27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

ROBOTI WATUMIKA KUFANYA SHUGHULI ZA KILIMO

Na JUSTIN DAMIAN


WAKATI nchi nyingi za Kiafrika ikiwamo Tanzania zikitumia nguvu ya binadamu na wanyama kwenye shughuli za kilimo ikiwamo kuvuna, wenzetu wa nchi zilizoendelea wanatumia roboti kufanya kazi hizo.

Uingereza moja ya nchi zilizopo barani Ulaya, imeanza kutumia roboti karibu katika kila hatua ya shughuli za kilimo ikiwamo hatua ya mwisho ambayo ni uvunaji. Kazi hizi sasa zinaweza kufanyika pasipo msaada wowote wa binadamu.

Hands Free Hectare, ni shamba la majaribio ambalo watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Harper Adams kilichopo katika kijiji cha Edgmond nchini wameweza kutengeneza roboti ambaye ana uwezo wa kuvuna tani 5 za shayiri bila msaada wa binadamu. Roboti huyo pia ana uwezo wa kuotesha, kuweka mbolea, kuvuna na kuhifadhi mavuno.

Timu ya watafiti chini ya mradi huo, wanasema hatua hiyo ni mafanikio makubwa na itakuwa ni chachu ya kuchangia kuongeza uzalishaji wa mazao haswa katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya mazao mbalimbali yanaongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu.

Watafiti hao wametumia mashine za kilimo ambazo zimekuwa zikitumika kwenye shughuli za kawaida za kilimo pamoja na programu maalumu ya kompyuta ambayo ndiyo humuongoza roboti huyo mkulima.

“Kwenye kilimo hakuna mtu aliyeweza kugundua teknolojia ambayo inatoa suluhisho kwa shughuli zote kuanzia kupanda hadi kuvuna,” anasema Jonathan Gill ambaye ni mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Harper Adams.

Watafiti hao walinunua mashine ndogo ndogo za kilimo ikiwa ni pamoja na trekta na mashine ya kuvuna nafaka. Walitumia mashine hizo kutengeneza roboti huyo anayeweza kufanya kazi pasipo usimamizi au uangalizi wa binadamu.

Hatua ya kwanza ya utengenezaji ilihusisha kutengeneza mfumo wa mawasiliano kama wa radio. Hatua ya pili ilikuwa ni kutengeneza programu ya kompyuta ambayo inaweza kuendesha matendo yote ya roboti huyo pasipo kuwa na makosa,” anaongeza mtafiti huyo

Mtafiti mwenza, Martin Abell, anayefanya kazi kwenye kampuni ya kilimo kwa ajili ya malighafi za viwanda na ambaye ameshirikiana na chuo hicho kikuu anasema, roboti hao wamewekewa ukomo wa muda wa kufanya matendo mbalimbali.

“Roboti huyu hufanya kazi kulingana na melekezo ambayo tayari yameshawekwa na kwa kuzingatia muda maalumu. Kila tendo limewekewa muda wake kulingana na namna ambavyo linatakiwa kutekelezwa,” anasema

Anasema mara ya kwanza waliweka mfumo ambao roboti huyo alifanya kazi kwa kufuata mstari ulionyooka jambo ambalo lilisababisha uharibifu mkubwa wa mazao. Hata hivyo anasema, tatizo hilo limeweza kufanyiwa marekebisho na kwamba ufanisi kwa sasa ni mkubwa na wa kuridhisha

“Ukilinganisha kiasi kilichokuwa kinavunwa kwa kutumia mashine za kawaida kwa kutumia roboti utagundua kuwa roboti ameleta ufanisi mkubwa zaidi kwa kuwa kiasi kinachopotea ni kidogo sana,” anaongeza

Anasema pamoja na roboti huyo, watafiti pia wametengeneza kifaa kama ndege ambacho huiongoza roboti hiyo kukata majani ambayo hayatakiwi kuwepo shambani kisha kuyapeleka moja kwa moja kwa watafiti.

Watafiti wanasema, teknalojia ya roboti katika kilimo itawawezesha wakulima kuweza kuwekea mimea yao mbolea na kunyunyuzia dawa za kuua wadudu na magugu kwa usahihi zaidi na pia kuboresha ubora wa udongo. Ili kuweza kufanya kazi anayoamrishwa kwa muda mdogo roboti hao wamewekewa uwezo wa kuongeza uwezo wa kufanya kazi kulingana na mazingira pamoja na mahitaji.

Baadhi ya mambo ambayo roboti huyo anafanya ni pamoja na kuweza kutambua mimea ambayo ni dhaifu na hivyo kuiwekea mbolea huku ile inayokuwa vizuri ikiachwa bila kuwekewa mbolea na hivyo kuepusha matumizi yasiyo ya lazima ya mbolea

“Kwa sasa mashine zinazotumika kwenye kilimo ni kubwa, zinafanya kazi kwa haraka na pia zinachukua nafasi kubwa ardhini lakini ufanisi wake si mzuri sana ukilinganisha na roboti huyu ambaye hutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi,” anasema.

Timu ya Chuo Kikuu cha Harper Adams iliyoshiriki kumtengeneza roboti huyo imesema inapanga kutumia shayiri iliyovunwa na raboti huyo kutengeneza bia chache ambazo zitagawiwa kwa washiriki wa mradi wa kumtengeneza roboti huyo.

Timu hiyo imesema inaendelea kufanya utafiti zaidi wa kuwezesha roboti kutumika katika hatua nyingi zaidi katika shughuli za kilimo kwa siku zijazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles