25 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

TUTAKAZA MKANDA KUFIKISHA KODI SH TRILIONI MBILI–MAGUFULI

Na MWANDISHI WETU-KIGOMA

WAKATI takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikionyesha makusanyo ya kodi kwa mwezi ni wastani wa Sh trilioni moja hadi 1.3, Rais Dk. John Magufuli, amesema kibano cha kodi kikiongezwa kidogo, mapato yatafika hadi Sh trilioni mbili kwa mwezi.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana asubuhi, wakati akihutubua wananchi wa Wilaya Kibonda, kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Kibondo-Nyakanzi.

“Fedha zinazofanya miradi ni zenu, Serikali haina shamba, haina chochote, inategemea kodi za wananchi, ndiyo maana mimi nawachukia sana wanaokwepa kulipa kodi,” alisema.

Pia alisema wanaokwepa kulipa kodi si wananchi wa kawaida, bali ni watu wakubwa kwa sababu wananchi wanalipa hata wanapotoa nauli za basi.

“Mkipanda kwenye basi, lililipiwa kodi lilivyonunuliwa na mafuta yakiwekwa mnalipa mkodi, ni jukumu tu la waliokusanya kodi kwenye vituo vya mafuta wazirudishe Serikalini, lakini wapo wanaobaki nazo. Hao ndio nataka kulala nao mbele, nimeshatoa siku 14 na sasa hivi zimekabaki 12 au 13,” alisema na kuongeza:

“Serikali ikikusanya kodi, baadaye inazirudishe kwenye maendeleo ya wananchi, tulipoingia madarakani kwa awamu ya tano, kodi zilizokuwa zinakusanywa kwa mwezi ilikuwa kati ya shilingi bilioni 800 hadi 850, tulipobana tu kidogo, tunakusanya shilingi trilioni 1.2 hadi shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi.

“Nina uhakika tukibana zaidi tutapata shilingi trilioni mbili ama shilingi trilioni mbili na kitu, tulipokusanya hizo shilingi trilioni 1.2 hadi shilingi trilioni 1.3, ndugu zangu wa Kakonko na Watanzania kwa ujumla, tulianza kuzitumia fedha hizo, tulianza kwa kutoa elimu bure kwa watoto wetu kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari wanasoma bure, hakuna kulipa ada.

“Walikuwa wanasoma group (kundi) la watu fulani tu wakubwa, watoto wa masikini hawaendi shule, nikasema haiwezekani.

“Kwenye kampeni niliwaambia nitasomesha Watanzania bure, wakasema haiwezekani, nikawaambia nimekuwa waziri kwa miaka 20 najua zinapovuja nitaenda kuziba hukohuko.”

Alisema fedha nyingi zimekuwa zikivuja serikalini kutokana na matumizi mabaya ndani ya Serikali.

“Watu wanazunguka wanatembea kila mahali, semina za ajabu ajabu, mikutano ya ajabu ajabu, posho za ajabu ajabu, hizo ndiyo zimekuwa ni fedha za wananchi  wanyonge. Na mimi nimesema semina hamna, maposho ya ajabu ajabu hamna, kusafiri hadi nikupe kibali, ili fedha zinazobaki zirudi kwa wananchi,” alisema.

Alisema kwa matokeo ya kubana fedha hizo, kwa mwaka huu bajeti ya dawa imepanda kutoka Sh bilioni 30 hadi Sh bilioni 250 na vitanda vya Sh bilioni 33 vimenunuliwa kwa ajili ya hospitali.

 

ATOBOA SIRI KUWATEUA PROFESA NDALICHAKO NA DK. MPANGO

Katika hatua nyingine, Magufuli, alitoboa siri ya kuwateua Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Alisema awali wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka juzi, kulikuwa na mazungumzo kati yake na mawaziri hao juu ya kuwania ubunge, hata hivyo, viongozi hao wakasema endapo watakwenda jimboni hawatachaguliwa.

“Tumeamua kuongeza shule za kidato cha tano na sita na waziri huyu (Profesa Ndalichako) ni mchapa kazi kweli, na alipokuwa anataka kuja kugombea ubunge huku  sijui alitaka kugombea jimbo gani, akaniambia nataka kwenda kugombea  nikamwambia nenda wewe profesa watakupa, akasema kule hawawezi kunipa.

“Akaogopa kweli kuja kugombea kwa sababu mngemnyima, nikaona nimteue tu kwenye nafasi yangu, ili kusudi afanye kazi kwa niaba ya wana Kigoma, na Watanzania wote kwa ujumla.

“Pakawepo mwingine alikuwa anaitwa Dk. Mpango, nikamwambia nenda basi na wewe ukagombee Kigoma watakupa, akasema Kigoma hawawezi wakanipa, hawajali, nilipopata urais naye nikampa ubunge nikampa na uwaziri wa fedha.

“Yeye ndiye anasimamia fedha Tanzania nzima, sasa ninawaomba ndugu zangu wa Kigoma, muwe mnawakumbuka wale watakaowasaidia, mambo mengine mnahangaika hapa, mengine ni nyie wenyewe huwa mnakoseaga koseaga,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. kwa niaba ya wananchi wa Arumeru Mangharibi tunamuunga mkono Rais wetu mpendwa Dr.John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana anayoifanya kuiletea Tanzania yetu maendeleo.
    Tunamwomba Mheshimiwa Rais wetu atukumbuke nasisi wana Arusha kututembelea karibu sana Mh.Rais.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles