upige hatua mbele.
Sehemu nyingine hakuna nafasi ya namna hiyo hivyo inabidi kupita kwenye maji ndani ya mto. Kwa kuwa ilikuwa wakati wa kiangazi, kina cha maji kilikuwa kimepungua. Sehemu nyingine maji yanafika katika magoti na sehemu nyingine kina ni kirefu na maji yanafika kifuani. Aina ya nguo na viatu kwa safari ya namna hiyo ni muhimu. Nguo na viatu vya mazoezi vinafaa kwa matembezi ya aina hiyo.
Itaendelea wiki ijayo…