Na SAFINA SARWATT -KILIMANJARO
KADA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Kilimanjaro, Fredi Mushi amekihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mushi ambaye alitangaza kujiunga na CCM mjini Moshi jana, kabla ya kuhamia Chadema mwaka 2015, alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumzia sababu za uamuzi huo, Mushi alisema alihama mwaka 2015 wakati huo kufuata mafuriko ya Chadema na sasa amerudi baada ya kugundua alikuwa amefuata mkumbo.
“Huyo atakayesema nimenunuliwa sina bei wala sinunuliwi na kama wanavyofikiria kwa sababu hata nilipohamia Chadema sikununuliwa zaidi ya kufuata mkumbo na mafuriko ambayo hayakuwa na Ilani.
“Leo hii nimerejea kama mwana mpotevu aliyeamua kurudi nyumbani na kuomba msamaha. Naomba katibu unipokee sitarudia kosa,”alisema Mushin a kuongeza:
“Baada ya kimya cha muda mrefu nimekaa chini nikatafakari kwa kina nikagudua kwamba sipo mahali sahihi, nimegundua Chadema hakina ilani.
“Kilio cha vijana ilikuwa kupigania raslimali za nchi hii lakini bahati nzuri Mungu amesikia na kumleta Rais Dk. John Magufuli, vijana wenzangu tumuungune mkono rais wetu katika kupambana na vita dhidi ya ufisadi”.
Naye Katibu wa CCM, Jonathan Mabihya aliyempokea Mushi ofisini kwake, alizungumzia madai ya Chadema kusema kwamba chama hicho kinanunua wanachama wake wakiwamo madiwani.
Alisema masuala ya siasa ni utashi wa mtu mwenyewe.
“Tangu nizaliwe sijawahi kuona binadamu ananuliwa, hilo nimekuja kusikia kwa hao ndugu zangu wa upinzani, sijajua thamani halisi ya bei ya binadhamu, kama wao wananunua wanachama watuambie.
“Wanachama wao wakihamia CCM wanaambiwa kanunuliwa lakini wa CCM akihamia kwao hajanunuliwa inawezekana ni biashara yao kununua watu,” alisema Mabihya.
Alisema suala la wanachama kuhama kwenda chama kingine ni utashi wa mtu na kwamba watambue CCM haina muda mchafu wa kukaa na kupanga bei ya kununua mtu.
“CCM haina muda mchafu wa kukaa na kupanga bei za kununua watu kama nyanya sokoni nawatahadharisha ndugu zangu kwamba CCM si chama cha biashara ya kununua watu.
“Ilani ya chama ni kutekeleza miradi mbalimbali katika jamii hivyo watu waache siasa za majungu kwa sababu hatuna nafasi ya kusikiliza majungu,” alisema.