NA AZIZA MASOUD,
KILA mtoto anazaliwa na kipaji chake, yupo anayezaliwa na kipaji cha kuimba, kucheza mpira na ubunifu wa vitu mbalimbali, tatizo kubwa ni katika kuviendeleza.
Kwa maana hiyo, watoto wanazaliwa wakiwa na vipaji ambavyo vikiendelezwa huwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Nimeona mara kadhaa wazazi/walezi wakiwakataza watoto wao kufanya baadhi ya vitu kwa madai kuwa havina faida kwenye maisha yao, wapo ambao hawapendi kuona watoto wao wakicheza mpira, kwani huona kuwa wanapoteza muda na mchezo huo hauna maendeleo kwenye maisha yao.
Nimeshuhudia pia mzazi akimkataza mtoto wake wa kike kuimba kwa madai kuwa, jambo hilo halina faida kwa maisha yake ya baadaye.
Ni kweli kwa mzazi ambaye anapenda maisha mazuri ya mtoto wake na anayeamini katika ajira za kuajiriwa hatapenda kuona mtoto wake anacheza mpira au kuimba, wengi wanaamini mambo hayo yanapoteza muda kwasababu hajayaandaliwa mazingira mazuri.
Lakini ni vyema wazazi wakaelewa kuwa, kumsaidia mtoto kuendeleza kipaji chake kunaweza kuwa na maana kubwa katika maisha yake ya baadaye, karne hii ya sasa watu ambao wamejiajiri kupitia vipaji vyao wengi wamefanikiwa, kikubwa kinachotakiwa ni kuwa mstari wa mbele kumsaidia kutambua mbinu anazotakiwa kuzifanya kwa ajili ya kufanya mambo yenye faida.
Anza hiviÂ
Kwanza gundua kipaji, chunguza na uone anafanya mambo gani ambayo unaweza kumsaidia kuyaendeleza.
Mweleze faida zake na hasara zake, msaidie kujiendeleza, huku ukihakikisha anafanya vizuri kwenye masomo yake, kwani ndiyo yatamuweka kwenye nafasi nzuri ya kuendeleza kipaji chake.
Mweleze muda muafaka wa kufanya mambo yake, mtengenezee misingi mizuri, kwa maana kwamba hata akiingia huko kwenye kujiendeleza asije akatetereka.
Muonye kutojihusisha na mambo mabaya, kama ana kipaji cha uimbaji mueleze madhara ambayo anaweza kupata kama hataingia kwa malengo maalumu, jaribu kumueleza kwamba, yeye awe kama yeye na si kufuata mkumbo.