27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAMKE ANAPOJIFUNGUA KICHANGA MAJINI

NI hali ya kawaida linapokuja suala la kuzaa, kitu kinachofikiriwa ni kwenda kujifungua mtoto katika vituo vya afya au hospitali.

Hospitali hizi huwa majengo yaliyo ardhini, ingawa pia kuna wengine wengi hujifungulia majumbani.

Lakini pia katika zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia, kama ‘hobby’ vile au bahati mbaya wengine hujifungulia kwenye gari, njiani au angani ambayo hutokea bahati mbaya kwa vile inategemea kibali cha daktari.

Lakini tukio la kuzaa ndani ya maji kwa wengi ni suala geni na linaloonekana la nadra, lakini linalowezekana katika zama hizi.

Video ya mwanamke akijifungua mtoto akiwa kwenye maji imevuma mitandaoni tangu mwanzoni mwa mwezi uliopita baada ya kuonekana akijifungua kwa urahisi kuliko inavyofikiriwa.

Wanawake wengi hutatizika sana wanapojifungua mtoto au watoto lakini kwa mwanamke huyu, Audra Lynn, inaonekana kuwa shughuli rahisi kwake.

Kujifungua hudhaniwa kuwa kitendo kinachochukua muda mrefu kikiambatana na maumivu makali ndiyo maana kuna misemo kuhusu uchungu wa uzazi, lakini kwa mama huyu haikuwa hivyo.

Amewathibitishia walioishuhudia video hiyo kwamba mtazamo huo si wa kweli, kutokana na kitendo chake hicho cha kuzaa majini kutokea kwa haraka sana na bila maumivu makubwa.

Video yake akijifungua huko Orange katika Jimbo la California nchini Marekani, imeshangaza wengi kwa sababu mtoto anaonekana kutoka baada ya misuli yake kujikaza mara chache tu.

Ikiwa imepakizwa katika mitandao ya Instagram na Facebook mwanzoni mwa mwezi uliopita, video hiyo ilitazamwa zaidi ya mara milioni 16 ndani ya siku chache tu.

Mumewe Robbie Williams alieleza kuwa kumwangalia mkewe Audra akizaa ilikuwa kana kwamba anaangalia ‘pub’ yake aipendayo ikiteketea moto.

Hilo lilitokea katika bwawa la kujifungulia huku mumewe akiwa kando yake

Mkunga Lisa Marie Sanchez Oxenham ambaye alipiga video hiyo na kuiweka mtandaoni anasema lilikuwa ‘tukio la kushangaza’.

Kile ambacho huwezi kukiona katika video hiyo ni kwamba kichwa kilikuwa tayari kimetoka.

“Kwa hiyo, nilimwambia Audra asubiri misuli ijikaze tena na hapo ndipo mtoto akachomoka,” anasema.

“Furaha ya mama inagusa sana. Anaposema mtoto wangu mvulana, inawafanya watu kulia. Ni tukio linalogusa moyo sana.”

Baada ya kuzaliwa, alimtoa  taratibu kutoka majini na kumkumbatia kifuani mwake.

Wote yeye na mwenzi wake walimwaga machozi huku mwanamume akionekana kutoamini kwa uwapo wa mtoto wake mikononi mwa mwenzi wake huyo.

Faida ya kuzaa ndani ya maji ni kuwa inaharakisha uzazi na kama ilivyoonekana katika video hiyo iliyoteka mitandao ya jamii.

Kwa mujibu wa Barbara Harper, mwasisi wa Asasi ya Kimataifa ya Uzazi Majini, kitu kimoja kinachotokea katika uzazi wa majini kuwa ukiwa kama mkunga sehemu kubwa ya mikono yako ‘inakuwa mifukoni’ na kuacha uzazi utokee bila ushiriki wako.

Kwa maneno mengine, anamaanisha kuwa uzazi wa njia hiyo haumpi kazi kubwa mkunga kama ule wa njia ya kawaida.

“Inaweza kutisha ukisikia hivi lakini ndiyo ukweli,” anasema.

Video hiyo ndani ya siku chache ikiwa imesambazwa zaidi ya mara 100,000 kwenye Facebook na watu 23,000 wamechangia maoni.

Watu hao walikuwa wepesi kutoa maoni kwa namna wanavyohisi au kusapoti.

Rachel Miles alitoa maoni akioneshwa kuvutiwa na tukio la kumtoa mtoto taratibu kutoka majini na kumkumbatia kifuani mwake.

Carol Stemple alitania akisema; “angalia hii si mbaya sana huku Megan Williamson akisema kwa ufupi; “aliufanya uzazi uonekane rahisi mno.

Wachangiaji wengine, Christy alikubaliana na wengine na kusema kuwa ilikuwa video na tukio zuri sana na alimshukuru mkunga kwa kushea video hiyo.

Lisa Marie anasema hajashangaa sana kwamba video hiyo aliyoirusha mitandaoni imevuma sana.

“Ninaamini video hii imevuma sana kwa sababu ni tukio zuri, la upendo, la faraghani na lenye mazingira yaliyotulia.

“Ni jambo ambalo huwa hatulihusishi na kujifungua tena na watu hawawezi kutosheka.

John Bradshaw aliona video na kuuliza; “Kwanini wanalia? Na kwanini wanakiacha kichwa cha kichanga ndani ya maji kwa muda mrefu, mbona hakuna rangi ya damu majini. Nini maana ya kitendo hiki?

Mchangiaji Gabriel Quinones alikubaliana na hilo na kuuliza; “Iwapi damu na kwanini mikono yote ya mwanamume iko nyuma ya mwanamke kana kwamba anashika kitu Fulani,”?

Ash McLendon alijibu swali hilo akisema; “hakuna damu kwa sababu hakuchanika kama ilivyo kwa wanawake wengine. Mikono ya mume iko nyuma kuwa tayari kwa lolote kusaidia kumshika mtoto ikibidi.

Kwa ujumla kauli na maoni ya shemu kubwa ya wachangiaji mitandaoni kuhusu video hiyo zilikuwa hasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles