Na AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM
SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya maendeleo ya jamii, Ocode, limetumia Sh milioni 836 kwa ajili ya kuboresha shule nane za msingi zilizopo katika wilaya ya Kinondoni na Temeke.
Akizungumza wakati wa kuadhimisha wiki ya elimu iliyofanyika katika Shule ya Msingi Buza, Mkurugenzi wa Ocode, Joseph Jackson, alisema fedha hizo zimetumika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo miundombinu katika shule za Serikali kupitia awamu ya pili ya mradi wa kuboresha elimu.
Alisema mradi huo wa miaka mitatu unaojulikana kama KITE, umeanza kutekelezwa rasmi mwaka 2015 na utamalizika mwaka 2018.
“Mpaka sasa tumejenga miundombinu ya vyumba vya madarasa mfano hapa tulipo (Shule ya Msingi Buza), tumeshajenga vyumba vinne vya madarasa, maktaba, ofisi ya walimu pamoja na bwalo la kulia chakula kwa wanafunzi,” alisema Jackson.
Alisema mradi umejikita zaidi katika ujenzi wa miundombinu wa shule teule, kununua samani za shule, kufundisha walimu mbinu za kufundishia pamoja na kutoa elimu ya afya kwa wanafunzi.
Alisema awamu ya kwanza ya mradi huo ambao ulikuwa na mafanikio makubwa kwa wanafunzi ulianza kutekelezwa kuanzia 2012 na kumalizika 2015.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Wilaya ya Temeke Idara ya Udhibiti Ubora, Josephine Buyagwa, alisema mradi huo mbali na kuongeza vyumba vya madarasa pamoja na madawati unawasaidia zaidi walimu kupata mawazo mapya katika utendaji kazi wao.
“Walimu wanatakiwa kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kupata mbinu mpya za kujifunzia, tukisema tusubiri Serikali pekee itoe mafunzo hawawezi kuwafikia walimu wote, kupitia huu mradi walimu wetu wataweza kuongeza uelewa wa masuala mbalimbali na kuweza kuyatumia katika kazi zao,” alisema Buyagwa.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi ya Kibondemaji, Hassani Msonzo, alisema mradi huo ambao umeisaidia shule yake kupata vyumba sita vya madarasa na mashimo 12 ya choo ni chachu kubwa ya kuleta mabadiliko ya elimu ya msingi katika shule zilizoteuliwa.
Shule zilizonufaika na mradi huo kwa upande wa Manispaa ya Temeke ni pamoja na Buza, Kibondemaji, Bwani na Mtoni Kijichi, wakati wanufaika wa Wilaya ya Kinondoni wakiwa ni Kawe A, Tumaini, Mtambani na Bunju A.