Na, HUSSEIN JUMA, SHINYANGA
NIENDELEE kumshukuru Mungu kwa uhai ambao sisi ametujaalia kuiona siku hii ya leo. Vilevile nichukue nafasi kubwa na adhImu kabisa kulishukuru gazeti la Mtanzania kwa kuchapisha Makala yangu hii ili kufikisha ujumbe ambao si wangu tu, bali ni wa wanafunzi wote Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM); malalamiko ambayo yamekuja kufuatia ongezeko la gharama za chuo za malazi (DIRECT COSTS).
Pamoja na kuwa leo nataka niweke baadhi ya mambo sawa, lakini pia ningependa kuongezea kitu ambacho nilikisahau kwenye Makala yangu ya wiki iliyopita ambacho pia ningependa kukizungumzia hapa, suala la malipo ya Uthibiti wa Ubora wa Elimu ambayo awali yalielezwa kuwa ni malipo ya Tume ya Chuo Kikuu Nchini. Kwa hiyo, leo nitazungumzia masuala mawili kama nilivyoyaainisha hapo juu.
Jana Oktoba 3, 2017, saa 06:18 mchana nimepigiwa simu kwa nambari 0715 035 001 ambayo nimeongea nayo na kujitambulisha kuwa yeye ni Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo tajwa (mazungumzo yamechukua dk.1 sekunde. 26). Alichokizungumza ni kujaribu kuniweka sawa juu ya kile nilichokiandika kwenye Makala ya wiki iliyopita na kuchapishwa kwenye gazeti la Mtanzania toleo Na. 8681 la Septemba 27, 2017; Makala iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Serikali itusaidie haya UDOM’
Mshauri wangu ameniambia kuwa nimeandika vizuri, lakini nimedanganya juu ya ongezeko la gharama za malazi ambalo limeongezeka kutoka Sh. 500 kwa siku hadi 950 kwa siku na hivyo kufanya jumla ya gharama hizo kuwa ni Sh. 263, 500 kwa mwaka. Kutokana na hilo, Mshauri wangu ameniomba kurekebisha taarifa hii, ambayo kwa maelezo yake ni kwamba, ongezeko hilo si la kweli, bali ukweli ni kwamba, ongezeko ni la 250; kutoka Sh. 500 hadi Sh. 750 linalofanya jumla ya ongezeko kuwa ni Sh. 228, 500.
Bahati mbaya sana nilipojaribu kumtafuta kwa simu kwa nambari hiyo hiyo ya simu kwa lengo la kumpa ufafanuzi halisi, matokeo yake simu hiyo inatumika muda wote. Pamoja na mengine, kwa namna simu ilivyokatwa inanipa wasiwasi kuwa hajapendezwa na nilichokiandika. Nimejaribu pia kumwandikia ujumbe wa maandishi (message), napo pia hajajibu.
Ukweli ni kwamba, tangazo la Septemba 19, 2017 (picha zake naambatanisha) linaonesha ongezeko la Sh. 450 na si Sh. 250 anavyodai mshauri wangu. Ongezeko hilo ni kutoka Sh. 500 kwa siku hadi Sh. 950 kwa siku na ndilo lililowashtua wanafunzi na kuanza kulijadili ambapo Septemba 20, 2017 hoja zilianza kujadiliwa kwenye mitandao ya kijamii na uongozi wa wanafunzi kuahidi wangefuatilia na kuleta majibu sahihi.
Siku hiyo hiyo, kama nilivyoeleza kwenye Makala yangu inayodaiwa kuwa na taarifa zisizosahihi, Rais wa Kitivo cha Elimu kupitia Makamu wake Monica Elias alikuja na majibu kuwa, wamejitahidi kuushawishi uongozi wa chuo juu ya ongezeko hilo na hatimaye uongozi huo umeamua kupunguza gharama hizo. Badala ya ongezeko kuwa Sh. 950, uongozi wa chuo umepunguza hadi kufikia Sh. 750 kwa siku na hivyo kufanya jumla ya gharama kuwa Sh. 228, 500 kwa mwaka. Kutokana na maelezo haya, ndipo tangazo la pili lilipotoka siku hiyo hiyo ya Septemba 20, 2017 na kuwekwa kwenye tovuti ya chuo Wanafunzi walipojaribu kuhoji juu ya kwa nini hasa gharama hizo zisibaki kama awali, hadi leo uongozi umebaki na sababu zile zile za awali na kuendelea kushikilia msimamo kuwa wangewajulisha endapo kutakuwa na mabadiliko. Na ufafanuzi huu nimeusema vizuri kabisa kwenye Makala hiyo.
Kwa jitihada zangu, nikajitahidi kumtafuta Waziri Mkuu Kitivo cha Elimu na baadaye Rais mwenyewe ambapo wote wameendelea kushikilia msimamo huo wa awali. Sababu zenyewe nadhani nilizisema pia kwenye makala iliyopita, ila kwa haraka haraka ni sababu tatu, (i) Serikali kupunguza ruzuku ya chuo, (ii) gharama za maisha kupanda na (iii) kuchangia gharama za ukarabati wa chuo.
Sasa, kutokana na kile anachodai Mshauri wangu kuwa si taarifa sahihi, leo nimeamua kuambatanisha picha za matangazo yote mawili (la Septemba 19, 2017 na la Septemba 20, 2017) kama yanavyoonekana ili anisaidie sehemu ambapo nimekosea na nakubali kurekebisha endapo kutakuwa na makosa, kwani na mimi ni binadamu.
Lakini pia niendelee kusema tu kwamba, gharama hizo ni nyingi sana hasa kwa mwanafunzi wa kawaida kabisa ambaye hana hata mkopo. Nimpe mfano pia kuwa, Semester iliyopita pekee, kuna baadhi ya wanafunzi walishindwa kabisa kulipa gharama hizo za Sh. 169, 000 na kuchukua muda mrefu pasi na kusajiliwa, Je leo gharama ya Sh. 223, 500 wataweza kuilipa bila matatizo? Ndio kinachotufanya tuiombe Serikali itusaidie, kwani maisha ni magumu kwa wote.
Suala la pili ambalo sikulisema kwenye Makala ya wiki iliyopita ni uhalali wa malipo ya fedha ya Sh. 20,000 kwa ajili ya ‘Quality Assurance’ ambayo pia hadi sasa majibu yake yamekuwa yakiongeza maswali mengi miongoni mwa wanafunzi. Fedha hiyo mwaka wa masomo 2015/2016 haikuwa imeelekezwa kulipwa. Maelekezo yalikuja baadaye wakati wanafunzi wakiwa kwenye foleni ya kufanyiwa udahili (Registration) na hivyo kutakiwa kila mwanafunzi alipe mara moja kabla ya udahili. Wanafunzi waliitikia vizuri.
Baadaye zikaibuka hoja, kwa nini fedha hiyo inalipwa? Jibu lililotolewa ni kwamba, fedha hiyo ni kwa ajili ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU). Cha ajabu, fedha hiyo imeendelea kulipwa na toka ianze kulipwa, hakuna risiti (receipt) ililyowahi kutolewa kwa mwanafunzi yoyote. Swali tena likarudi pale pale, Je fedha hii ni halali? Kama siyo halali, kwa nini haina risiti kama malipo mengine?
Kwa tafsiri ya kawaida, ‘Quality Assurance’ ni ‘Udhitbiti wa Elimu’ ambao kwa kawaida hufanywa na karibu kila nchi zilizoendelea kwenye sekta ya elimu. Mfano mzuri ni Malaysia, Ufini (Finland) na kwa sasa Uchina chini ya mfumo wao wa elimu unaojulikana kama Tai Pei ambapo maana yake ni kwamba, chuo husika huhakikisha elimu inayotolewa chuoni ni ya ubora wa hali ya juu na inakidhi vigezo. Wao wanafanyaje? Nimeeleza kwenye Makala nyingi sana kuwa, wao hufanya tafiti, tafiti ambazo kwa kawaida hugharimu. Kwa mujibu wa mfumo wa Ufini kwa mfano, tafiti hizi hugharamiwa na Serikali yenyewe.
Sasa hebu tuje kwenye hali ya kawaida kabisa, kwamba tufanye fedha ile ni kwa ajili ya ‘Quality Assurance’ kama inavyoaminika, lakini kwa Chuo Kikuu cha Dodoma, kitu ambacho pekee hufanyika ni ‘Evaluation’, tena kwa njia ya mtandao kwa gharama za wanafunzi hao hao. Ni kwa mara ya kwanza mwaka huu tumeshuhudia Dk. Mutahabwa akizunguka katika kila shule kufanya utafiti wakati wa mazoezi kwa vitendo.
Na kama fedha hiyo ni kwa ajili ya TCU, utaratibu umebadilishwa. Mwanafunzi kwa sasa anaomba moja kwa moja chuoni kwa gharama zake mwenyewe. Lakini bado malipo hayo yameelekezwa kulipwa kama kawaida na risiti hazijawahi kutolewa popote.
Sasa wanafunzi bado wanaendelea kuhoji uhalali hasa wa malipo haya uko wapi? Je, kuna malipo halali yasiyo na risiti? Kama fedha ndogo tu ya UDOSO fee, kiasi cha Sh. 5, 000, inatolewa risiti, iweje fedha hiyo ikose risiti? Bado naendelea kusema kuwa ipo haja ya kupata msaada juu ya hili.
Nimalizie kwa jambo lingine ambalo pia nililisema vizuri kwenye Makala iliyotangulia. Suala la ongezeko la malipo ya fedha kwa ajili ya Serikali ya Wanafunzi (UDOSO). Ongezeko hili wanafunzi walipolalamika, majibu yalikuja kuwa, lipo kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga mwaka wa kwanza. Kwa kawaida hawa hawana wa kuwasemea na wataona ni sawa tu.
Fedha hiyo ni kweli kabisa na wala hakuna anayebisha juu ya malipo yake. Tatizo ni kwamba, kwa nini iongezwe kwa mwaka wa kwanza pekee? Na mbaya zaidi, pamoja na malalamiko yote, hakuna sehemu yoyote ambayo viongozi wa Serikali hii ya wanafunzi walishawahi kusomea wanafunzi mapato na matumizi juu ya fedha hiyo. Sasa, inawezekanaje kuongezwa wakati hatujui hasa matumizi yake?
Suala la malipo kuwa tofauti linakwenda mpaka kwenye gharama hizo za malazi, ambapo mwanafunzi anayeanza masomo mwaka wa kwanza analipa tofauti na wanaoendelea. Kwa mfano, malipo ya Sh. 228, 500 baada ya ongezeko la Sh. 250 kwa mujibu wa tangazo la Septemba tarehe 20, 2017 na kama Mshauri wa wanafunzi alivyothibitisha ni tofauti kabisa na kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwenye fani ile ile. Mwanafunzi anayeendelea na masomo (mwaka wa pili na kuendelea) anatakiwa kulipa Sh. 228, 000 wakati yule wa mwaka wa kwanza anatakiwa kulipa sh. 268, 750 katika kada ile ile. Je, hapa kwa nini?
Wakati mwingine wanafunzi hurudi kufanya mitihani upya endapo watafeli ya awali, mitihani ambayo inaitwa ‘Sup. Exams’. Pamoja na kuwa wamelipa fedha za malazi, wanafunzi hutakiwa kulipa kiasi cha Sh. 7, 000 kila mmoja kwa ajili ya chumba hali ya kuwa mwaka haujaisha. Je, hili nalo limekaaje?
Mimi niendelee kutoa rai kuwa, kuna haja kubwa ya msaada wa aidha ufafanuzi ama marekebisho juu ya malalamiko haya ili mtoto wa maskini aendelee kupata elimu ya juu bila bughuza ya aina yoyote, kwani elimu hii ni muhimu sana kwenye maendeleo ya mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Natanguliza shukrani.
+255 759 947 397