27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MTAALA WA MAFUNDI SIMU UTAKAVYOKUWA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


UFUNDI simu ni mojawapo ya taaluma inayokua kwa kasi kutokana na kifaa hicho kuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano.

Kulingana na takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), hadi sasa kuna laini za simu za mkononi zipatazo milioni 40.

Ripoti ya Uchumi wa Simu za Mkononi iliyozinduliwa nchini mwaka jana, inaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa manane barani Afrika ambayo yana soko kubwa la simu za mkononi.

Simu za mkononi zimekuwa kama sehemu ya maisha ya kila mwanadamu, ni chombo kizuri na cha uhakika kwa mawasiliano ya haraka, kujifunza mambo mapya, kukuza uchumi na mambo mengine.

Matumizi ya simu za mkononi yanatoa mchango mkubwa katika kutatua matatizo ya mawasiliano barani Afrika na pia kuna utaratibu wa kutuma fedha hata katika maeneo ya mbali nchini kwa kutumia simu ya mkononi.

Hivyo ni dhahiri kuwa matumizi ya teknolojia hiyo ambayo yanazidi kuongezeka kila siku kwani teknolojia hiyo sasa inatumika katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo na imesaidia kurahisisha maisha ya watu wengi.

Ingawa simu ya mkononi ni kifaa chenye faida katika mawasiliano lakini tatizo huja pale kunapotokea uharibifu.

Changamoto hiyo imesabababisha kuibuka kwa watu wasiokuwa na ujuzi rasmi ya kukitengeneza kifaa hicho na kusababisha malalamiko kutoka kwa watumiaji.

Vijana mafundi simu wako wengi waliojitafutia ajira kwa njia ya kutengeneza simu za mikononi na kutengeneza ajira na kadiri wimbi la kukosa kazi linavyozidi kukua ndivyo ambavyo vijana wengi wanazidi kujikita kwenye ufundi huo.

Vijana ambao hawana ujuzi wamekuwa wakifanya uharibifu mkubwa na kusababisha kuwe na kesi nyingi za simu zilizoharibiwa kwa kuchomachoma na kifaa kama hothair gun, kifaa cha kuunguza nywele ‘dry hair’ na kusababisha heshima ya ufundi kupotea.

Kwa kutambua changamoto hiyo, TCRA iliziomba Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kufanya utafiti na kubaini kuwa kuna uhitaji mkubwa wa ujuzi katika sekta hiyo.

Matokeo ya utafiti huo yaliwasilishwa wiki iliyopita na kikosi kazi kilichofanya utafiti huo wakati wa mkutano wa pamoja uliohusisha mafundi simu ambao pamoja na mambo mengine ulijadili changamoto wanazokumbana nazo.

Utafiti huo ulihusisha mafundi 261 kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro ulibaini mafundi wengi wa simu nchini hawana mafunzo rasmi ya taaluma hiyo.

MATOKEO YA UTAFITI

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mkuu wa Chuo cha Veta Kipawa, Mhandisi Lutenganya Lucius, anasema wamebaini kuwa mafundi wengi walifundishwa na jamaa zao na wengine wanatumia utundu wao.

Anasema asilimia 54 ya mafundi walipata mafunzo lakini asilimia 80 ya mafunzo hayo hayakuwa rasmi na asilimia 20 hawakupata kabisa mafunzo.

“Tumebaini mafundi wengi walipata mafunzo kwa kufundishwa na jamaa zao na wengine hawakufundishwa na mtu bali wanatumia utundu wao wenyewe,” anasema Mhandisi Lutenganya.

Kiongozi wa Kikosi Kazi kilichofanya utafiti huo, Dk. Petro Pesha kutoka DIT, anasema utafiti ulikuwa na lengo la kubaini mapungufu na kutengeneza mtaala kwa ajili ya kuyaondoa.

“Tulichagua mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro kwa sababu ina mafundi wengi, tuliangalia mazingira yao ya kazi na kuangalia kama wanafuata taratibu zilizowekwa,” anasema Dk. Pesha.

JINSI MTAALA UTAKAVYOKUWA

Mjumbe wa kikosi hicho, Dk. Paul Fahamuel kutoka DIT, anasema mtaala tayari umekamilika na wanatarajia kuwa kabla ya mwisho wa mwaka huu kozi zitaanza kutolewa.

Anasema mafunzo yatakayotolewa yatahusisha mafundi waliko kazini na wale wanaotaka kujifunza ambapo watajengewa uwezo wa teknolojia ya ufundi

Anasema kozi hiyo itatolewa kwa muda wa miezi mitatu na gharama ya mafunzo ni Sh 350,000.

“Mtaala unalenga kuwapa mafundi ujuzi wa masuala muhimu katika sekta ya mawasiliano. Tunataka tuwe na mafundi watakaotoa huduma nzuri zaidi na kuboresha sekta hii,” anasema Dk. Fahamuel.

Kupitia programu hiyo hata mafundi waliopata mafunzo nje ya mfumo rasmi wataweza kupimwa viwango vya ujuzi wao kwa kutumia mtaala huo na kutambuliwa rasmi ujuzi wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Habibu Bukko, anasema mafunzo yatakayotolewa yanalenga kuwasaidia wale wote wanaohitaji kujiajiri katika ufundi wa simu na kujipatia kipato cha kuendesha maisha.

“Lakini pia masomo haya yatakuwa msaada kwa wale ambao ni mafundi simu kujifunza vitu wasivyovijua kuhusu kushughulikia matatizo mbalimbali ya simu za wateja wao,” anasema Bukko.

Anasema pia wana mpango wa kuwatambua mafundi waliojifunza nje ya mfumo wa kawaida ambapo watapimwa na wakikidhi yatakayokuwemo katika mtaala huo watapatiwa vyeti.

“Kuna mafundi wengine unakuta wanafunga kifaa ili mradi simu iwake na kufanya kazi lakini kumbe si kifaa husika. Simu itafanya kazi lakini baada ya siku mbili inaanza kukoroma,” anasema.

TCRA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Fortunata Mdachi, anasema teknolojia ya simu za mkononi inazidi kukua ndio maana tumeona umuhimu wa kuwa na kozi mbalimbali kwa ajili ya mafundi simu ili kuwe na watu wenye ujuzi katika sekta hii.

Anasema changamoto ya kukosekana kwa ujuzi imesababisha baadhi ya mafundi kuharibu simu za wateja, mfumo wa rajisi za utambulisho katika simu.

Anasema baada ya mafunzo hayo mafundi wa simu nchini watatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutengeneza simu kutoka mamlaka hiyo.

“Mafundi wa simu, wanatakiwa kuomba leseni ya kutengeneza simu na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa simu,” anasema Mdachi.

Mwisho.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles