32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MWIJAGE AZINDUA BODI TIC, KUKOSEKANA TOVUTI NONGWA

 

Na LEONARD MANG’OHA


MWISHONI mwa wiki iliyopita Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) sambamba na tovuti mpya ya kituo hicho.

Uzinduzi wa bodi ulikuwa ni utekelezaji wa utaratibu wa kawaida baada ya ile iliyokuwapo awali kumaliza muda wake hivyo Rais Dk. John Magufuli, akamteua Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Profesa Longinus Rutasitara, kushika nafasi ya Profesa Lucian Msambichaka, aliyemaliza muda wake.

Uzinduzi wa tovuti ulilenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa TIC na kurahisisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali kuhusiana na fursa za utalii nchini sambamba na kupungua usumbufu kwa watu wenye nia ya kuwekeza nchini kupata taarifa za awali kuhusu mazingira ya uwekezaji.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kupata taarifa kuhusu miundombinu, maeneo ya uwekezaji, aina ya miradi inayoweza kupata msamaha wa kodi na vigezo vyake, upatikanaji wa nishati ya umeme na maji.

Geoffrey Mwambe ni Mkurugenzi Mtendaji TIC, anasema tovuti hiyo itakuwa chachu katika utoaji wa taarifa mbalimbali zinazohusu fursa na huduma za uwekezaji na mazingira ya uwekezaji nchini.

“Suala la utoaji wa taarifa ni muhimu na ni matakwa ya kisheria, TIC ilikuwa na mapungufu makubwa katika tovuti yake ambayo uendeshaji wake haukuwa chini ya kituo ambayo ni kasoro kubwa sana.

“Hivyo basi kusababisha kuwa na mapungufu makubwa katika utoaji wa taarifa zinazohusu nchi hasa kwenye masuala ya uwekezaji,” anasema Mwambe.

Anaeleza kuwa tovuti ya awali licha ya kuwa ilikuwa ikitumiwa na TIC, lakini ilikuwa ikiendeshwa na shirika moja la nje ya nchi na wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano wa kituo hicho hawakuwa na uwezo wa kuidhibiti au kuirekebisha.

Anasema jambo hili ni hatari si kwa TIC peke yake bali hata kwa usalama wa taarifa za Serikali na kukosa umiliki wa wazi.

Anasema jambo hilo lilikuwa ni hatari kwa Serikali yenyewe haikuweza kutunza taarifa zake. Anasema kukosekana kwa tovuti imara na yenye taarifa za kina kuhusu uwekezaji kuliwafanya waulizwe maswali mengi katika ziara mbalimbali wanazokwenda kuvutia uwekezaji nje ya nchi.

“Nilipokuja hapa nikaamua tuwe na tovuti ambayo itamwezesha mtu kupata taarifa zote muhimu ili tunapokwenda kutafuta wawekezaji twende na taarifa ambazo mtu hawezi kuzipata kwa urahisi tu ambazo hazipaswi kuwekwa kwenye tovuti kwa masilahi ya Taifa,” anasema Mwambe.

Hili ni suala jema na lenye kupaswa kupongezwa na huenda litabaki kuwa miongoni mwa yale yatakayokuwa yakitumika kumkumbuka Mwambe hata baada ya kumaliza muda wake kama Mkurugenzi wa TIC.

Japo limekuja kwa kuchelewa sana ila ni nafuu kwa sababu limeshughulikiwa kwa sababu lilikuwa jambo la ajabu kwa taasisi ya Serikali muhimu kama TIC ambayo ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha Serikali inatimiza azma yake ya kuwa nchi ya viwanda kuelekea uchumi wa kati kutumia tovuti ambayo yenyewe si mmiliki halali, ni aibu kubwa.

Naamini kuwa Mkurugenzi huyu ambaye ameiongoza TIC kwa miezi minne sasa, anatambua umuhimu wa kuwa na mtandao thabiti wa taasisi yake ili kurahisisha utoaji wa taarifa.

Ndiyo maana katika mazungumzo yake anaeleza kuwa kukosekana kwa tovuti yenye taarifa thabiti za uwekezaji kuliwafanya wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Tanzania kulazimika kusafiri kuja nchini kutafuta taarifa ambazo wangeweza kuzipata kirahisi wakiwa nchini mwao.

Wachunguzi wa mambo wanasema bila kuwa na mawasiliano ya kuaminika ya mtandao tumerudisha nyuma kasi yetu ya maendeleo kwa kiasi kikubwa na hivyo kuacha washindani wetu na Afrika ya Kusini kutamba kwa kuwavutia  wawekezaji kwani wao taarifa zao hupatikana kwa urahisi tofauti na sisi.

Waziri Mwijage anaitaka TIC kuhakikisha inaunganisha tovuti hiyo iliyozinduliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa zote za bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya biashara na Serikali inapata makusanyo sahihi ya kodi.

Mwenyekiti anayemaliza muda wake Profesa Lucian Msambichaka, anaieleza Bodi mpya na TIC kwa ujumla inapaswa kutambua kuwa ina jukumu kubwa la kuhakikisha inakuwa sehemu ya kutolewa mfano na kila mtu anayefika kituoni hapo kupata huduma.

Anawashauri kuthamini muda na kutambua kuwa unafanana kote duniani hivyo wahakikishe wawekezaji hawatumii muda mwingi kukamilisha taratibu za kuwekeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles