Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017 katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhani, ambapo alisema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika kata husika.
Alisema idadi ya wapiga kura ndio inatoa bajeti ya mahitaji ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama karatasi za kura pamoja na idadi ya vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua wanne.
“Lakini pia kuna watu wa ziada kama wasimamizi wasaidizi wako ngazi ya kata na jimbo ambao wanahusika kusimamia zoezi la uchaguzi katika maeneo husika,” alisema.
Alifafanua kuwa gharama nyingine za uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka Tume kwenda kwenye halmashauri husika na kutoka halmashauri kwenda kwenye kata ambako uchaguzi unafanyika.
Gharama hizo pia zanahusu utoaji wa elimu ya mpigakura kupitia machapisho mbalimbali ya elimu ya mpigakura, maelekezo mbalimbali kwa watendaji wa uchaguzi.
“Kwenye uchaguzi huu mdogo bajeti yetu ni Sh bilioni 2.5. sio kwamba kila kata itatumia gharama sawa za fedha hizi, bali kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huu itatumia Sh milioni 150,” alisema Kailima.
Mwisho
Mahakama yamfutia kesi RC Adam Malima
Na Kulwa Mzee
-Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Chakula wa awamu ya nne, Adam Malima na dereva wake baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuomba kuondoa kesi dhidi yao.
Uamuzi wa DPP wa kuondoa kesi hiyo umekuja siku chache baada ya Malima kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Kesi hiyo jana ilikuja mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri.
Akiitaarifu mahakama Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kesi ilitakiwa kuendelea kusikilizwa lakini DPP amewasilisha hati ya kuiondoa.
“Mheshimiwa hakimu DPP kawasilisha hati ya kuondoa kesi hiyo chini ya kifungu cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 91(1). Anasema hana kusudio la kuendelea nayo hivyo anaomba iondolewe,”alidai.
Hata hivyo wakati kesi hiyo ikiondolewa mshtakiwa Malima hakuwepo mahakamani, lakini Dk. Amani Malima ambaye ni mdhamini wake alieleza mahakamani kwamba, mshtakiwa amepata udhuru wa kikazi yuko mkoani Mara.
Baada ya kusema hayo, Hakimu Mwijage alitaka Jamhuri waeleze sababu ya kuondoa kesi hiyo, lakini walishindwa na badala yake walinukuu kifungu hicho cha sheria kinachotoa mamlaka kwa DPP kufuta kesi.
Hakimu Mwijage alikubali hoja za Jamhuri na kutamka kwamba kesi dhidi ya washtakiwa wote wawili imeondolewa wako huru.
Washtakiwa katika kesi hiyo walikuwa wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kumzuia polisi kufanya kazi yake.
Washtakiwa hao, Malima na Ramadhani Kwagwande walifikishwa mahakamani Mei mwaka huu na kusomewa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Inadaiwa katika hati ya mashtaka kwamba, shitaka la kwanza linamkabili Ramadhani, anadaiwa Mei 15 mwaka huu maeneo ya Masaki kwa nia ya kukataa kukamatwa kwa kuegesha gari lenye namba T 587 DDL vibaya, alimjeruhi ofisa wa Kampuni ya Priscane Business Enterprises, Mwita Joseph na kumsababishia maumivu ya mwili.
Shitaka la pili la shambulio linamkabili Malima ambapo anadaiwa katika tarehe hiyo Masaki alimzuia Polisi H 7818 Abdul kufanya kazi yake ya kumkamata Ramadhani ambaye alifanya kosa la kujeruhi.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda tukio hilo maeneo ya Masaki karibu na Double Tree Hotel, baada ya kusomewa mashtaka, wote walikuwa wakiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala.
Washtakiwa walikuwa nje kwa dhamana yenye masharti kwamba kila mshtakiwa awe na mdhamini mmoja, mwenye barua ya utambulisho kutoka ofisi yoyote inayotambulika na wasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni tano.