25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

BUNGE KUJADILI HALI YA USALAMA NCHINI

Na MWANDISHI WETU -DODOMA

MKUTANO wa nane wa Bunge la 11, unatarajia kuendelea leo mjini hapa baada ya mapumziko ya mwishoni mwa wiki.

Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kutikisa Bunge kabla halijaahirishwa Ijumaa wiki hii, ni uwasilishaji wa taarifa ya hali ya usalama wa nchi.

Taarifa hiyo itawasilishwa siku yoyote wiki hii baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuiagiza Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, wiki iliyopita akiitaka ikutane na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini ili kujadili mwenendo wa usalama wa taifa.

Hoja hiyo ya Spika, ilikuja baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), kuliomba Bunge liiagize kamati hiyo ikutane na vyombo hivyo vya ulinzi na usalama ili kuangalia namna ya kukabiliana na matumizi mabaya ya silaha za moto yanayofanywa na baadhi ya watu.

Katika maelezo yake hayo, Bashe alisema kuna haja suala la usalama wa taifa kujadiliwa kwa kuwa hadi sasa hakuna mbunge mwenye uhakika wa usalama wake baada ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini hapa.

“Mheshimiwa Spika, nasimama hapa nikitumia kanuni ya 47, sehemu ya kwanza na ya pili kwa sababu limetokea tukio la kutikitisa nchi na Bunge lako tukufu.

“Mheshimiwa Spika, tukio hilo ni la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na tayari Bunge limeshatoa kauli, Waziri wa Mambo ya Ndani, ameshatoa kauli na hata Rais nimemuona ametoa kauli kupitia twitter.

“Hapa nchini, yamekuwa yakitokea matukio mbalimbali ambayo sisi kama wabunge, tunapaswa kupata taarifa za matukio hayo kwani sisi ndiyo wawakilishi wa wananchi.

“Kuna tukio la kutekwa kwa Ben Saanane, ameshatekwa pia Roma Mkatoliki na vyombo vya ulinzi vimechunguza matukio hayo, lakini hadi sasa hakuna taarifa zozote tulizopata sisi kama wabunge.

“Hata mheshimiwa Nape Nnauye, aliwahi kutishiwa bastola hadharani na hadi sasa hakuna taarifa tulizopewa sisi kama wabunge ingawa tunatakiwa kuzipata.

“Wakati hali ikiwa hivyo, jana mheshimiwa Lissu ameshambuliwa, tena akiwa katika majengo ya mawaziri na viongozi wengine mjini hapa.

“Kutokana na hali ilivyo, mheshimiwa Spika, mimi nashauri Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge, ikae na vyombo vya ulinzi na usalama ili tuelezwe juu ya kinachoendelea kwa sababu hadi sasa hakuna anayejua uhakika wa usalama wa maisha yake,” alisema Bashe na kuungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge waliosimama.

Akitoa majibu ya hoja hiyo, Spika alisema hana tatizo juu ya kamati hiyo ya Bunge kukutana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwa hoja hiyo ni ya msingi.

“Kama hoja ni hiyo, mimi sina tatizo na kwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, mheshimiwa Adadi Rajabu yuko hapa na ananisikia, basi naagiza kwamba baada ya saa moja kuanzia sasa, akutane na wajumbe wake katika ukumbi wao wa kawaida.

“Wakishakuwa tayari, taarifa yao wailete bungeni hapa ijadiliwe kabla ya Bunge kuahirishwa Ijumaa ijayo,” alisema Spika Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles