Na DERICK MILTON-SIMIYU
SERIKALI imesema watumishi wa umma ambao walikutwa na vyeti feki na baadaye wakakata rufaa wakieleza vyeti vyao viko sahihi, hatima yao itajulikana mwishoni mwa mwezi huu, uamuzi utakapotolewa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurian Ndumbaro, wakati akiongea na watumishi wa halmashauri sita za mkoa wa Simiyu, wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani hapa.
Ndumbaro alisema hatua mbalimbali zinaendelea kwa wale wote waliokata rufaa kuhakiki upya vyeti vyao kama kweli ni sahihi kama wao walivyoeleza wakati wanakata rufaa.
Mbali na kueleza hayo, Ndumbaro hakuweza kutaja idadi ya watumishi waliokata rufaa kati ya wale waliokutwa na vyeti feki na kubainisha kuwa rufaa hizo zinapitiwa kwa umakini, ili kubaini kama ni kweli au la.
“Tunatarajia hadi kufikia tarehe 30, mwezi Juni mwaka huu, wale wote ambao walikata rufaa baada ya kubainika wana vyeti feki tutatoa majibu ya rufaa zao, ambazo tulikuwa tunaendelea kuzipitia kwa makini,” alisema Ndumbaro.
Hivi karibuni Rais Magufuli aliwafukuza kazi zaidi ya watumishi wa umma 9,000, baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, iliyoonyesha wana vyeti feki.
Mbali na hilo, katibu huyo alisema serikali inakamilisha hatua za mwisho kutangaza ajira mbalimbali ifikapo Julai, mwaka huu, ili kuweza kujaza nafasi mbazo watumishi wake wamefukuzwa kazi, kutokana na zoezi la vyeti feki.
Kwenye kikao hicho, kilichofanyikia katika ukumbi wa KKKT Bariadi, Katibu Mkuu huyo aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote kuwachukulia hatua za haraka watumishi wa umma ambao wamekuwa wakidhalilisha utumishi wa umma.