29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

FAIDA UWEKEZAJI KATIKA MILIKI YA NYUMBA

Na FARAJA MASINDE,

KWASASA uwekezaji katika nyumba ni jambo linalokubalika na kuchukuliwa kama mfumo wa rasilimali wenye faida na hivyo kuvutia kundi kubwa la wawekezaji wa hapa na nje ya nchi.

Hakuna asiyetambua kuwa, kumiliki nyumba iwe ya kuishi au ya biashara, kuna faida nyingi zinazozidi matarajio ya walio wengi. Umiliki huu humpa mmiliki faida nyingi, ikiwamo kulinda mali za mmiliki dhidi ya mfumuko wa bei, kwani ardhi na nyumba ndio rasilimali pekee zinazoongezeka thamani kadiri muda unavyopita au kuongezeka katika mipangilio ya kiuhasibu na uchumi kwa ongezeko la thamani na njia sahihi ya kujiwekea akiba, kama wanavyofanya mashirika mengi ya hifadhi ya  jamii kwa kuwa na majengo mengi kama hadhari ya kuporomoka thamani kwa fedha  na mali zao.

Pamoja na yote hayo, ni wazi kuwa, faida hizi huja na changamoto zake.

Katika makala haya ya makazi, leo tutajikita zaidi katika kuangalia faida zaidi kuliko changamoto, ili kuwahamasisha Watanzania wengi kujihusisha na sekta hii inayoashiria utajiri. Ndiyo maana kuna kodi ya majengo.

Kuna wakati baadhi ya watu hufikia hatua ya kuchukia mfumuko wa bei pale wanapokuwa hawana rasilimali madhubuti ya kukabiliana nao.

Ikiwa unamiliki nyumba kwaajili ya makazi, biashara, chuo, nyumba ya kupangisha au vitu vingine kama kisima cha kuchimba mafuta, shamba la mazao hai, mgodi wa dhahabu nk, ni dhahiri utakuwa na furaha kwa kuwa utaona mfumuko wa bei ukifanya kazi mubashara unapokuongezea kipato.

Mfumuko wa bei tafsri yake ni kuongeza bei ya rasilimali yako haraka zaidi ukilinganisha na gharama ulizotumia kwenye kuwekeza pamoja na gharama za uendeshaji.

Kwasasa baadhi yetu tunaweza tukawa tunaona kuwa kodi za nyumba zimepanda maradufu, lakini baada ya kipindi cha miaka 10 ijayo zitaonekana ni nafuu sana kuliko ilivyo hivi sasa.

Hii inatokana kwamba, unapokuwa unamiliki nyumba unafanya biashara ya kuingiza pesa wakati wa mfumuko wa bei, panapotokea mfumuko wa bei wa kiwango kikubwa pesa yako itakuwa inapungua thamani kwa kiwango kikubwa mno, huku rasilimali zako zikizidi kuongezeka thamani yake maradufu. Huo ndio msingi wa uchumi.

Baada ya hapo hali ya uchumi hurejea na kufanya ongezeko la kodi ya nyumba.

Uwekezaji katika nyumba hurahisisha sana mchakato wa kuhamisha utajiri wako kwenda kizazi kingine. Kwani unaweza kumilikisha mali toka kizazi kimoja hadi kingine kwa kusudi la kufanya maisha ya kizazi husika kuwa mazuri zaidi.

Chukulia mfano sasa hivi vijana wanalalamika sana kuwa hawatakuwa na uwezo wa kumiliki nyumba kama ilivyo kwa wazazi wao kwa sababu ya gharama kubwa za ujenzi.

Fikiria ni kwa namna gani hali hii itakuwa ngumu kwa watoto wao endapo wazazi wenyewe wameshindwa kuwekeza katika nyumba.

Inapotokea kuwa wazazi wako wanakupa moja kati ya nyumba zao wanazomiliki maisha huwa mepesi ikiwa na maana kwamba utakuwa huwezi kukabiliwa na mikikimikiki ya maisha, hususan kulipia kodi. Nyumba itakupa furaha na kuridhika kwa moyo kuwa uko salama na ni kwako.

Uwekezaji katika nyumba, hususan katika nyumba za makazi unakuwezesha kutumia juhudi kidogo sana kujenga uchumi wako, hasa katika utafiti wa nyumba unayohitaji na aina ya wapangaji unaowahitaji.

Nyumba utakazochagua zinatakiwa ziwe kwenye maeneo bora na yanayopakana na sehemu nzuri ili kuongeza uwezekano wa kupata wapangaji.

Baada ya kupata taswira kamili na uchambuzi juu ya kiasi cha kodi wanachotakiwa kulipa hiyo ni ishara tosha kuwa umewathamini wapangaji wako na unaweza kutumia nafasi hii katika kufanya uwekezaji usiohusisha fedha.

Sambamba na hili, nyumba yako inakupa usalama wa hali juu kinyume na fedha ambazo hazitoi mchango mkubwa zaidi ya wasiwasi wa kuporwa au kupoteza, vilevile nyumba hutatua mahitaji ya msingi ya binadamu kwa maana ya makazi.

Kwani hata pale inapotokea umeyumba kiuchumi bado unakuwa na mahala sahihi pa kukimbilia kama siyo kuanzia, kwani ni rasilimali isiyoshuka thamani na badala yake hupanda kulingana na namna unavyoijali na mazingira uliyopo.

Uwekezaji katika nyumba unakuwezesha kufuatilia mali zako, kwa kuwa mali unazomiliki zinaweza kufuatiliwa na hivyo kukufanya ujijengee himaya yako mwenyewe kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia wengi wakifanya.

Unapowekeza katika hati fungani binafsi au hata hatifungani za umma, unaimarisha kwa kiasi kikubwa sana imani na uadilifu katika kuongoza.

Kwa kuwekeza katika nyumba unakuwa na uhakika kabisa wa kile ambacho kitafuata endapo utazingatia njia sahihi zinazofaa.

Unapomiliki mali ambazo muda wote zinaongezeka thamani na kukubalika muda wote hiyo inakupa morali nzuri ya kuongeza kiasi cha mtaji ambacho kitakusaidia kuongeza kiasi cha mali au utajiri wako.

Katika uchumi kama huu wa hapa kwetu, kumiliki mali ambazo hazihamishiki kama vile nyumba unapata hoja thabiti ya kuiwasilisha kwa maofisa wa benki pale unapofanya nao mazungumzo kwa ajili ya faida ya akiba au pale unapohitaji kuchukua mkopo na hili limekuwa likiwasaidia watu wengi wanaowekeza kwenye nyanja hii kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kupata mafanikio makubwa.

Kwa sasa inaaminika kabisa kuwa nyumba ni dhamana ambayo inapendelewa sana na mabenki kabla ya kutoa mkopo na hukubalika kirahisi kama dhamana mahakamani. Juu ya hili hakuna kitu mtu atakachokwambia mpaka pale utakaponunua nyumba yako, hii yote ni kwa sababu ya mambo ambayo hayawezi kuthibitika.

Hata hivyo, kuna uwezekano usimiliki nyumba tangu mwanzo, inafurahisha pale ambapo hutokea kuwa humlipi kodi mtu yeyote inapofika mwisho wa mwezi.

Ni fahari kubwa pale inapotokea mtu ukamiliki nyumba yako mwenyewe na kujiepusha na changamoto za kodi kila inapofika muda fulani. Isitoshe, masharti mengine ya kukodi nyumba yana usumbufu na unyanyasaji ambao  unakatisha tamaa.

Pindi inapotokea hali ya kiuchumi imeyumba kwa muda kwenye soko, wamiliki wengi wa nyumba wamekuwa wakitumia nyumba zao kama kitega uchumi chao madhubuti.

Kwa namna hii ni kwamba, kwa wale ambao wapo katika hali ngumu ya kiuchumi, hawatakiwi kukata tamaa, kwani mara nyingi changamoto za kifedha huwa ni za muda tu. Kisheria kama mtu amepata na matatizo anaweza kujidhamini mwenyewe kwa kutumia hati za nyumba yake na kuendelea kuwa huru kwa dhamana inayolingana na nyumba yake.

Baadhi ya vitega uchumi hudhihirisha kuwa vinahitaji juhudi ndogo sana na inahusisha ufadhili mwingi wa ziada ili kuleta ongezeko la thamani kufuatana na wakati uliopo.

Hata hivyo, kuna kundi lingine la watu ambalo hawana pesa ya kianzio katika uwekezaji wa makazi, jambo ambalo limekuwa likitafsiriwa kama ni watu wasio na mipango ya kuishi mjini kwa zaidi ya miaka mitano au hawataki kuingia katika mkanganyiko wa kuanza kusimamia wapangaji.

Wakati mwingine pia watu hawa hufikiria juu ya kujiunga na mifuko ya pamoja ya uwekezaji kama vile katika Taasisi kama ya Watumishi Housing Company au UTT-AMIS.

Ulipaji kodi una faida zake; kama vile mnyumbuliko, hata hivyo kodi ya nyumba kama yenyewe ilivyo haiwezi kujenga uchumi au utajiri.

Kama unatarajia kuwekeza pesa yako ipo na haina kazi yoyote au ipo kwenye akiba ambayo haina faida kubwa, unashauriwa kuwa ni vyema zaidi ukafikiria kuwekeza kwenye sekta ya nyumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles