NAIROBI, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta, Jumatatu alidai kuwa katu hawezi kushindwa na kiongozi wa NASA, Raila Odinga kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumanne ijayo.
Akizungumza kwenye mikutano ya kisiasa katika kaunti za Kisii na Bomet, Rais Uhuru aliyeandamana na naibu wake William Ruto, alisema ni kichekesho kwa NASA kudai kuwa watamshinda.
“Kama nilimshinda nilipokuwa nakabiliwa na kesi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mwaka 2013, atanishinda vipi sasa hivi nikiwa ndani ya Serikali?” alihoji.
Aliwataka wakazi wa Kisii wasipotoshwe na Raila, na wajitokeze kwa wingi Agosti 8 wampe nafasi nyingine ya kukamilisha maendeleo aliyoyaanzisha.
Alikuwa akizungumza katika uwanja wa michezo wa Gusii ambako pia alisema kuwa eneo la Etago litakuwa kaunti ndogo.
“Watu wa jamii ya Kisii nawaomba mnipigie kura na nitazidi kufanya kazi na nyinyi hadi nitakapomaliza muhula wangu,” alisema Rais Uhuru.
Alijipiga kifua huku akisema kuwa tangu mwaka 2013 Jubilee imewafanyia kazi watu wa jamii ya Abagusii bila ya kujali kama walimuunga mkono katika uchaguzi mkuu uliopita.
Pia alisema kuwa reli ya kiwango cha SGR ambayo imeunganisha Nairobi na Mombasa, itajengwa na kupitia Kaunti ya Kisii ikielekea Kisumu.