*Polisi wawatawanya kwa mabomu, madiwani wakamatwa
NA HARRIETH MANDARI – GEITA
JESHI la Polisi mkoani Geita, jana limewatawanya kwa mabomu na risasi za moto, wananchi waliokuwa wametanda kwenye lango la kuingia katika mgodi wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu Geita (GGM) wakizuia magari kuingia au kutoka.
Watu hao wakiongozwa na madiwani wa halmashauri mbili za mji na Wilaya ya Geita, walikuwa wakitaka kampuni hiyo ilipe deni la Dola za Marekani zaidi ya bilioni 12 (Sh bilioni 26). Fedha hizo ni ushuru wa huduma katika halmashauri hizo.
Mtanzania ilishuhudia watu waliokuwa wamejaa kwenye lango la kuingia katika mgodi huo wakikimbia ovyo baada ya polisi kupiga mabomu ya machozi na kufyatua risasi hewani.
Baadhi ya waendesha bodaboda waliopita eneo hilo, pia walishushwa na kupigwa pamoja na abiria wao.
Katika vurugu hizo, watu watatu walijeruhiwa, akiwamo askari mmoja, kijana aliyejulikana kwa jina moja la Steve, aliyevunjika mguu na dereva wa gari la Halmashauri ya Mji wa Geita, Sylvester Muhendeka.
Gari hilo lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara, lilivunjwa kioo cha upande wa kulia.
Madiwani wawili na mwananchi mmoja walitiwa nguvuni na polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema uchunguzi unaendelea dhidi yao.
HALI ILIVYOKUWA
Hali hiyo ilianza kujitokeza saa 10.00 kwa kuweka mawe kwenye barabara inayoingia mgodini hapo na kukata bomba la maji kwenye chanzo cha maji yanayokwenda mgodini kilichopo Nungwe.
Mbunge wa Geita, Joseph Msukuma (CCM), aliiambia Mtanzania kuwa alisikitishwa na Kamanda Mwabulambo kumtuhumu kuwa ndiye mchochezi wa mgogoro huo.
“Cha kushangaza hili suala hata sikuwapo, nimeitwa na madiwani jana, nikaharakisha kuja hapa kusikiliza malalamiko ya wananchi wangu.
“Sasa nashangaa inakuwaje Kamanda Mwabulambo anakuwa na chuki binafsi na mimi na ninazungumza hapa kwa hasira, hata nikipigwa risasi sasa hivi ni yeye,” alisema.
Alisema cha muhimu zinahitajika hizo fedha ambazo ni malimbikizo tangu mwaka 2004 na akawahakikishia madiwani kuwa zikilipwa, zitatumika ipasavyo katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Sisi hatutaki kuvunja amani, tunachodai ni malipo kutoka GGM ya malimbikizo ya deni la kodi za huduma tu basi,” alisisitiza.
KAULI YA DHARAU
Akizungumzia suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Costantine Moorland, alilaani kitendo cha polisi kutumia nguvu kuwatawanya viongozi na wananchi ambao walikuwa nje ya mgodi.
“Kwa kweli hapakuwa na aina yoyote ya uvunjifu wa amani, sasa tunashangaa kuona watu wanapigwa na kulipuliwa mabomu ya machozi.
“Kuna vifo vinatokea mgodini, lakini haujawahi kuona nguvu kubwa kama iliyotumika hapa,” alisema Moorland mwishoni mwa kikao cha madiwani na wajumbe wa kamati ya ulinzi ya mkoa kilichofanyika baada ya hali kutulia.
Alidai RPC Mwabulambo alitoa kauli ya dharau kwa madiwani kwamba hakutegemea madiwani wa CCM kufunga barabara badala yake alitegemea wangekuwa ni madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Alimtaka Kamanda Mwabulambo kuiomba radhi CCM na Serikali kwa ujumla kwa kauli alizotoa, akisisitiza kuwa amekidhalilisha chama hicho.
“Kauli hiyo inadhihirisha wazi kuwa polisi wanakuwa na upande wanapoenda eneo la kazi na hilo halitakiwi.
“Kwa kutuuliza kwa dhihaka iwapo sisi ni CCM au siyo, hiyo kauli ni mbaya kwa sababu sisi tulikuwa tukidai haki ya kodi hiyo kwa niaba ya wananchi wetu,” alisema.
MADIWANI LAWAMANI
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga, aliwalaumu madiwani hao kwa kukata bomba la maji katika chanzo cha maji cha Nungwe na akashauri suala hilo limalizwe kwa kutumia busara kwa manufaa ya wana Geita.
“Waheshimiwa madiwani tuweke mbele hekima na busara, tuweke mbele huduma za jamii, za mgodi wa GGM na wananchi kwa jumla ziendelee kwa amani.
“Hebu tuwe watulivu wakati tukitafuta suluhu, kudai haki ni sawa, lakini ni njia zipi mnatumia kuzidai? Tuache kudai haki kwa njia ya fujo ya aina hii kwa sababu sheria za nchi haziruhusu,” alisema.
HAKUNA SULUHU
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi, alisema baada ya vurugu hizo, alikaa na uongozi wa GGM, lakini haikupatikana suluhu ya uhakika.
“Hata hivyo tumewasiliana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani juu ya suala hili na tumekubaliana kukutana Jumatatu ijayo kujadili.
“Ni matumaini yangu kuwa katika kikao hicho tutapata suluhu kwa kuwa Naibu Waziri na Kamishna wa Madini na wataalamu watakuja na nyaraka zote,” alisema.
UVUNJIFU WA SHERIA
Kamanda Mwabulambo, alisema kitendo kilichofanywa na madiwani kufunga barabara zote zinazoenda katika mgodi wa GGM na kukata bomba linalopeleka maji mgodini ni uvunjifu wa sheria.
“Wakiwa kama viongozi kwenye jamii ambako ndiko sheria ndogo wanazitunga na kuzifanyia kazi, halafu kinyume na hilo wao wamekuwa ndiyo wavunjifu wa sheria hizo, Serikali haikuweza kulinyamazia na ndiyo maana tulienda eneo la tukio kuwasitisha,” alisema.
Alikanusha madai kuwa aliikashifu CCM, madai ambayo madiwani hao waliyatoa wakisema kwamba aliwadhalilisha.
Kamanda Mwabulambo alisema madiwani ndio waliotumia vibaya madaraka kwa sababu walitumia hadi magari ya Serikali katika kuandamana.
Alisema polisi wamewakamata madiwani wawili na raia mmoja na uchunguzi unaendelea dhidi yao.
Alikataa kutaja majina ya wanaoshikiliwa na polisi akidai kuwa hatua hiyo itavuruga uchunguzi unaoendelea.
MWENYEKITI WA MTAA
Mwenyekiti wa Mtaa wa Compound, Edgar Onyango, alilaumu kitendo cha Kamanda Mwabulambo kuamuru askari kutumia nguvu kuwatawanya wananchi.
Akichangia kuhusu chuki miongoni mwa wananchi wanaoishi jirani na mgodi, Onyango alisema wamekuwa na malalamiko, lakini hakuna lililotekelezwa.
“Zipo nyumba nyingi tu zimepasuka kutokana na milipuko ya migodini, hakuna maji na matatizo mengi tu, lakini tumekuwa tukidai GGM kuchangia huduma za jamii bila mafanikio.
“Wakati umefika kwa wao kuwa mstari wa mbele kusikiliza malalamiko ya wananchi,” alisema.
Mkazi wa Nyamalembo jirani na mgodi wa GGM, Rebeka Stefano, alilaumu kitendo cha uongozi wa mgodi kuwafukuza kuchimba dhahabu na kuendesha shughuli zozote za maendeleo.
Hadi Mtanzania inaingia mtamboni mji wa Geita ulikuwa shwari, huku madiwani katika kikao chao na wajumbe wa kamati ya ulinzi walikubaliana kusuburi suala hilo litafutiwe ufumbuzi Jumatatu.