DAMASCUS, Syria
WIZARA ya Ulinzi ya Urusi imesema kwamba kwa mara ya kwanza Serikali ya Marekani imethibitisha kuwa magaidi wanaofanya mashambulizi katika Jimbo la Idlib nchini Syria, hawatumii silaha za kawaida pia wanatumia na za kemikali.
Taarifa hiyo imetolewa jana na msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Jenerali Igor Konashenkov, wakati akizungumzia ripoti iliyotolewa na Marekani na akasema kwamba katika maelezo hayo kuna kikundi kinachoitwa Hayat Tahrir al-Sham ambacho kinashirikiana na kingine cha Jabhat al-Nusra, kikundi ambacho kilidhibitiwa nchini Urusi kutokana na kwamba kilikuwa kikitumia silaha nzito na vifaa vilivyotengenezwa na silaha za kemikali.
“Ningependa kueleza kuwa Serikali ya Marekani kwa mara ya kwanza imekubali rasmi kuwa magaidi kutoka kundi la Jabhat al-Nusra, hawana tu silaha nzito bali pia ningependa kusisitiza kwamba wanatumia silaha za kemikali katika Jimbo hili nchini Syria ili kutekeleza mashambulizi ya kigaidi, jambo ambalo kwa mara nyingi tumekuwa tukilionya katika kulipigia kelele katika ngazi mbalimbali za kimataifa,” alisema Konashenkov.
Msemaji Mkuu huyo aliongeza kwamba tukio moja la matumizi ya silaha za kemikali lilitokea katika eneo la Khan Shaykhun lililopo katika Jimbo hilo la Idlib na lawama zikaelekezwa na Marekani kuwa lilifanywa na majeshi ya Syria jambo ambalo halikuwa kweli.
“Wakati wapiganaji ambao kwa kweli walifanya mashambulizi hayo tulikuwa tukiwataja kuwa wana uhusiano na kundi la Jabhat al-Nusra, lakini Marekani ilikuwa ikitilia shaka. Lakini sasa, taarifa ya Idara ya Serikali ya Marekani imeweka kila kitu wazi kwamba kundi la ugaidi la Jabhat al-Nusra ambalo lilikuwa na ushirikiano pia Al-Qaeda ambalo lilisambaratishwa nchini Urusi ndilo linalotumika kutumia silaha za kemikali ili kuteketeza maisha ya raia wasio kuwa na hatia nchini Syria,” alisema Konashenkov.
Katika hatua nyingine, msemaji huyo aliongeza kuwa bado haijulikani kwanini Serikali ya Marekani inahitajika kutumia makombora ya gharama kubwa ya kushambulia ndege ya Syria ya Shayrat. Amesisitiza kuwa wangeweza kutumia vizuri zaidi mamilioni hayo ya dola kwa kutoa migomo kwa magaidi wa Jabhat al-Nusra.
Kwa upande mwingine Jenerali huyo ametupilia mbali madai ya Serikali ya Marekani ya kwamba majeshi ya Urusi ndiyo yalikuwa yakitumia silaha hizo katika makazi ya raia.