MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema kuanzia leo kutakuwa na mvua kubwa ambayo itanyesha kwa siku tano mfululizo hususan katika mikoa ya pwani.
Mvua hiyo inakisiwa itakuwa na ukubwa wa milimita 50, kiwango ambacho ni kikubwa mno.
Jambo hili limekuja ikiwa ni siku tano zilizopita, ambako mvua kubwa ilinyesha katika Jiji la Dar es Salaam na kusababisha athari kubwa za watu kadhaa kupoteza maisha na uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Mvua hiyo ilisababisha shughuli nyingi za kijamii kusimama kwa muda kutokana na maeneo mengi kutopitika au kufikika kwa urahisi.
Wakati bado wananchi wa Dar es Salaam wanagugumia maumivu haya, TMA imesisita kuwa mvuna inayokuja ni kubwa zaidi ya ile iliyotangulia.
Siku zote waswahili wanasema heri kujenga ukuta kuliko kuziba ufa.
Kwa mfano katika Jiji la Dar es Salaam ambalo kwa namna moja au nyingine limekuwa likiathirika zaidi kutokana na maeneo muhimu ambayo yanapaswa kupitisha maji kuvamiwa na watu kisha kujenga bila kufuata utaratibu wowote.
Hali hiyo, imesababisha maeneo mengi ya katikati ya jiji kukumbwa na maji mara nyingi na kusababisha uharibifu mkubwa ambao kwa namna moja au nyingine unaweza kuepukika.
Si hilo tu, katika maeneo ya pembezoni kumekuwa na uvamizi mkubwa wa maeneo hatarishi ambayo wananchi wameamua kujenga nyumba za makazi au biashara huku mamlaka husika zikiwaangalia.
Tunasema hivyo kwa sababu katika mvua iliyonyesha wiki iliyopita tumehushudia namna ambavyo wananchi wa maeneo hayo walivyoathirika na maji mengi ambayo yalikosa njia ya kutokea.
Tukirejea kwenye tahadhari ya TMA, ambayo imeonyesha kuwa mvua hiyo itanyesha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na Pwani, huku visiwa vya Pemba na Unguja navyo vikiguswa na hali hiyo,ni wazi wananchi wa maeneo haya wanapaswa kuwa makini mno.
Mamlaka hiyo, imewataka wananchi wote kuzingatia ushauri huo ili kuepuka maafa ambayo yanaweza kutokea kwa kuchukua tahadhari  katika maeneo waliopo.
Tunatambua wananchi wengi ambao wanaishi maeneo mbalimbali, wanatambua athari za mvua katika makazi, ikizingatiwa kila kukicha Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwapa elimu.
Kwa miaka mingi tumeendelea kuwa mashuhuda namna ambavyo mvua hizi zinavyoathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja au zaidi, wakati mwingine hata Taifa kutokana na ukweli kwamba wapo wananchi wanaotegemea mazao mabayo huharibika vibaya au kusombwa na maji.
Kwa msingi huo, tunaamini Watanzania ni waelewa katika hili lazima waonyesha kuwa wako makini ili kuepukana na athari zinazoweza kutokea wakati huu.
Sisi MTANZANIA, tunaamini taarifa za TMA zimekuja wakati mzuri ambao unaweza kusaidia kunusuru maisha ya watu na mali zao endapo tutachukua hadhari.
Kwa msingi huo, tunaisisitiza mamlaka hii, ihakikishe inatoa taarifa za namna hii kila wakati  hasa kwa maeneo ambayo yanaweza kukumbwa na mvua hii ili kuepukana na maafa ya mvua zinazotarajiwa kunyesha.
Tunamalizia kwa kuwasihi wananchi na Watanzania kwa ujumla kujenga utamaduni wa kufuatilia matangazo ya hali ya hewa kila wakati.
Ndiyo maana tunasema tunasisitiza wananchi wa maeneo yote yaliyotajwa na TMA wazingatie ushauri huu kwa uzito wa kipekee ili kuepuka madhara.