NA CHRISTOPHER MSEKENA
WAANDAAJI wa tuzo za vijana 100 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika ‘Most Influential Young Africans’ (MIYA 100), usiku wa kuamkia jana walitoa orodha ya vijana walioingia kwenye tuzo hizo mwaka 2017, wakiwamo Watanzania 8 maarufu wametajwa.
Tuzo hizo ambazo huzihusisha nchi ya Nigeria, Afrika Kusini, Kenya, Malawi, Ghana, Libya, Gambia, Senegal, Liberia, Algeria, Gabon, Rwanda na nchi zingine za Afrika zimewataja Watanzania kama Ali Kiba, Diamond Platnumz, Elizabeth Michael, Flaviana Matata, Lilian Makoi, Jokate Mwegelo, Nancy Sumari na Millard Ayo.
Sifa zilizofanya mastaa hao watajwe kwenye orodha hiyo ya vijana 100 wenye ushawishi barani Afrika ni pamoja na umri wa miaka 40 kushuka chini, uwezo binafsi wa kuishawishi jamii bila kuhusisha viwango vya elimu.
Mastaa wengine kwenye tasnia ya burudani waliotajwa ni pamoja na Davido na Wizkid kutoka Nigeria, AKA, Cassper Nyovest na Nasty C kutoka Afrika Kusini.