22.3 C
Dar es Salaam
Monday, September 30, 2024

Contact us: [email protected]

WORLDSHARE INAVYOGUSWA NA CHANGAMOTO SEKTA YA ELIMU

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


ELIMU imekuwa ni kipaumbele katika mataifa mengi ikiwa ni rasilimali ya kipekee inayoweza kuinua familia na jamii kutoka kwenye umaskini na kuongeza ukuaji wa uchumi wa nchi.

Licha ya umuhimu huo bado mamilioni ya watoto nchini hawapati elimu inayotakiwa kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali kama za upungufu wa madarasa, madawati, walimu, matundu ya vyoo, vitendea kazi, maabara na maktaba.

Changamoto hizo na zingine zimesababisha baadhi ya shule kushindwa kutimiza malengo yao kitaaluma.

Kwa kutambua changamoto zinazokabili sekta ya elimu nchini, Shirika lisilo la kiserikali la Worldshare ambalo linajihusisha na kusaidia watoto walioko kwenye mazingira magumu, liliamua kuanza kuzisaidia shule zenye mahitaji.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Nara Kim, anasema lengo la shirika hilo ni kumfikia kila mtoto mwenye unyonge na kumpatia tumaini na furaha.

“Tunatambua na kuthamini maendeleo ya elimu Tanzania ndio maana tumekuwa tukitembelea shule zenye mahitaji na kuzisaidia ili wanafunzi waweze kusoma vizuri.

“Makundi ya walio pembezoni na walio kwenye mazingira magumu, yasiyofikika kirahisi na ambayo bado hayajanufaika na haki yao ya elimu lazima yapewe kipaumbele.

“Kazi kubwa ya Worldshare ni kufadhili watoto wenye ualbino, yatima, walemavu na walioko kwenye mazingira magumu. Tunataka kumfikia kila mtoto mwenye unyonge na kumpatia tumaini na furaha,” anasema Kim.

Anasema wamekuwa wakichimba visima katika shule za serikali za msingi na sekondari na kwamba tangu mwaka 2010 hadi sasa wamechimba zaidi ya visima 78 katika maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa shule zilizonufaika na misaada inayotolewa na shirika hilo ni Shule ya Msingi Kichangani iliyoko Manispaa ya Kigamboni na Shule ya Msingi Karume iliyoko Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Shule ya Msingi Karume ilichimbiwa kisima cha maji wakati Shule ya Msingi Kichangani ilipelekewa msaada wa mabegi ya kuhifadhia madaftari kwa wanafunzi.

Nara anasema ujenzi wa kisima hicho umegharimu Sh milioni 10 ambazo zimehusisha pia ununuzi wa pampu ya umeme, tanki la kuhifadhia maji na mabomba.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hillgard Wambusha, anasema kutokana na kuchimbiwa kisima hicho wanafunzi wake sasa wataondokana na adha ya ukosefu wa maji ambayo ilikuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

“Shule yetu bado ni changa hivyo, msaada huu wa kisima utatusaidia kuweka mazingira bora ya utoaji elimu, tunaomba msituchoke muendelee kututazama kwa jicho jingine kwa kututatulia changamoto zingine,” anasema Mwalimu Wambusha.

Anasema bado wanakabiliwa na changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa, kukosekana kwa uzio, vyoo vya walimu na upungufu wa matundu ya vyoo vya wanafunzi,” anasema.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2013 ina wanafunzi 871 ambao ni wa darasa la awali hadi la tano.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kichangani, Mwinda Ulungu, anasema inakabiliwa na changamoto za miundombinu kama vile uhaba wa vyumba vya madarasa, vyoo, nyumba za walimu na umeme.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, shule hiyo ina wanafunzi 203 na walimu tisa huku vyumba vya madarasa vikiwa vitano na nyumba tatu za walimu.

“Tuna changamoto nyingi kama walimu hawana kabisa vyoo, tunaomba wadau wazidi kutusaidia ili kuinua kiwango cha taaluma,” anasema Mwalimu Ulungu.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Taaluma wa Manispaa ya Kigamboni, Naomi Makolobela, anasema Shule ya Msingi Kichangani iko pembezoni na ni mojawapo ya shule zilizoko kwenye mazingira magumu katika manispaa hiyo.

“Wadau wengi wamekuwa wakielekeza nguvu katika shule za mjini, tunaomba waziangalie na shule zilizoko pembezoni ili watoto waweze kusoma vizuri,” anasema Makolobela.

Ofisa huyo anasema licha ya changamoto zilizopo wanafanya jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba zinatatuliwa ili kuongeza ubora wa elimu inayotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles