UAMUZI wa Wizara ya Mifugo ikishirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wa kuteketeza kwa moto vifaranga hai vya kuku zaidi ya 6,000 umetushtusha.
Msingi wa kushtushwa kwetu na tukio hilo kwanza ni jinsi uteketezaji wake ulivyofanyika na pili hatua zilizozingatiwa na Wizara na TFDA kabla ya kuviangamiza vifaranga hivyo.
Tunatambua kwamba uteketezaji wa vifaranga hivyo ni kuzingatia sheria zinazokataza uingizaji wa vifaranga vya kuku kutoka nje ya nchi na tunapenda ieleweke kwamba kwa namna yoyote ile hatupingi utekelezaji wa sheria za nchi.
Hata hivyo, hoja yetu ni busara iliyotumika katika utekelezaji wa sheria hiyo na jinsi uteketezaji wenyewe ulivyofanyika.
Ni maoni yetu kuwa ingawa kilichofanyika ni utekelezaji wa sheria, maofisa husika wangeweza kutimiza matakwa hayo ya kisheria katika hali ya kificho ili kutoibua hisia tofauti miongoni mwa jamii.
Tunaamini kuwa kitendo cha kuchoma moto hadi kufa kiumbe hai chochote ambacho kinafanyika hadharani huibua hisia za huruma, maumivu na pengine ukatili kwa watu wanaokishuhudia.
Hisia za namna hiyo zinaweza kujenga dhana ya ukatili dhidi ya ndege na wanyama na pia zinaweza kuibua mvutano baina ya watekelezaji wa sheria na watetezi wa haki za wanyama.
Aidha, tunaamini kuwa katika tukio hilo lililotokea eneo la Namanga mkoani Arusha, maofisa wa serikali waliomkamata mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina la Mary Matia akiingiza vifaranga hivyo vyenye thamani ya Sh. milioni 12.5 walikuwa na kila sababu ya kumpa adhabu mbadala ya kuchoma vifaranga.
Imani yetu hiyo inajengwa katika msingi kwamba mfanyabiashara huyo anadai kuwa ana mkopo wa benki wa sh milioni 12 alizonunulia vifaranga hivyo.
Ni wazi kuwa hataweza kulipa mkopo huo kwa sababu msingi wa biashara yake umeteketezwa na huenda akaingia kwenye matatizo zaidi iwapo benki itaamua kutaifisha mali za wadhamini wa mkopo wake ili kufidia deni lake.
Wizara na TFDA ingeweza kumuadhibu mfanyabiashara huyu kwa kumpiga faini kulingana na uzito wa kosa alilofanya. Adhabu hiyo, kwanza ingemnusuru na hali ya kufilisika, pili ingeliingiza taifa mapato na pia ingeepusha uteketezaji wa vifaranga hai hadharani ulioibua hisia tofauti kwa jamii.
Kwa kuzingatia imani na mtizamo wetu kuhusu suala hili, tunaungana na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ambaye amekaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa sheria ya magonjwa ya mifugo namba 17 ya mwaka 2003 kifungu 8 (1), inayompa Waziri uwezo wa kukamata mifugo ama bidhaa za mifugo zilizoingia nchini kinyume na sheria cha 31 (1) 43 (a na b) na 61 (1) inaweza kurudishwa bungeni kufanyiwa mabadiliko ili utekelezaji wake usiibue hisia hasi kwa jamii.