31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

PONDA APEWA SIKU TATU KUJISALIMISHA POLISI

Na FERDNANDA  MBAMILA-DAR ES SALAAM


KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ametoa siku tatu kwa Katibu wa Jumuya ya Kiislamu na Msemaji wa Shura ya Maimam, Sheikh Ponda Issa Ponda, kujisalimisha mwenyewe.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema ikiwa Ponda atashindwa kujisalimisha mwenyewe, watamtafuta ili wamkamate na kumchukulia hatua za kisheria.

“Ponda ametoa lugha za kukejeli shughuli za Serikali, kitendo ambacho ni kinyume  na taratibu za nchi, pia anamakosa mengine ya jinai,”alisema Mambosasa.

Alisema pamoja na wito huo tayari askari polisi wametumwa kumtafuta kila kona. “Ninaomba aje mwenyewe kujisalimisha kituoni kwetu ili tuweze kumhoji, itakua vizuri zaidi kuliko kusubiri kukamatwa,”alisema Mambosasa.

Awapiga polisi chenga

Juzi polisi walivamia mkutano wake na waandishi wa habari kwa nia ya kumkamata, lakini hawakufanikiwa badala yake wakaondoka na baadhi ya waandishi.

Askari hao walifika saa 4:45 asubuhi katika hoteli moja iliyopo Kariakoo ambayo Sheikh Ponda alikuwa akifanyia mkutano huo wakiwa kwenye magari mawili.

Muda wanafika eneo hilo, ilikuwa ni dakika chache tangu Sheikh Ponda kuondoka eneo hilo baada ya kumaliza mkutano wake.

Ponda alifika kwenye hoteli hiyo saa 3:45 asubuhi na kuwasubiri waandishi na saa 4:10, alianza mkutano wake ambao ulitumia dakika 20 na kuisha.

Saa 4:45, aliondoka hoteli hapo huku baadhi ya waandishi na wenyewe wakaondoka.

Mara baada ya kuondoka, polisi hao walivamia eneo la mkutano huo na kuwakataza waandishi wa habari kutotoka ndani ya ukumbi huo mpaka watakapompata Sheikh Ponda.

Baadhi ya askari walifanya ukaguzi wa hoteli nzima ili kuangalia kama amejificha au laa, huku wengine wakiwa wamebaki na waandishi kwenye ukumbi ambao mkutano ulifanyika.

“Hakuna mwandishi yeyote kutoka ndani ya hoteli hii mpaka tumpate Sheikh Ponda, mliopo ndani hakuna kutoka,”alisikika askari mmoja akiwaambia waandishi.

Baada ya kufanya ukaguzi huo na kushindwa kumpata Sheikh Ponda, polisi waliwaruhusu baadhi ya waandishi kuondoka katika hoteli hiyo huku wengine wakiambiwa waende Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano.

Kesi za Ponda

Ponda kwa miaka ya hivi karibuni amekuwa na kesi mbalimbali anazofunguliwa na polisi maeneo mbalimbali nchini.

Mwaka 2012, Ponda alidaiwa kuvamia Uwanja wa Markaz uliopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam akiwa yeye pamoja na wafuasi wake.

Polisi walimkamata na kumfikisha mahakamani na kusomewa mashtaka matano ambayo ni pamoja na kula njama, kujimilikisha mali, kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Markaz, wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh milioni 59 na shtaka la uchochezi.

Hata hivyo, alihukumiwa kwenda jela mwaka mmoja ambapo mwaka 2013 alitoka na kuingia kwenye mgogoro mwingine na serikali ambao ni pamoja na kudaiwa kuwashawishi waislamu wasikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwa madai kuwa zimeundwa na Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata), ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali yake.

Alidaiwa kuwaagiza waumini hao kuwa endapo watu hao watajitokeza kwao na kujitambulisha kwamba ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha wawapige.

Kauli hiyo aliitoa akiwa katika eneo la Uwanja wa Ndege, Morogoro, ambapo pia alidaiwa  kuwaambia Waislamu kuwa Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi ili kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi hao ni Waislamu.

Alidaiwa kuwaambia wafuasi wake kuwa Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa huko ni Wakristu.

Katika kesi hiyo, polisi waliimarisha ulinzi mkali na kutumia usafiri wa helikopta ili kumpeleka mahakamani katika mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Morogoro kesi yake ilipokua ikitajwa.

Hata hivyo, serikali ililazimika kumnyima dhamana wakati kesi hiyo ilipokua inaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles