27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

NYUMA YA PAZIA HISTORIA YA KIBITI

Mkuu wa Jeshi la polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mangwi, Kata ya Mchukwi wilayani Kibiti, alipokwenda kuwapa pole baada ya kutokea mauaji ya baadhi ya viongozi wao

NA YONA MARO,

HISTORIA ya Mkoa wa Pwani ni njia inayounganisha karibu maeneo yote nchini – Ukitaka kwenda kokote kutokea Dar es Salaam lazima upite Mkoa wa Pwani.

Ikumbukwe kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni eneo kuu la biashara nchini kwa miaka mingi.

Kwa wanamkakati wa machafuko, vita na mipango mingine, njia ya kwenda Dar es Salaam wanaweza kuitumia zaidi.

Maeneo haya ya Pwani yana historia pana ni mazoefu kwa vita na machafuko kuanzia Vita ya Majimaji dhidi ya Wajerumani, Vita ya Dunia kati ya Uingereza na Ujerumani, vita ya Ureno na Waarabu kugombea Kilwa na mengine yaliyowahi kutokea, ambayo yameelezwa katika historia kadha wa kadha, ndio kusema hiki kinachoendelea Pwani si kigeni sana kihistoria.

Maeneo ya Pwani kuna mbuga za wanyama, mto mkubwa, maliasili nyingi toka misitu ya huko, ardhi kubwa yenye rutuba, bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, kuna shughuli za utafiti zinaendelea ili kuangalia uwezekano wa kupata nishati zaidi za gesi, mafuta, madini na mengine mengi.

Kwa ugunduzi wa gesi tu, tayari eneo hili ni tajiri na litaendelea kuwa miongoni mwa maeneo tajiri zaidi duniani kufika 2050 na kuendelea.

Utajiri huu wa gesi umevutia watu wengi kujipatia maeneo kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa viwanda, mashamba na sekta nyingine mbalimbali, kama uwekezaji ukishamiri na kuanza kuzalisha. Ina maana maendeleo yataongezeka na maisha kuwa rahisi, lakini hii haitakuwa rahisi kwa washindani wetu wa kibiashara, wale wa mbali tuliozoea kununua kwao nishati kama mafuta na gesi au tuliowategemea kwa muda mrefu.

Pia mradi huu wa gesi, hasa bomba ulipewa kwa nchi ambayo nayo imekua kwa kasi kwa muda mfupi wa miaka 50 mpaka kuwa miongoni mwa mataifa tajiri sana duniani.

Ushindani wa taifa hilo na mengine lazima utaletwa huku kwenye bomba la gesi, kama kipindi kile bomba la kwenda Zambia – kwa hiyo vita yao inaweza hata kuhamishwa maeneo kama haya kwa njia za amani au vurugu.

Maeneo ya Pwani pia ni maarufu kwa biashara haramu, kuanzia zile za magogo, vyakula na bidhaa nyingine mbalimbali na kwa maeneo ya Pwani kama Kibiti ambayo ni masikini na yamekuwa wazi kwa muda mrefu, ni rahisi kwa makundi ya kiharamia kuwekeza huko kwa muda mrefu.

Eneo la Kibiti, Bungu, Ikwiriri na jirani kama Kilwa kuna jamii zenye mahusiano ya karibu ya kikabila na dini, ni ngumu sana kuivuruga jamii kama hii, lakini pia ni rahisi kwa jamii kama hii kuamua jambo kwa pamoja na hata wanapogeukana ni rahisi kujuana, kwa hiyo inafanya ugumu kwa vyombo vingine kuingilia kati kwa kutumia kete za kutisha, kuwagawanya na mbinu nyingine ambazo zinaweza kuleta hofu.

Kutokana na historia ya vurugu toka enzi na enzi, neema ya gesi iliyopatikana na ujio wa wawekezaji, hasa katika sekta za viwanda, hali inaweza kuwa vuta nikuvute kwa jamii yenyewe na mamlaka nyingine.

Pamoja na rasilimali hizo, maeneo mengi ya Pwani ni maskini wa kutupwa, huduma za kijamii ni hafifu kama hospitali, shule, vyuo na taasisi mbalimbali ambazo zinaweza kuwa kioo cha mwamko wa maendeleo kwa wakazi wa maeneo hayo.

Kwa hiyo, hata hao wauaji na waleta fujo nyingine watakuwa na mambo waliyonayo kichwani ambayo inawezekana wanatumia kama propaganda ili wengine waendelee kuwaunga mkono na kukataa yale ya serikali.

Hili ni suala la kisaikolojia linalotakiwa kutazamwa na wataalamu wa fani hii kujua madukuduku ya wananchi, wale waliokamatwa mpaka sasa, ndugu zao na mengine mengi ili kuweza kutengeneza mikakati itakayoweza kusaidia jamii hizi na taifa kwa ujumla.

Hebu fikiria hili .
Kumetokea vurugu kati ya wakulima na wafugaji – wakulima ndio wenye ardhi, hawa wafugaji huenda na kuondoka kulingana na msimu. Wafugaji wengine wakaamua kubaki huko huko karibu na wakulima bila kufuata sheria na taratibu. Mkulima anapolalamika kwa kiongozi wa kijiji, mfugaji atakwenda kutoa fedha kama rushwa ili asiambiwe kitu.
Mkulima anajua kabisa kwamba fulani amepokea rushwa kutoka kwa mfugaji ili amtetee.

Mkulima ataweza kuanzisha vurugu, polisi wakija pale kwanza watachukua taarifa za viongozi wa kijiji na kwenda kumshughulikia mkulima.

Mkulima yule hatakuwa na eneo jingine la kuongelea wala kujitetea, ndipo hapo naye anapoamua liwe litakalokuwa na kwasababu ya kiimani, anaweza kupata msaada kutoka kwingine na hapo ndipo kazi inapoanza kuwa ngumu.

Mara nyingi hawa wanaokuja kutoa misaada hutaka kubaki na masilahi yao, wanaotoa misaada nao wana mitandao yao, hasa kwenye mashirika ya kijasusi yanayojua kwa wazi kuwa  eneo fulani kuna rasilimali hii, kitakachofuatia ni mambo ya kutisha tu.

Tatizo kama hili lingeweza kumalizwa mapema kwa vyombo vya usalama kuwa huru kwenye majukumu yao, bila kuingiliana na taasisi nyingine pale tu inapokuwa muhimu.

Nini kifanyike?

Kwanza nianze kupongeza hatua ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro kwa mkakati wake wa kuanzishwa Kanda Maalumu ya Kipolisi eneo la Kibiti, ambayo itaongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga.

Pamoja na pongezi hizo naungana naye kuwa vitendo vya kihalifu vinavyofanywa katika maeneo hayo haviwezi kumalizwa kwa nguvu ya polisi bali kwa ushirikiano na wananchi wa maeneo hayo.

Kwa muktadha huo nikoleze makala haya kwa kushauri kuwa ni vema na muhimu sana kuwapa vijana mafunzo ya kiupelelezi na kuwapatia malipo ya kazi hiyo. Vijana hao wanaweza kupewa mafunzo ya muda mfupi na mrefu. Vijana hao watakuwa kiungo kati ya vyombo vya ulinzi na usalama kwenye majukumu yao ya kila siku. Vijana ndio hasa wanaojua matatizo ya vijana wenzao, maana wanajuana wenyewe kwa wenyewe.

Serikali ijenge mikakati ya kuinua uchumi wa maeneo haya kwa kuvutia watu wa maeneo mengine ya nchi kwenda kuwekeza katika maeneo kama kilimo, ufugaji, uvuvi, miundombinu ya mawasiliano na barabara.

Vivutio vingine ni pamoja na shule, hospitali, usafiri na hoteli.

Serikali ifikirie pia masuala ya kodi kwa bidhaa au mali zinazotokana na ardhi ya maeneo haya. Inachekesha na kushangaza pale mkazi wa Kibiti anapolazimika kwenda kununua kitanda cha Sh 100,000 – 300,000 Dar es Salaam, wakati mbao zinatoka huko huko Kibiti – utaona hapa tatizo liko wapi, bila hata kulieleza kwa undani .

Fursa za kwenda shule zifunguliwe na ziwe rahisi kwa jamii kama hizi zilizokuwa nyuma kimaendeleo, ili baadaye waje kumiliki uchumi wao wenyewe na kuweza kurithisha wengine.

Mfano pale fursa za kwenda kusoma masuala ya gesi na mafuta vigezo kwa watu wanaoishi maeneo ya mali husika vipunguzwe na wawe wengi, ili hapo baadaye waje kuwa mfano kwa wengine waliobaki na hata vizazi vijavyo.

Vyuo vya masuala ya misitu, uvuvi, gesi, mafuta, kilimo na biashara vipelekwe huko au vyuo vilivyopo vifungue matawi huko watu waende kusoma na kuchangamana.

Ni wakati sasa kwa njia za uchumi kufunguliwa na kuunganisha maeneo ya Pwani, hasa mikoa ya Kusini, ukiwamo Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Morogoro, kuunganika huko kutazihusisha nchi jirani, ikiwamo Malawi, Msumbiji na Zambia.

0786 806028

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles