NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA Yussuf Manji na wenzake watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, wameachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kusema hana nia ya kuendelea kuwashtaki.
Manji ambaye pia ni Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya soka ya Yanga, alikaa mahabusu kwa siku 76 baada ya kuibuka taarifa za kukamatwa kwake Juni 30, mwaka huu na kusomewa mashtaka Julai 5, akiwa amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Mfanyabiashara huyo na wenzake, walifikishwa mahakamani jana mchana kimya kimya kwa dharura baada ya Jamhuri kuomba hati ya kuwaleta kwani kesi yao ilikuwa inatajwa Septemba 18, mwaka huu.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, aliifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kwamba Jamhuri waliomba hati ya kuwaita washtakiwa.
“Tuliomba hati ya kuwaita washtakiwa, DPP kawasilisha hati, anasema hakusudii kuendelea kuwashtaki kwa kesi hii ya uhujumu uchumi, anaomba kuondoa mashtaka chini ya kifungu cha sheria 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20,” alidai Kishenyi na kuiomba mahakama iliondoe shauri hilo.
Alipotakiwa kujibu kama ana kitu cha kuzungumza, Wakili wa Manji, Hajra Mungula, alidai anakubaliana na maombi ya DPP.
Hakimu Shaidi alisema mashtaka yameondolewa, hivyo mahakama inawaachia huru washtakiwa wote.
Baada ya mahakama kusema hayo, Manji aliomba kuzungumza na hakimu alipomuuliza kama anahitaji kuzungumzia malalamiko yake ya kuvuliwa udiwani, alijibu alitaka kuzungumzia hilo.
Hakimu Shaidi alimfahamisha Manji kwamba malalamiko ya kuvuliwa udiwani atayashughulikia sababu tayari yuko huru, hatakamatwa.
Manji aliondoka katika viunga vya mahakama kwa kutumia gari aina ya Alteza ya bluu yenye namba za usajili T 383 DFN kuelekea uraiani.
Septemba 4, mwaka huu, Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili Kishenyi, iliomba washtakiwa hao kuchukuliwa na polisi kuhojiwa kuhusu kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 33 ya mwaka huu.
Mahakama iliruhusu na washtakiwa hao walienda kuhojiwa kukamilisha upelelezi na siku iliyofuata walirejeshwa mahakamani na kurudi magereza.
Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Deogratius Kisinda, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.
Hata hivyo Manji anakabiliwa na kesi nyingine ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroine katika mahakama hiyo ambayo iko katika hatua ya utetezi.
MASHTAKA SABA YALIYOWAKABILI
Manji na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 na mihuri.
Mfanyabiashara huyo alisomewa mashtaka kwa mara ya kwanza akiwa kalazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Julai 5, mwaka huu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali, Tulumanywa Majigo, alidai kuwa Juni 30 katika eneo la Chang’ombe A wilayani Temeke, Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ zenye thamani ya Sh milioni 192.5 na kwamba, mali hiyo ilipatikana kinyume cha sheria.
Katika shtaka la pili, Julai Mosi katika eneo hilo, walidaiwa kukutwa na polisi wakiwa na mabunda manane ya vitambaa hivyo yenye thamani ya Sh milioni 44 mali ambayo ilipatikana isivyo halali.
Washtakiwa katika shtaka la tatu walidaiwa kuwa Juni 30 katika eneo hilo, walikutwa na muhuri wenye maandishi “Mkuu 121 Kikosi cha JWTZ” bila kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Katika shtaka la nne, walidaiwa kuwa Juni 30, eneo la Chang’ombe A, walikutwa wakiwa na muhuri wenye maandishi “Kamanda 834KJ Makutupora, Dodoma” bila kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Shtaka la tano, walidaiwa kuwa Juni 30 katika eneo hilo, walikutwa na muhuri wenye maandishi, “Commanding Officer 835KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe” bila kuwa na uhalali.
Katika shtaka la sita, walidaiwa kuwa Julai Mosi katika eneo hilo, walikutwa na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari SU 383 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Washtakiwa katika shtaka la saba, walidaiwa kuwa Julai Mosi kwenye eneo hilo, walikutwa na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari SM 8573, ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.