29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

OKWI HABARI YA MJINI

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, raia wa Uganda, Emmanuel Okwi, amedhihirisha uhodari wake baada ya kuiwezesha timu yake kupata ushindi mnono dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.

Simba imeanza ligi hiyo kwa kupata ushindi wa mabao 7-0 na mara ya mwisho kupata ushindi mnono ilikuwa msimu wa ligi 2012/13 walipowafunga watani wao wa jadi, Yanga mabao 5-0 katika Uwanja wa Taifa, huku Okwi akifunga mabao mawili.

Katika mchezo huo wa jana, Okwi aliifungia Simba mabao manne katika ushindi wa mabao hayo saba na kuiwezesha kukalia usukani wa ligi hiyo.

Katika mchezo huo ulioanza kwa kasi, mshambuliaji wa Simba, Juma Luizio, alikosa bao la wazi baada ya kupiga mpira uliogonga mwamba wa chini wa goli na kutoka nje.

Furaha ya mashabiki wa Simba ilianza katika dakika ya 18, baada ya Okwi kuiandikia timu yake bao la kwanza baada ya kupokea pasi kutoka kwa Muzamiru Yassin.

Simba ilionekana kutawala zaidi mchezo huo na katika dakika ya 22, Okwi aliipatia timu yake bao la pili baada ya kuwapiga chenga mabeki wa Ruvu Shooting na kuachia shuti lililojaa wavuni.

Furaha ilizidi kuongezeka kwa mashabiki wa timu ya Simba baada ya Okwi kuipatia timu yake bao la tatu ‘Hat Trick’ katika dakika ya 35, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shiza Kichuya.

Hali ilizidi kuwa mbaya kwa Ruvu Shooting ambao walionekana kuzidiwa, walipofanya mabadiliko katika dakika 37 kwa kumtoa Chande Magoja na kuingia Zubeir Dabi.

Mwamuzi wa mchezo huo, Erick Onoka, kutoka Arusha alimwonyesha kadi ya njano, Ishala Juma wa Ruvu Shooting baada ya kumchezea vibaya kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima aliyetolewa nje na kuingia Mohamed Ibrahim.

Simba ilipata bao la nne katika dakika ya 43 lililofungwa na Shiza Kichuya, baada ya kupokea krosi kutoka kwa beki Erasto Nyoni.

Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Simba katika dakika ya 45 baada ya Juma Luizio kuifungia timu yake bao la tano akiunganisha krosi ya Erasto Nyoni na kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao hayo.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu hizo kufanya mabadiliko, Simba wakimpumzisha Muzamiru Yassin na nafasi  kuchukuliwa na Said Ndemla, wakati Ruvu Shooting walimtoa Hamis Mcha na kuingia Said Dilunga.

Ruvu Shooting walifanya tena mabadiliko katika dakika ya 50 kwa kumtoa Said Madega na kuingia Amani George.

Okwi alizidi kudhihirisha uhodari wake baada ya kuifungia Simba bao la sita katika dakika ya 52, baada ya kuunganisha krosi iliyopiga na Said Ndemla.

Ruvu Shooting walianza kuonyesha uhai katika dakika ya 57 baada ya Baraka Mtuwi kupiga mpira wa adhabu uliopaa juu ya lango la Simba.

Simba walifanya tena mabadiliko katika dakika 65, kwa kumtoa beki Method Mwanjale na kuingia Jjuuko Murshid na katika dakika 81, beki Erasto Nyoni aliifungia timu yake bao la saba baada ya kupiga shuti lililomshinda kipa wa Ruvu Shooting, Bidii Hussein.

Hadi mchezo huo unamalizika, Simba ilitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 7-0 na kuongoza ligi hiyo kutokana na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.

Katika  michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, timu ya Ndanda FC imefungwa bao 1-0 na Azam FC katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Mwadui nao waliifunga Singida United mabao 2-1 katika Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati Mtibwa Sugar wakiifunga Stand United bao 1-0 katika Uwanja wa Manungu, Morogoro.

 

Njombe Mji imekubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Tanzania Prisons, katika  Uwanja wa Sabasaba.

 

Mbeya City vs Majimaji Uwanja wa Sokoine, Mbeya

 

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema ushindi huo mnono umetokana na morali kubwa ya ushindi wa Ngao ya Jamii, lakini pia kambi ya Afrika Kusini na kwamba huo utakuwa mwendelezo katika michezo mingine ya ligi hiyo.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Abdulmutik Hadji, alisema wamepoteza mchezo huo kutokana na kuwakosa wachezaji wake sita waliopo kwenye mashindano ya Majeshi nchini Rwanda.

 

Simba:

Aishi Manula, Ally Shomary, Method Mwanjale/Jjuuko Murshid, Salim Mbonde, James Kotei, Emmanuel Okwi, Muzamiru Yassin/Said Ndemla, Juma Luizio, Haruna Niyonzima/Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya

Ruvu Shooting:

Bidii Hussein, Said Madega/ Amani George, Yusuph Nguya, Mangasini Mbonosi, Shaibu Nayopa, Baraka Mtuwi, Chande Magoja/Zubeir Dabi, Shabab Juma, Ishala Juma, Jamal Soud, Khamis Mcha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles