26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SALAH AIPELEKA MISRI KOMBE LA DUNIA

CAIRO, Misri

MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Mohamed Salah, juzi ameisaidia timu yake ya taifa ya Misri kufuzu michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Urusi.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Alexandria, Misri ilikata tiketi ya michuano hiyo baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Congo Brazzaville.

Bao la ushindi la Salah lilipatikana kwa mkwaju wa penalti dakika ya 95 na kuisaidia Misri kutinga michuano hiyo baada ya kupita miaka 28.

Baada ya mchezo huo, Rais wa Misri,  Abdel Fattah al-Sisi, ambaye alikuwa miongoni mwa wageni rasmi  aliwashukuru wananchi wake waliojitokeza kuisapoti timu yao ya taifa.

Congo walianza kupata matumaini baada ya beki wao, Arnold Bouka, kuipatia bao la kusawazisha kabla ya Salah kuongeza la pili dakika ya 95 kwa mkwaju wa penalti ambayo iliirudisha Misri katika michuano hiyo tangu mwaka 1990.

Misri walitambua kwamba ushindi pekee ndio utawasaidia kufuzu michuano hiyo wakitokea kundi E baada ya Uganda kupata suluhu dhidi ya Ghana siku moja kabla katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mandela, Uganda.

Miamba hiyo ya Afrika wamewahi kushinda mataji manne ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu 1990 – 1998, 2006, 2008 na 2010 lakini walionekana kucheza chini ya kiwango katika michezo ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia.

Mbali na Misri, Nigeria ndiyo timu ya kwanza kufuzu michuano hiyo kutoka Afrika baada ya kukaa kileleni mwa kundi B wakiwa wamebakiwa na mechi moja kwenye kundi ambalo liliitwa “Kundi la Kifo”.

Nigeria waliwahi kuingia katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo mwaka 1994, 1998 na 2014, lakini walitoka kwenye michuano hiyo hatua ya makundi 2002 na 2010.

Mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Cameroon na Algeria ambao waliwahi kuingia katika mzunguko wa pili kwenye michuano hiyo iliyofanyika Brazil mwaka 2014, tayari wameshatolewa baada ya kuwa na matokeo mabaya kwenye kampeni.

Mbali na Nigeria, taifa jingine lililojikatia tiketi hiyo mapema ni Ubelgiji na Costa Rica ambao ni mara yao ya tano kushiriki Kombe la Dunia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles