30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAHEKALU YA LUGUMI KUPIGWA MNADA

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

NYUMBA tatu za kifahari za mfanyabiashara maarufu nchini, Said Lugumi, zinatarajiwa kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutokana na kudaiwa mabilioni ya shilingi.

Nyumba hizo zilianza kushikiliwa na TRA tangu Aprili mwaka huu na jana Kampuni ya Udalali ya Yono ambayo ni wakala wa kukusanya madeni ya mamlaka hiyo ilitangaza kuzipiga mnada.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono, Scholastica Kevela, alisema nyumba hizo ni ile iliyoko Mtaa wa Mazengo, Upanga kiwanja namba 701, yenye hati miliki namba 18173/35 ambayo ni ya makazi na matumizi ya ofisi.

Mbali na hiyo pia alisema maghorofa mawili yaliyoko Mbweni jirani na Kambi ya JKT Wilaya ya Kinondoni   kiwanja namba 47 Kitalu namba 2, yenye hati miliki namba 72456 ambayo ni ya makazi na nyingene ni ile iliyopo kiwanja namba 57 kitalu namba 2 yenye hatia namba 11839 ambayo inafaa kwa ajili ya makazi zote zinatarajiwa kupigwa mnada Septemba 9, mwaka huu.

Alisema mnada huo pia utahusisha mashine tatu za kutengeneza mabati na folkifti moja ambazo zipo katika yadi ya Yono Bahari Beach mali ya Lugumi zinatarajiwa kupigwa mnada Septemba 2, mwaka huu.

“Tumepewa kazi ya kukusanya kodi ambayo Lugumi anadaiwa, anadaiwa kiasi gani hilo waulizwe TRA lakini ni mabilioni ya shilingi. Wanaotaka kuzinunua tunawakaribisha wafike siku ya mnada,” alisema Kevela.

Kwa mujibu wa Kevela, mfanyabiashara huyo alikuwa na taarifa za kudaiwa deni hilo na kwamba walizifunga nyumba hizo ili aweze kulipa kodi anayodaiwa.

“Serikali ilikuwa ikifanya naye mawasiliano lakini kama TRA inaturuhusu kufanya mnada maana yake ni kwamba ameshindwa kulipa. Na sisi kama kampuni tutaziuza ili kodi yote ipatikane,” alisema.

MTANZANIA ilitembelea katika nyumba hizo na kukuta kukiwa na walinzi pamoja na magari ya kifahari yaliyokuwa yameegeshwa ndani ambayo ni Hammer na Toyota V8.

DENI ANALODAIWA

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Lugumi anadaiwa na TRA zaidi ya Sh bilioni 14.

Hata hivyo alipotafutwa Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alithibitisha kuuzwa kwa nyumba hizo lakini hakuwa tayari kutaja kiasi wanachomdai.

“Kiasi hatuwezi kusema kwa sababu ni makubaliano kati yetu na yeye. Tumefikia hatua hiyo baada ya hatua zote kushindikana, kulikuwa na makubaliano lakini hajayatekeleza,” alisema Kayombo.

Sakata lake bungeni

Kutokana na mtifuano huo mapema mwaka jana Kamati Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilifanya uchunguzi kuhusu mkataba tata wa kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited.

Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd ilipewa zabuni na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Hata hivyo mashine hizo zilifungwa kwenye vituo 14 tu vya polisi wakati kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha za mkataba.

Mkataba huo wa Lugumi ambao ulitikisa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kwa kuhusishwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kupitia  Kampuni aliyoiasisi ya Infosy Limited ambayo ni mnufaika wa mradi huo.

Waziri huyo aliondolewa Mei 20, mwaka jana kwa kile kilichoelezwa kutokana na ulevi suala ambalo lilizua mjadala kuhusu hatia ya sakata la Lugumi kwa kudaiwa kuwa linazimwa taratibu.

Zabuni ya kufunga mashine hizo ilizua utata ambapo  ilitangazwa Septemba 22, mwaka 2011 na mkataba  ukasainiwa Septemba 23  mwaka huo kwa kipindi cha siku moja mkataba ulisaini jambo ambalo lilielezwa ni hatari kwa maslahi ya nchi.

Wakati wa uchunguzi wa kamati hiyo ilibaini tofauti ya fedha katika mkataba huo ambako wakati taarifa ya Jeshi la Polisi inaonyesha  walitoa Sh   37,163,940,127.7, taarifa ya Ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  inaonyesha fedha zilizotolewa ni Sh   37,742,913.007 ikiwa na tofauti ya Sh milioni 500.

Ripoti ya mkataba huo tata ilitarajiwa kuwasilishwa bungeni kati ya Septemba na Novemba mwaka jana baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuridhia lakini katika hali ya kushangaza Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson aliahirisha mjadala huo kwa kuitaka Serikali itekeleze mkataba huo kwa mujibu wa makubalino.

Mwisho

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles