Na JOHANES RESPICHIUS -DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi wanaoishi maeneo ya ukanda wa pwani kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha kuanzia Octoba 31 hadi Novemba 3, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, maeneo yatakayoathiriwa zaidi na mvua hizo ni mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na visiwa vya Pemba na Unguja.
Taarifa hiyo ilisema kuwa vipindi vya mvua kubwa zinazozidi milimita 50 zinatarajiwa kunyesha ndani ya saa 24. Kiwango cha juu kinakadiliwa kufikia asilimia 80.
“Baadhi ya maeneo ambayo yataathirika ni ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani pamoja visiwa vya Unguja na Pemba.
“Mvua hiyo inatarajiwa kusambaa katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Lindi kuelekea siku ya Ijumaa Novemba 3, mwaka huu,” ilisomeka taarifa hiyo.
Taarifa ilisomeka zaidi kuwa hali hiyo inatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua (Inter Tropical Convergency Zone –ITCZ) katika maeneo hayo.