NA SWAGGAZ RIPOTA
INASIKITISHA unapoona kipaji kikubwa ndani ya msanii Rashid Makwilo (Chid Benz) kikizidi kudumaa. Hivi nani hafahamu kama Chid ni bidhaa yenye fedha nyingi? Utakuwa na chuki binafsi endapo utatilia shaka uwezo wake kisanaa.
Toka alipopata nafasi ya kutambulika kwenye anga la muziki wa Bongo Fleva, Chid Benz alikuwa na bahati ya kupendwa rapa mwenye uwezo wa kuchana na kuimba, kufanya mitindo huru (free style) kwa namna yoyote aliyotaka hali kadharika kukinyambua kipaji chake na kuwapa burudani watanzania.
Muziki ulimpa umaarufu kuliko matukio aliyoyafanya nje ya sanaa lakini Chid Benz yule wa mwaka 2009 siyo huyu wa 2017. Amekuwa binadamu anayesikitisha watu kuliko kuwaburudisha, bila shaka mama yake mzazi anasikia uchungu akiutazama mwenendo mbaya wa mama yake.
Machi 22 mwaka jana,Babu Tale na Kalapina walifanikiwa kumfikisha, Chid Benz kwenye kituo cha Life and Hope Rehabilitation Organization, kilichopo Bagamoyo kwa ajili ya kupata matibabu (Methadone) itakayomsaidia kuacha na matumizi ya dawa za kulevya aina ya Clack (Cocaine iliyo unguzwa) ambazo zilipelekea afya yake kudhoofu.
Baada ya kuachwa kituoni hapo na kuanza kupata matibabu, alianza kupata afya, mwili wake uliodhoofu ulianza kurudi tena na yeye akajiona amepona mpaka Mei 25 ziliposambaa tetesi za kuwa amekimbia kwenye kukaa kule Bagamoyo na amerejea Dar es slaam kuendeleza maisha.
Mara akaanza kuonekana kwenye studio za Wasafi akipiga picha na wasanii kama Diamond Platnumz na Harmonize. Matumaini kwa mashabiki yalirejea upya baada ya kuona hali ya Chid Benz imetengamaa, nakumbuka akaachia ngoma yake aliyomshirikisha Rayvanny unaoitwa Chuma.
Baada ya hapo kimya kikatawala mpaka Desemba 31 mwaka jana ziliposambaa picha zake kwenye mitandao akiwa kwenye hali mbaya kiafya mpaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alifika nyumbani kwa mama wa rapa huyo kumjulia hali na kuangalia namna ya kumsaidia.
Lakini Juni 26 mwaka huu Chid Benz aligonga tena vichwa vya habari za burudani baada ya kurudi kwenye muziki kwa kishindo. Rapa huyo aliibuka na ngoma inayoitwa Muda akiwa amemshirikisha Q Chief wimbo uliobeba hadithi na majuto makubwa kutokana na muda alioupoteza akiwa kwenye kipindi cha utumiaji wa dawa za kulevya.
Ukubwa wa wimbo wa Muda ulimpa shavu la kutumbuiza uwanja wa Uhuru, Dar es salaam katika tamasha la usalama barabarani lililofanyika Agosti 12 mwaka huu. Alionyesha uwezo mkubwa sana pale uwanjani, alishangiliwa mno alipozunguka pale uwanja kuwasabahi mashabiki zake.
Alionyesha wazi kuwa uwezo bado anao, anahitaji kupewa nafasi zaidi ili aonyeshe kile Mungu amekiweka ndani yake lakini ghafla wiki hii Chid Benzi amezua gumzo tena baada ya yeye na wenzake watano kukamatwa na dawa za kulevya na kuwekwa mahabusu katika kituo cha Msimbazi.
Na jumatano ya Agosti 16Â ambapo walipandishwa kizimbazi katika Mahakama ya Wiyala ya Ilala kufuatia maombi yaliyowasilishwa na upande wa Jamuhuri ya kuomba Chid Benz na wenzake kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa muda wa miaka mitatu.
Chid Benz na wenzake walifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Rita Tarimo kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Glory Mwenda ambaye alidai kuwa watuhumiwa hao walifikishwa kizimbani kufuatia kiapo kilichowasilishwa na kituo cha Polisi Msimbazi, Dar es Salaam.
Mbali na kuwekwa chini ya uangalizi wa polisi na Mahakama kwa kipindi cha miaka mitatu pamoja wadhamini wao ambao watasaini bondi ya shilingi milioni 2. Hivyo Chid Benz na wenzake wakatoka nje kwa masharti hayo.
Wataalamu wa masuala ya dawa za kulevya wanasema mtu ambaye tayari ameingia kwenye utumiaji wa dawa za kulevya ni ngumu kuacha kama wenyewe hawajaamua kuacha. Naamini tukio hili limeonyesha wazi Chid Benz hayupo tayari kuacha mpaka pale atakapoongea na nafsi yake na kuamua mwenyewe kuacha na kujikita kwenye muziki.