Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema anayo orodha ya watu mashuhuri, viongozi wastaafu na wabunge wanaojishughulisha na ujangili hivyo atahakikisha analala nao mbele.
Dk. Kigwangalla amesema licha ya kuwa na orodha hiyo anaendelea kuwafuatilia wengine ambapo katika hilo hataangaliwa mtu kwa sura yake.
“Tunawafuatilia na tukijiridhisha kwamba wanahusika na vitendo vya ujangili tutalala nao mbele, hatutakuwa na huruma kwa sababu tumepewa kazi ya kulinda rasiliamali za nchi na tutaifanya kwa uaminifu na uadilifu mkubwa,”amesema.
Dk. Kigwangalla amesema jitihada kubwa zimefanywa na serikali kudhibiti vitendo vya ujangili hivyo ni lazima na wao wakiwa viongozi wapya waziendeleze kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kama kuna mtu alikuwa anafikiria kwamba uongozi umebadilika na labda tutalegeza katika eneo la kukamata majangili, hapana, ndiyo kwanza tunazidi kukaza nati kuimarisha kitengo chetu cha intelijensia, ndani ya nchi na nje ya nchi ili kudhibiti ujangili ipasavyo,” amesema.