NA CHRISTOPHER MSEKENA
KUFUATIA changamoto mbalimbali ambazo shindano la urembo nchini (Miss Tanzania) limekuwa likipitia, kamati ya shindano hilo imelazimika kufanya jambo lililopokewa kwa mitazamo tofauti na washika dau wa urembo.
Changamoto hizo zimepeleka kamati ya shindano kufanya uteuzi wa mrembo ambaye wiki hii amekwenda China kuliwakilisha Taifa kwenye mashindano ya 67 ya urembo wa dunia yatakayofikia kilele Novemba 18, mwaka huu, kwenye ukumbi wa Sanya City Arena, nchini humo.
Mrembo Julitha Kabete, mwenye miaka 21, amepata bahati hiyo ya kuteuliwa kufuatia shindano la Miss Tanzania kutofanyika mwaka huu, kutokana na changamoto kadha wa kadha.
Julitha Kabete Alhamisi wiki hii, alikabidhiwa bendera na mwakilishi wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Habiby Msammy, katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt, jijini Dar es Salaam na kwenda kushindana na warembo 120 kutoka mataifa mbalimbali.
Wasifu wa mrembo huyu unakidhi. Unampa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya dunia, kwani amekuwa mwingi wa tabia njema na mwerevu aliyeweza kupenya kwenye mashindano kadhaa ndani na nje ya Tanzania.
Mwaka jana Julitha alishinda shindano la Miss Dar City Center, Miss Ilala mpaka akaingia kwenye tano bora ya warembo wa Miss Tanzania 2016, hali kadhalika alishiriki kwenye shindano la urembo Afrika, ambapo alifanya vyema na kujipatia dili la kuwa balozi wa mabadiliko ya hali ya hewa.
Hivyo kwa wasifu huo ambao sina shaka anao, kamati ya shindano la Miss Tanzania ikampa jukumu la kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya dunia, hivyo kuwa mrembo wa 23 wa Tanzania kutuwakilisha kwenye shindano hilo.
Lakini ubora wa mrembo wetu, ambaye ni lazima kama Watanzania tumpe sapoti, mtindo wa kumpata umeacha maswali kwa wadau wa urembo nchini, huku wengi wakionyesha kutokukubaliana na mchakato huo, kwani inaonekana warembo wengine hawajatendewa haki.
Ili kuepusha lawala kama hizi, ni lazima kamati ya shindano la Miss Tanzania ijipange upya na kuhakikisha jambo hili la kuteua mwakilishi wa Miss World halijirudii tena, bali shindano lifanyike na kutoa usawa kwa warembo wote wenye sifa kuwania nafasi hiyo.