Na Amina Omari, TANGA
KUKOSEKANA kwa masoko na majukwaa ya kutoa elimu ya ubunifu kwa ajili ya wafugaji hasa wa ng’ombe wa maziwa, kimekuwa kikwazo kwa wafugaji kupata faida ya mazao yatokanayo na mifugo.
Hayo yamesemwa na Mkufunzi Mwandamizi kutoka Chuo cha Nelson Mandela, Dk.Kelvin Mtei, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka Halmashauri ya Lushoto, Bumbuli na Korogwe Vijijini.
Alisema kupitia mradi wa maboresho ya ufugaji, wamebaini changamoto zinazowakabili wafugaji ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.
“Kupitia mafunzo hayo wafugaji wataweza kubadilika kutoka katika ufugaji wa kimazoea na kufuga kisasa kwa kupata mazao bora pamoja na kujengewa uwezo wa kutafuta masoko,” alisema Dk. Mtei.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Kazimbaya Makwega, alisema kupitia mafunzo hayo wafugaji wameongeza thamani ya mazao yao na kubadilisha dhana nzima ya ufugaji.
“Wafugaji wangu wataweza kujiongezea kipato kwani sasa watajua namna bora ya utunzaji wa ng’ombe hao wa maziwa kwamba si tu kwa ajili ya kufuga ili kujipatia kipato ngazi ya familia bali kufuga kibiashara,” alisema Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, magonjwa kama kupe yamekuwa yakisababisha vifo kwa mifugo.
Mkuu wa Kampasi ya Chuo cha Mifugo cha Buhuri, Vinance Tarimo, alisema Serikali kupitia wizara husika imeanza kuchukua hatua.
Alisema tayari timu ya wataalamu imetumwa nchini Kenya kwa ajili ya kujifunza aina moja ya chanjo ya kuzuia ugonjwa huo.