27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SHANGWE ZA FIESTA KURINDIMA TABORA

Na MWANDISHI WETU

SHANGWE za tamasha la Tigo Fiesta zitakuwa zikirindima Tabora leo kwa wakazi wake kupata burudani ya aina yake kutoka kwa wasanii mbalimbali watakaopanda jukwaani.

Wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wamejipanga kutoa burudani ya uhakika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, ili kuwaridhisha mashabiki wao ambao wana kiu ya kuwaona wakiimba nyimbo kwa kuwashuhudia tofauti na kuwasikiliza redioni au kuwashuhudia kwenye runinga.

Wasanii ambao wako mkoani hapa tayari kwa ajili ya kuwapa mashabiki wao burudani katika tamasha hilo la Tigo Fiesta ni pamoja na Chege, Ney wa Mitego,

Nandy, Maua Sama, Darassa, Rostam, Mr Blue, Young Dee, Aslay, Jux, Msami na Ben Pol.

Wasanii Roma Mkatoliki na Stamina wamekuwa wakiwapagawisha mashabiki wa tamasha hilo kutokana na kuwateka kihisia kupitia wimbo wao wa pamoja uitwao ‘Hivi ama vile’.

Pia Chege atakuwa kivutio katika Tigo Fiesta na mashabiki wa muziki wa kizazi kipya watakuwa na shauku ya kutaka kumshuhudia akiimba nyimbo zake mbalimbali, ikiwamo ile mpya ya ‘Runtown’ sambamba na ule wa ‘Kelele za Chura’ aliyomshirikisha mwanadada Nandy, ambaye ni miongoni mwa wasanii watakaokuwapo katika tamasha hilo.

Kwa upande wa Ney wa Mitego, anatarajiwa kuwapagawisha wakazi wa Tabora akiwa na wimbo wake wa ‘Wapo’ na nyinginezo.

Nandy, ambaye ameonekana kuliteka jukwaa katika Tigo Fiesta tangu ilipozinduliwa jijini Arusha, naye anasubiriwa kwa hamu kutoa burudani akiwa na wimbo wake wa ‘Wasikudanganye’, Nagusagusa na nyinginezo.

Meneja wa Tigo Kanda ya Ziwa, Gwamaka Mwakilembe, alisema mwaka huu wameamua kudhamini Fiesta ili kusaidia vipaji vya wasanii na kuwaletea wateja wao burudani pamoja na kuwapatia vifurushi wanaponunua tiketi za Tigo Fiesta kwa Tigopesa.

Kauli mbiu ya Tigo Fiesta mwaka huu ni ‘Tumekusoma’ na kwamba baada ya wasanii hao kuuwasha moto Tabora, burudani hiyo itaendelea katika mikoa Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tigo Fiesta, Sebastian Maganga, alisema kuwa, Tigo Fiesta ni burudani ya kipekee ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na kwamba mashabiki wamefurahia burudani Arusha na wataendelea kufurahia zaidi katika mikoa mingine.

“Tutawaletea wasanii wenye hadhi kulingana na mapendekezo ya mashabiki husika wa mkoa huo, tena wale waliojizolea sifa ndani na nje ya nchi,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles