NA WAANDISHI WETU, MTWARA
TATIZO la ajira nchini limeanza kuchukua sura mpya baada ya baadhi ya wakazi wa vijiji vilivyopo mkoani Mtwara ‘kununuliwa’ kwa ajili ya kwenda kushiriki zoezi la upigaji kura wa kuwachagua viongozi wa Msumbiji, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 15 mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa zaidi ya mwezi mmoja umebaini kuwa, idadi kubwa ya wakazi wa vijiji vya Msimbati, Madimba, Chipuputa na vijiji vingine vilivyopo Wilaya ya Nanyumbu wamekubali kuukana utaifa wao ili kupewa vitambulisho vya wapiga kura vya Mtwara.
MTANZANIA Jumatano limefanikiwa kuwaona maofisa uchaguzi kutoka Msumbiji wakiendesha zoezi la kuwaandikisha na kuwapa vitambulisho vya kupigia kura baadhi ya wananchi wa Tanzania kwa madai kuwa ni raia wa nchi hiyo waliolewa nchini.
Mmoja wa maofisa hao ambaye alizungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini kwa madai kuwa si msemaji wa suala hilo, alisema kuwa kazi kubwa wanayoifanya ni kuwaandikisha raia wao wanaoishi kwenye vijiji hivyo na si vinginevyo.
“Tunao raia wa nchi yetu ambao wamelowea Tanzania kwa muda mrefu, hatuoni sababu ya kuwanyima haki yao ya kuchagua na ndio maana tumewafuata huku kuwaandikisha ili kuwapa nafasi ya kuchagua kiongozi wao kwenye uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba, sidhani kama tumevunja utaratibu,” alisema ofisa huyo.
Pamoja na ofisa huyo kutoa maelezo hayo, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya viongozi na wakazi wa vijiji husika ili kujua ukweli wa mambo, ambapo wengi wao walikiri kuwa zoezi hilo mbali ya kuwalenga wanaoitwa raia wa Msumbuji waliolowea Tanzania, lakini pia linawagusa raia wa Tanzania ambao hukubali kujiandikisha na kupewa vitambulisho vya kupiga kura ili iwe rahisi kwao kwenda kufanya biashara nchini humo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimbati, Salum Athuman Tostao, alisema ni kweli maofisa hao walikuwa wakizunguka katika vijiji wakiwaandikisha wananchi na kuwapatia vitambulisho hivyo vya kupigia kura.
“Katika kijiji changu hawajajiandikisha watu wengi sana, ila vijiji vingine kama Madimba huko ndiko walikojiandikisha wengi zaidi, sisi viongozi tulishangazwa na tukio hilo, tulishindwa kufahamu nini kinaendelea,” alisema Tostao.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Madimba, Said Ngumbo, alikiri kufika kwa maofisa hao kutoka Msumbiji hata hivyo, alisema walimwambia kuwa wana baraka zote za Serikali ya Tanzania.
Aidha, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Nanyumbu, Shaban Mbarouk, alisema zoezi hilo limehusisha idadi kubwa ya wa
wa eneo lake na kwamba maofisa hao walikuwa wakiwauliza wananchi maswali machache kwa lengo la kuwatambua raia wao, lakini ukweli ni kwamba wengi walioandikishwa na kupewa vitambulisho ni Watanzania.
“Unajua hao maofisa wa Msumbiji walikuwa wakiwauliza wananchi kama wanafahamu kijiji chochote cha Msumbiji, mtu akitaja kijiji chochote cha nchi hiyo anaandikishwa na kupewa kitambulisho, huu ni utaratibu mbovu kabisa ambao umesababisha Watanzania wengi kupachikwa uraia wa Msumbiji unaowapa nafasi ya kupiga kura nchini humo,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Festo Kiswaga, alithibitisha kuwapo kwa jambo hilo, ambapo alidai kuwa baada ya kugundua hali hiyo ofisi yake ilianza kuchukua jukumu la kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili kuepuka kurubuniwa.
Alisema kuwa wamewaeleza wakazi wa vijiji vilivyokumbwa na jambo hilo kwamba, hatua yao ya kujiandikisha kama wapiga kura wa Msumbiji, inawaondolea sifa ya kuchagua viongozi wao kwa upande wa Tanzania.
“Unajua vijana wengi walikuwa wanalenga kupata vitambulisho vya Msumbiji ili waweze kuingia huko kirahisi na kwenda kufanya biashara, lakini pia wengine walijiandikisha kwa kutokujua, hili ni tatizo ambalo tulilitambua na kuanza kutoa elimu kwa wananchi na kuwaamuru waliochukua vitambulisho hivyo wavirudishe kwa hiari yao,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Ponsiano Damian Nyami, alisema zoezi la maofisa wa uchaguzi wa Mtwara kuandikisha watu wao kwa ajili ya kupiga kura wanalijua.
Nyami alisema hana uhakika kama wapo baadhi ya Watanzania wameandikishwa kwenye zoezi hilo, ingawa inawezekana ikawa hivyo na kwamba ofisi yake kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya wote wa mkoa huo watahakikisha wanalifanyia kazi ili kuepusha watu wengi kurubuniwa.
“Tunazo taarifa za watu hawa kutoka Msumbiji, tunachokijua wanaandikisha watu wao, zoezi hili limekuwa likifanyika duniani kote, si vibaya kwa nchi kuwaandikisha wananchi wao waliopo kwenye nchi mbalimbali, lakini hata hilo la raia wetu kuandikishwa linawezekana, nikiwa kama Kaimu Mkuu wa mkoa nitahakikisha hilo tunalifanyia kazi hata mkuu wangu akirudi nitamueleza suala hili,” alisema Nyami.
Aidha, aliweka wazi kuwa suala hilo haliwezi kuepukika kwenye mikoa yote iliyopo mipakani kutokana na nchi kutokuwa na vitambulisho vya Taifa vinavyomtambulisha raia halali wa nchi hii.
“Ni ngumu kwa nchi hii kuzuia hali hiyo kutokana na kukosekana kwa vitambulisho vya taifa, Wasukuma wanatumia neno getegete na sisi Wafipa tunatumia neno tometome ikiwa na maana kitu halisi chenye uhalisi unaostahili, sasa kwa nchi yetu ni ngumu kumjua Mtanzania tometome na getegete,” alisema Nyami.
Alisema suala hilo linaweza kutua kwenye maeneo mengi yaliyo mipakani kutokana na vijana wengi kukosa shughuli za kufanya, ambapo hawaoni tabu kurubuniwa kwa fedha kidogo ambazo wanaamini zitakidhi mahitaji yao.