NA AMON MTEGA-Â Â SONGEA
MWENYEKITI wa Chama cha Walimu (CWT) Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Mathias Mwanjisi, amezitaka baadhi ya taasisi zinazojihusisha na kuwakopesha fedha watumishi wa Serikali ambao robo tatu ni walimu waache tabia ya kuwachukulia watumishi hao kadi za benki, ili kuondoa udhalilishaji juu ya watumishi hao.
Wito huo aliutoa jana, wakati akizungumza kwenye mkutano wa kawaida wa chama hicho ulioambatana na uchaguzi wa kuziba mapengo mbalimbali ya uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikiwadhalilisha watumishi, hasa walimu kwa kuwachukulia kadi zao za benki, jambo ambalo limekuwa likiwafanya watumishi hao kuwa wanyonge katika maeneo yao ya kazi.
Alisema kuanzia sasa uongozi wa chama hicho utazitafuta taasisi hizo na kukaa nazo meza moja ili kuondoa hali hiyo inayowakuta baadhi ya walimu pindi wanapokuwa wamekwenda kukopa fedha kwenye taasisi hizo.
Aliwageukia watumishi hao kuwa nao wajifunze kuacha kuchukua mikopo bila kuwa na tija yoyote, kwani kufanya hivyo ni kujikandamiza kimaendeleo na mwisho wa siku wanajikuta wanadhalilika bila sababu za msingi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Tume ya Utumishi ya Walimu Tanzania (TSC), Manispaa ya Songea, Gosbert Nchimbi, alisema baadhi ya walimu wamekuwa wakikiuka tarabu za kazi kwa kufanya utoro makazini.
Alisema hadi sasa kuna kesi 23 ambazo zinawakabili walimu na mwajiri wao ambazo zinaendelea kuzungumzwa.
Naye mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Wanda Marwa, alisema changamoto hizo zinaikuta idara ya walimu kutokana na ufinyu wa vipato vilivyopo.