27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAHARIRI WAMVAA DK. MWAKYEMBE

TAMKO: Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri,(TEF),Theophil Makunga, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kupinga kufungiwa kwa gazeti la Mawio. Kushoto ni Katibu wa jukwaa hilo, Neville Meena na mjumbe wa jukwaa hilo, Jesse Kwayu. PICHA NA LOVENESS BERNARD

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limesema Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amekiuka Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kwa kujivika mamlaka ya kimahakama ambayo kimsingi hana.

Kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 kinatoa mamlaka kwa waziri kuzuia maudhui katika habari na si kufungia chombo cha habari kama Waziri Mwakyembe alivyofanya kwa kulifungia gazeti la Mawio.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga, alisema mchakato mzima wa kulifungia gazeti la Mawio umekiuka sheria hiyo ambayo Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa inalenga kusimamia weledi katika sekta ya habari.

“Jambo la kushangaza ni kwamba waziri mwenye dhamana ameamua kukiuka sheria hiyo kwa kutoa adhabu ambayo kimsingi ina sura ya uonevu. Maudhui yanayopaswa kuzuiwa na waziri ni yale yanayohatarisha usalama wa nchi au usalama wa umma.

“Tuhuma kwamba Mawio lilikiuka vifungu namba 50 (a), (b), (c), (d) na (e) vya sheria hiyo si za kweli kwani sehemu ya sheria inataja makosa ambayo mwandishi wa habari anaweza kutiwa nayo hatiani ikiwa atafikishwa mbele ya mahakama,” alisema Makunga.

Alifafanua kwamba vifungu hivyo vinahitimishwa kwa adhabu inayotolewa na sheria kwa makosa husika ambazo ni faini kati ya Sh milioni tano hadi Sh milioni 20, kifungo kati ya miaka mitatu hadi mitano au vyote kwa pamoja.

“Kwa kuwa waziri si mahakama, hana mamlaka ya kisheria ya kuwatia hatiani Mawio na hawezi kuwa rejea ya makosa yaliyotajwa katika sheria hii.

“Tunahuzunishwa na utamaduni uliojengeka wa kuona kwamba adhabu pekee ya kukimbilia ni kufungia vyombo vya habari, wizara hii imeacha dhana nzima ya malezi na mashauriano, mwenendo huu hauna afya kwa sekta ya habari na nchi yetu,” alisema.

Jukwaa hilo limeushauri uongozi wa gazeti la Mawio kwenda mahakamani kutafuta haki yake kama walivyowahi kufanya wakati gazeti hilo lilipofutwa Januari mwaka jana.

Naye Katibu wa TEF, Neville Meena, alisema mazingira ya ufanyaji kazi kwa waandishi wa habari nchini bado ni magumu, lakini wamejipanga kutumia njia ya mazungumzo ambayo wanaamini yanaweza kuleta majibu ya matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta hiyo.

Mjumbe wa TEF, Jesse Kwayu, alisema vyombo vya habari si adui wa Serikali, bali vipo kwa mujibu wa sheria na kuitaka Serikali kuacha kuvunja sheria inayosimamia sekta hiyo.

“Waziri Mwakyembe ajiulize mara mbilimbili ni mtu sahihi kusimamia uhuru wa habari? Yeye si bwana jela, amekwenda pale (wizarani) kusaidia sekta ya habari ikue,” alisema Kwayu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles