27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI WAPYA WATEULE WANENA

 Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, baadhi ya mawaziri wameelezea namna walipokea uteuzi huo.

Katika uteuzi huo alioufanya Rais Magufuli juzi Ikulu, Dar es Salaam, pia alifanya mabadiliko kwa kuwahamisha baadhi, kuwaondoa na kuwateua mawaziri, manaibu mawaziri wengine wapya huku akiongeza idadi ya wizara kutoka 19 hadi 21.

Mbali na hilo, ongezeko hilo la wizara lilitokana pia na kugawanya ile ya Nishati na Madini na ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mkuu huyo wa nchi pia ameongeza idadi ya manaibu mawaziri watano kutoka 16 hadi 21, kati ya hao 14 ni wapya.

Kutokana na hilo, sasa baraza jipya la mawaziri linaundwa na jumla ya mawaziri na manaibu mawaziri 42, tofauti na mwanzo ambapo walikuwa 35.

Gazeti hili jana lilizungumza na baadhi ya mawaziri walioteuliwa juzi, huku wakieleza furaha yao kwa kuaminiwa na mkuu wa nchi.

AWESO

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso, aliliambia MTANZANIA kuwa, anamshukuru Mungu kwa kuteuliwa na mkuu wa nchi kushika wadhifa huo akiwa kama kijana.

“Nimejisikia faraja sana…hii ni historia kwa Pangani kwa sababu tangu uhuru hatukuwahi kupata uteuzi wa aina hii.

“Pamoja na kwamba tunafurahi lakini tuna changamoto kubwa kwenye sekta ya maji, lakini tukishirikiana na timu ya wataalamu tutafanikiwa,” alisema Aweso.

Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani mkoani Tanga, aliwaomba wabunge wampe ushirikiano ili waweze kuwatumikia Watanzania.

NYONGO

Naye Naibu Waziri wa Madini ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo, aliahidi kuwatumikia Watanzania kwa uaminifu, uzalendo na uadilifu uliotukuka.

“Nimepokea uteuzi wa rais kwa furaha kubwa, pia pongezi ziende kwa wapigakura wangu kwa kunichagua na baadaye mkuu wa nchi kaniona…nitafanya kazi kwa uaminifu, uzalendo na uadilifu uliotukuka kwa masilahi ya Taifa langu,” alisema Nyongo.

MHANDISI NDITIYE

Kwa upande wake, Mbunge wa Muhambwe, Mhandisi Atashasta Nditiye ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, alisema atawatumikia Watanzania utumishi uliotukuka.

“Namshukuru sana rais kwa kuniamini kuteua kwa kulitumikia Taifa kupitia unaibu waziri, nahisi nina wito wa kuwatumikia zaidi wananchi. Ninawaahidi Watanzania kuwa nitawatumikia utumishi uliotukuka na mabadiliko ya kweli yanaonekana,” alisema Nditiye.

  1. KIGWANGALLA

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla ambaye sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, aliandika katika mtandao wa Instagram akisema alikuwa ziarani Kituo cha Afya cha Kilimarondo wilayani Nachingwea, Lindi.

Dk. Kigwangalla ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, alisema juzi saa nane mchana alipata ujumbe wa kuteuliwa kushika wadhifa mpya.

“Baada ya kumaliza kazi kituoni hapo na kuanza ku-rake njia ya kuelekea Liwale, Kituo cha Afya Kibutuka, ndipo mwenyeji wetu anaarifiwa na watu wa Liwale kuwa itakuwaje? Mheshimiwa ataendelea na ziara huku amebadilishiwa majukumu?

“Kilimarondo hakuna mtandao zaidi ya TTCL. Ni kilomita takribani 100 za vumbi kuelekea ndani huko.

“Ni tarafa ya pembezoni kwelikweli. Ni mahali ambapo Nachingwea inapakana na Tunduru,” alisema.

Alisema baada ya kupata taarifa hiyo, kila kitu ilibidi kisimame papo hapo.

“Namba za NWAMJW (Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto) ilibidi ziondolewe na safari ya kutoka huko ianze! Nimepokea salamu nyingi za pongezi na shukrani kwa Mungu aliye juu.

“Sitaweza kumjibu kila mtu, uungwana ni kutambua pongezi zenu na dua tele mlizotuombea, nawashukuru sana ndugu zangu. Tuzidi kuombeana dua tu,” alisema.

Alisema wana kazi ngumu ya kukimbia kukidhi matarajio ya kiongozi mkuu aliyewaamini na matarajio ya wananchi.

“Binafsi nawaahidi nyote kuwa sitawaangusha! Ahsanteni sana ndugu zangu, natarajia ushirikiano wenu wa kila hali,” alisema Dk. Kigwangalla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles