26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

KENYATTA: NITAMTAFUTA RAILA BAADA YA UCHAGUZI

NAIROBI, KENYA

Uhuru kumtafuta Raila

RAIS Uhuru Kenyatta amesema akiwa kiongozi anayejua wajibu wake, atamtafuta kiongozi wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, baada ya uchaguzi kama moja ya njia za kuiunganisha nchi.

Kiongozi huyo alisema hayo jana mara baada ya kupiga kura yake katika Shule ya Msingi Mutomo, Jimbo la Uchaguzi la Gatundu Kusini.

“Kwa kiongozi mwenye kufahamu wajibu wake, lazima atafute suluhu na huo ni mpango nilionao,” alisema Kenyatta akizungumzia mkakati wake baada ya uchaguzi.

Aidha Kenyatta aliyeambatana na mkewe Margaret na mama yake Mama Ngina, alieleza matumaini yake kuwa matokeo ya uchaguzi yatamaliza mkwamo wa kisiasa ulioshuhudiwa kwa miezi michache iliyopita.

Kenyatta ambaye jana aliadhimisha siku yake ya 56 ya kuzaliwa, alikiri kuwa Kenya imeathirika vibaya na ukabila, na alisisitiza kuwa kushiriki au kutoshiriki uchaguzi ni haki ya mtu inayopaswa kuheshimiwa.

Wakati Kenyatta akipiga kura katika Jimbo la Uchaguzi la Gatundu Kusini, naibu wake William  Ruto alipiga katika Shule ya Msingi Kosachei, Jimbo la Uchaguzi la Turbo, dakika chache baada ya saa nne kamili asubuhi.

Ruto aliyeambatana na mkewe Rachel, alieleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wapigakura wakati akipiga kura katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Alitetea hatua ya chama chake kuendelea na uchaguzi licha ya kujitoa kwa Raila, akisema yeyote ana haki ya kikatiba ya kupiga kura au kususa.

“Ni haki ya kila mtu kupiga kura au la. Tunawaomba wafuasi wetu wajitokeze kwa idadi kubwa kutupigia kura. Jubilee inastahili fursa nyingine ya kuongoza nchi,” alisema.

 

HALI ILIVYOKUWA

Mwitikio mdogo wa wapigakura, mchezo wa ‘paka na panya’ baina ya waandamanaji na polisi, watu kuuawa na kujeruhiwa, ufungaji wa mitaa inayoelekea vituo vya kupiga kura, ni miongoni mwa mambo yaliyoshuhudiwa wakati Wakenya wakipiga kura katika uchaguzi wa marudio wa urais jana.

Baadhi ya vituo vilikuwa vitupu na vingine kufungwa, hasa maeneo ya upinzani, huku Jaji wa Mahakama ya Juu, David Maraga akijitokeza kupiga kura.

Uchaguzi huo umefanyika licha ya kujitoa kwa Raila aliyeugomea, akisisitiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haijajiandaa kuuendesha kwa uwazi na haki.

Kwa ujumla uchaguzi licha ya mwitikio mdogo wa wapigakura kulinganisha na ule wa Agosti 8, ulifanyika kwa amani ukiondoa maeneo ambayo ni ngome za upinzani, kama vile Nyanza, Nairobi na Mombasa , ambako vifo na majeruhi vimeripotiwa.

 

Raila ashinda nyumbani kwake

Raila alitumia siku nzima jana akiwa nyumbani kwake Karen jijini Nairobi, ambako kwa wakati fulani alionekana akiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama chake cha ODM, Junet Mohammed.

Katika picha ambazo Mohammed alizituma katika mtandao wa jamii, wawili hao walionekana kwenye kochi wakiwa na magazeti mbalimbali ya siku hiyo.

 

Jaji Maraga ajitokeza

Jaji Mkuu David Maraga, alisafiri kwenda kijijini kwao katika Kaunti ya Nyamira, ambako alipiga kura katika uchaguzi wa urais wa marudio.

Hatua hiyo ya Maraga inapuuza wito wa Raila wa kulitaka taifa hilo lisusie uchaguzi huo kutokana na IEBC kutokuwa tayari kwa kazi hiyo.

Septemba Mosi mwaka huu, Jaji Maraga aliweka historia na majaji wenzake watatu, kwa kufuta matokeo ya urais ya Agosti 8, uamuzi ambao ulilalamikiwa vikali na Kenyatta.

Juzi Jumatano alijikuta akitangaza kuwa Mahakama ya Juu haitoweza kusikiliza kesi ya kuzuia uchaguzi huo kufanyika jana baada ya akidi ya majaji kutotimia kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ugonjwa, usalama na kile kinachoelezwa visingizio vingine.

Maraga, aliyeambatana na mkewe, alipiga kura katika kituo cha Bosose, Jimbo la Mugirango Magharibi alikopiga kura saa 7.55 mchana.

Kabla ya kupiga kura, Jaji Maraga alizungumza kwa muda mfupi na mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Nyamira, Jerusha Momanyi.

“Nishamaliza kilichonileta hapa na hivyo naweza kuondoka,” alisema baada ya kupiga kura, akikataa kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari.

 

Watatu wauawa

Watu watatu wameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa, wakati polisi walipopambana na waandamanaji sehemu mbalimbali za nchi jana.

Mtu mmoja alifariki dunia na wengine wanane kulazwa katika hospitali mbalimbali katika kaunti za Kisumu na Migori kufuatia mapigano baina ya waandamanaji na polisi.

katika eneo la Mto Athi, mwanafunzi wa kidato cha pili alipigwa risasi na kufariki dunia, huku wengine wawili wakilazwa hospitali kwa majeraha ya risasi baada ya polisi kuwarushia risasi za moto waandamanaji.

Mwili wa mvulana huyo uko katika Hospitali ya Mutonguni, Mto Athi, huku vijana wengine; John Mutua na Mildad Lodenyi wakitibiwa majeraha baada ya risasi kujikita miguuni mwao.

Mutuia alisema alikuwa akielekea nyumbani wakati alipopigwa risasi, huku Lodenyi akidai alishinda nyumbani wakati polisi walipovamia na kumpiga risasi baada ya kumkokota hadi barabarani.

Polisi waliwatimua waandishi wa habari waliokuwa wakiwahoji waathirika.

Majeruhi mwingine, Bernard Osiako, alisema kuwa alikuwa njiani wakati akipigwa risasi begani katika eneo la Muskiti karibu na Kondele.

“Ofisa wa polisi alinipiga risasi nikiwa katika barabara ya juu na sikuwa sehemu ya waandamanaji,” alisema Osiako, ambaye ni fundi magari.

Aidha majeruhi wanne wanelazwa katika Hospitali ya Rufaa na Ufundishaji Jaramogi Oginga Odinga kwa majeraha ya risasi, huku George Odhiambio anayedaiwa kupigwa risasi eneo la Mamboleo, akifariki dunia kwa majeraha.

 

Mchezo wa ‘paka na panya’

Katika maeneo ya Nairobi yaliyo ngome za Raila kama Kibera na kwingineko, waandamanaji walifunga barabara na vituo vya kura.

Polisi walilazimika kuzifungua barabara na vituo hivyo vilivyojazwa mawe na kukabiliana na waandamanaji kwa staili ya ‘kimbiza nikukimbize’, hadi walipolazimika kuomba msaada wa askari zaidi baada ya kuzidiwa.

Hali kama hiyo ilijitokea katika maeneo ya mji wa Mombasa, ambako waandamanaji walivunja vioo vya vituo vya kupiga kura, huku vingine vikijazwa vinyesi. Hata hivyo, polisi baadaye waliweza kudhibiti hali katika maeneo hayo.

 

Polisi wajitetea

Inspekta Jenerali wa Polisi, Joseph Boinnet, amekana polisi kutumia nguvu kupita kiasi kuyakabili makundi yaliyojaribu kuvuruga uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupiga kura yake katika Shule ya Msingi Lang’ata, Kaunti ya Nairobi, Boinnet alisema kuwa uchaguzi umeenda vyema na kwa amani, isipokuwa sehemu za Nyanza, Kibera na Mathare.

“Ripoti zinaonyesha kuna magenge ya wahuni yanayojaribu kuvuruga uchaguzi na polisi wanawakabili kwa mujibu wa sheria,” alisema Boinnet.

 

Mawakala 40 waitosa Jubilee

Maeneo yanayofahamika kama ngome za upinzani ya Nyanza, Pwani, mwitikio ulikuwa mdogo au uchaguzi kutofanyika kabisa, huku mawakala 40 wa Jubilee wakiingia mitini mjini Mombasa.

Waziri wa Utalii, Najib Balala, alisema mawakala hao ambao walipata mafunzo, pamoja na kulipwa posho, wamekiangusha chama hicho na watakiona cha moto.

Akizungumza baada ya kupiga kura huko Mwembe Tayari, Balala alisema mawakala hao watachukuliwa hatua kali.

Katika ngome za Jubilee, mwitikio haukuwa mbaya kadiri muda ulivyoenda. Foleni ilishuhudiwa maeneo ya Kati na Eldoret  baada ya awali asubuhi mwitikio kuwa mdogo mno.

Hata hivyo, kwa ujumla wake bado mwitikio huo katika ngome za Jubilee ulikuwa wa chini tofauti na ule wa uchaguzi wa Agosti 8.

 

Uchaguzi waahirishwa kaunti nne

Tume ya Uchaguzi iliahirisha uchaguzi katika kaunti nne za Nyanza kutokana na changamoto za uslaama.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, alisema uchaguzi umeshindwa kufanyika maeneo ya Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya kutokana na mandamano yaliyofanywa na waandamanaji wa Nasa.

“Kwa sababu hizo, marudio hayo sasa yatafanyika kesho iwapo usalama utarudi hali ya kawaida,” alisema Chebukati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles