NA VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM
HATIMAYE mtuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi ambaye pia mmiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Habinder Singh Seith, ameanza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Hatua ya kupatiwa matibabu kwa kigogo huyo inatokana na agizo la Mahakama ya Kisutu baada ya Wakili wa mshtakiwa, Joseph Makandege kudai kuwa mteja wake yupo hatarini kutokana puto alilonalo tumboni ambalo lineweza kupasuka ikiwa hatapatiwa matibabu tangu aliposhikiliwa.
Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa Seth alifikishwa hospitalini hapo Ijumaa wiki iliyopita na maofisa wa magereza na bado anaendelea na matibabu.
“Alipelekwa pale katika Kitengo cha Magonjwa ya Dharura, alitibiwa lakini sina uhakika kama alilazwa au waliondoka naye baada ya kupata matibabu,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakuwa tayari jina lake kutajwa gazetini kwa sababu za usalama.
MTANZANIA lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha ambaye alithibitisha kutibiwa kwa kigogo huyo wa IPTL.
“Ni kweli tulimpokea lakini hakulazwa kama ambavyo inasemekana, alipatiwa matibabu na kuruhusiwa. Lakini hii ni kesi ipo mahakamani ni vema uwatafute wasemaji wa jeshi hilo kwa taarifa zaidi,” alisema Aminiel.
Baada ya majibu hayo, gazeti hili lilimtafuta Ofisa Habari wa Jeshi hilo, Lucas Mboje ambaye alimtaka mwandishi kuwasiliana moja kwa moja na Mkuu wa Gereza la Segerea ambako Sethi amewekwa mahabusu.
“Ni vigumu mimi kujua juu ya hilo kwa sababu tunasimamia magereza nchi nzima… mkuu wa gereza yupo karibu zaidi na wafungwa na mahabusu, yeye atakupatia taarifa ya uhakika,” alisema.
Mkuu wa Gereza la Segerea, George Kavishe alithibitisha Sethi kupatiwa matibabu Muhimbili.
“Kimsingi si kwamba hatukutaka atibiwe huko bali kuna utaratibu ambao lazima ufuatwe na ndiyo maana tulimpeleka kwanza Amana akafanyiwa uchunguzi na ilipoonekana kuna ulazima kumpeleka Muhimbili akapewa rufaa kama ilivyo kwa wagonjwa wengine wote.
“Ameanza kupatiwa matibabu hapo muda sasa hali yake ni nzuri… lakini kuhusu vipimo na majibu siwezi kuweka wazi kwa sababu ni siri kati ya mgonjwa na daktari wake,” alisema.
Hivi karibuni, mawakili wa bilionea huyo waliiomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumruhusu mteja wao aende kutibiwa nje ya nchi kwa kile walichoeleza kwamba anasumbuliwa na uvimbe ‘baloon’ tumboni hali iliyosababisha akose usingizi siku nne.
Hata hivyo ombi hilo lilikataliwa na mahakama hiyo, badala yake iliamuru aende kutibiwa Muhimbili. Kabla ya kufikishwa Muhimbili alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Amana.
Seith anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi pamoja na mfanyabiashara James Rugemalira wa Kampuni ya VIP. Hadi sasa wote wako mahabusu.