Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuachia huru mfanyabiashara Yusuf Manji baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanamkabili ya matumizi ya dawa za kulevya.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha amesema mahakama hiyo imepitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na pande zote mbili wa utetezi na jamhuri na mashtaka hayo hayathibitika.
Amesema katika kesi hiyo, ushahidi uliotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo wa Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohammed Janabi, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili na dawa za kulevya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Francis Benedict na Daktari Mkuu wa Gereza Keko Eliud Mwakawanga walisaidia kutambua hali halisi.
Amesema kesi hiyo iko kitaalamu zaidi kuliko kisheria kutokana na ushahidi uliotolewa wa pande zote mbili.
Manji alikuwa akikabiliwa na kesi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin, ambapo  alifikishwa mahakamani hapo Februari 16, mwaka huu.