24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA YA VIWANDA: AJIRA NYINGI ZITATOKANA NA VIWANDA VYA KUZALISHA KWA MKATABA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shonaji wa suruali za Jeans wakati lipotembelea kiwanda cha Tooku kilichopo Mabibo External jijini Dar es salaam . Kushoto ni Meneja Mkuu Msaidizi wa kiwanda hicho, Rigobert Massawe.

VERA FLORIDA MUGITTU, SCOTLAND

VIWANDA vya kuzalisha kwa mkataba (Toll manufacturing) ndiyo suluhisho la ajira nchini. Huu ni utaratibu wa kujenga viwanda vya kukodisha ambapo mwekezaji anajenga kiwanda na kuwekeza kwenye mitambo, teknolojia na ujuzi wa kuzalisha bidhaa bila kumiliki bidhaa. Mwenye kiwanda huzalisha bidhaa za watu wengine kwa malipo bila kuhangaika kutafuta malighafi au soko la bidhaa.

Mwekezaji huyu anawekeza kwenye kutafuta teknolojia, ujuzi wa kusimamia na kutunza mitambo, kujua na kukidhi sheria na kanuni za kuzalisha bidhaa husika ikiwemo kutafuta vibali mbalimbali, ujuzi na utaalamu wa maabara ya kuchunguza bidhaa husika na kuzalisha mpaka kufungasha bidhaa husika. Kisha hutoa huduma kwa watu mbalimbali kwa malipo bila kujali wingi wa bidhaa za kila mkataba.

AJIRA VIWANDANI

Ukweli ni kuwa hatuwezi kusubiri mpaka kila anayetaka kuzalisha bidhaa apate uwezo wa kujenga kiwanda ndipo Watanzania waajiriwe. Kufanya hivyo ni kutegemea viwanda vijengwe na Watanzania wachache wenye uwezo au pengine wageni. Hata hivyo, je ni viwanda vingapi vitajengwa nchini vya kutosheleza kuondoa tatizo la ajira lililopo sasa hivi?

Tukumbuke inakadiriwa karibu Watanzania zaidi ya milioni moja huingia katika soko la ajira kila mwaka. Hii ni sawa na asilimia 2 ya Watanzania. Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa wengi wa hawa hawaajiriki kwa sababu za kutokuwa na ujuzi sahihi au kutokuwa na nafasi za kutosha za ajira. Hii inadhihirisha kuwa ili kuhakikisha watu hawa wanaajiriwa, tunatakiwa kuhakikisha mfumo wetu wa elimu unatoa maarifa sahihi na pia ajira za kutosha zinatengenezwa kila mwaka.

Pia uwezo wa viwanda kuajiri moja kwa moja ni mdogo sana. Kwa mfano kundi la makampuni ya Bakhresa ambalo linamiliki kampuni kubwa kuliko zote za kusaga nafaka Afrika Mashariki, kampuni za kuzalisha bidhaa za vyakula vya majumbani, kampuni ya usafiri wa majini na nyinginezo, limeajiri watu 2000 tu. Hivyo ajira nyingi ni zile za kutoa huduma, kusambaza bidhaa na si za moja kwa moja.

Hali kadhalika uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 24 (sawa na Sh bilioni 53.6 za Kitanzania) katika kiwanda cha Azam cha kusaga nafaka kilichopo jijini Kigali, Rwanda chenye uwezo wa kuzalisha tani 250 kwa siku umeweza kutengeneza ajira 100 za kudumu na vibarua 60 tu. Kati ya ajira hizo, 15 ni wataalamu kutoka India, Kenya, Tanzania na Ufaransa wanaoshika nafasi za juu za kusimamia masuala ya fedha, uzalishaji na ufundi. Kwahiyo bilioni 53 zimetengeneza ajira 160 tu za moja kwa moja.

Mfano mwingine ni Kiwanda cha Saruji cha Twiga (Twiga Cement) chenye pato la wastani wa Sh bilioni 213.8 kwa mwaka. Kiwanda hiki kimeajiri wafanyakazi 341 tu. Viwanda vingine ni vile vinavyomilikiwa na kundi la makampuni ya Mohammed Enterprises ambalo linamiliki viwanda vyenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja vilivyoko katika nchi 11 za Afrika. Nchi hizo ni Uganda, Ethiopia, Kenya, Sudani ya Kusini, Rwanda, Burundi, DRC, Msumbiji, Zambia, Malawi na Tanzania. METL imeajiri watu wapatao 24,000 katika ngazi na shughuli zake tofauti.

Hivyo, kimsingi ajira za moja kwa moja zinazotengenezwa na viwanda hazitoshi kuajiri Watanzania wote wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Pamoja na hayo, ukweli ni kuwa kadiri uwekezaji unavyokua, ndivyo matumizi ya teknolojia yanavyoongezeka ili kuongeza ufanisi. Matokeo yake ni kupungua kwa ajira.

Kwa mfano viwanda vya kuunganisha magari hutumia mashine (roboti) kwa karibu asilimia 90 ya uzalishaji wote ili kutengeneza magari mengi kwa muda mfupi na kwa ubora unaolingana. Hivyo ajira nyingi zitapatikana kwenye kuzalisha na kusambaza malighafi na kwenye kusambaza na kuuza bidhaa za mwisho na si kwenye shughuli za uzalishaji viwandani.

SERIKALI KULINDA USALAMA WA BIDHAA

Sasa hebu tufikirie uwepo wa viwanda vikubwa vya kisasa ambavyo vitatumiwa na watu wengi kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa mkataba na kuuzwa sokoni na watu tofauti. Viwanda ambavyo vitatumia rasilimali watu kidogo tulionao kuhakikisha kila bidhaa inayozalishwa nchini ni ya viwango vya kimataifa bila kulazimisha kila mtu kumiliki kiwanda na kutafuta wataalamu ambao hatuna.

Viwanda ambavyo kwa uchache na uwekezaji wake vitaweza kudhibitiwa kwa umakini na Serikali ili kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini kote ni salama kwa afya ya mlaji na haziathiri mazingira. Viwanda ambavyo kwa uchache wake tutaweza kuhakikisha vinapata nishati na miundombinu muhimu ya kufanikisha uendeshaji wake. Viwanda ambavyo vitakuwa na uwezo wa kifedha na utaalamu wa kubadilisha teknolojia kila inapohitajika. Viwanda ambavyo wamiliki wake hawatakuwa na shida ya kuhangaika kutafuta soko la bidhaa, jambo ambalo hupelekea kuzalisha chini ya uwezo wa mitambo yake.

UBUNIFU NA UZALISHAJI WA VIKUNDI

Hebu tufikirie pia uwezekano wa kijana aliyemaliza shule au kikundi cha vijana, au cha akinamama wajane kuzalisha nyanya za kopo, mafuta ya kula, sabuni, rangi za nyumba au bidhaa nyingine yoyote kwa kiwango cha juu bila kulazimika kumiliki kiwanda. Kwamba mtu yeyote anaweza kuchukua sampuli ya bidhaa aliyoiona sokoni au kuchukua picha kwenye mtandao na kwenda nayo kwa mzalishaji wa mkataba na kuonyesha nia yake ya kuzalisha bidhaa kama hiyo. Hata kama hawaijui jina. Kisha mwenye kiwanda na timu yake wakaifanyia utafiti wa kimaabara na kubainisha ni malighafi gani zinazohitajika kuzalisha bidhaa hiyo na kuwapa maelekezo.

Pia mmiliki wa kiwanda anaweza kuwaunganisha vijana hao na wataalamu wa kutoa ushauri wa kisheria kuhusu kuzalisha bidhaa zinazofanana na nyingine; wataalamu wa masoko watakaowaelimisha jinsi ya kutambulisha bidhaa sokoni (branding) na wataalamu wa kutengeneza vifungashio n.k.

Baadaye mwenye kiwanda atakubaliana nao gharama za kutengeneza bidhaa chache (hata dazeni moja tu) ili walijaribu soko. Hakika fursa hii ya kulijaribu soko kidogo kidogo na kuongeza uzalishaji kadiri soko linavyokuwa bila kuingia hasara za kuzalisha chini ya uwezo wa kiwanda, itawasaidia sana vijana wa Kitanzania kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi. Na pale bidhaa inapokosa soko, wanaweza kubadilisha bidhaa mara moja bila kulazimika kuwekeza upya kwenye mitambo.

Tufikirie pia jinsi uwezekano huu utakavyofungua fursa kwa wananchi wengi hasa vijana za kubuni aina za bidhaa na kuziingiza sokoni kidogo kidogo bila kuzuiwa na kukosa uwezo wa kuwekeza kwenye viwanda na mitambo.

Utaratibu huu hakika utajenga kundi kubwa la wanaomiliki ‘brands’ na kuziingiza sokoni nje na ndani ya nchi. Vijana wetu watakuwa wabunifu pia katika kutumia teknolojia ili kuliingia soko na kuongeza idadi ya bidhaa zinazomilikiwa na Watanzania, badala ya kuwa na bidhaa chache zinazomilikiwa na wachache. Kila Mtanzania atakuwa na fursa ya kuwa na bidhaa.

Utaratibu huu pia utawashawishi vijana kuwakusanya na kuwaunganisha wazalishaji wa malighafi. Pia utatoa fursa kwa wazalishaji wa malighafi kumiliki bidhaa za mwisho. Mfano kikundi cha vijana wa Rufiji wanaweza kukusanya nazi na kutengeneza bidhaa yao wenyewe ya nazi zilizosindikwa na kutafuta soko Msumbiji. Au vijana wa Singida au chama cha ushirika wakamiliki bidhaa bora kabisa ya mafuta ya alizeti n.k.

KUKODISHA HUDUMA ZA VIWANDA

Utaratibu wa kukodisha huduma za viwanda si mgeni nchini na duniani kote. Katika jamii nyingi nchini mashine za kusaga na kukoboa nafaka, hasa unga na mchele zinamilikiwa na mtu mmoja lakini zinatumiwa na watu wengi kwa malipo. Kupitia utaratibu huu mtu mmoja anawekeza kwenye mashine ya kusaga na yeye pekee ndiye anayejua mashine na vifaa vinavyohitajika na jinsi mashine inavyofanya kazi. Yeye pia anahakikisha ana vibali vyote vya biashara. Pia huifanyia matengenezo kila inapohitajika na kuhakikisha inafanya kazi wakati wote. Teknolojia inapobadilika yeye ndiye anayeshughulika kuipata na kuileta kijijini kwake. Mtu huyu anaweza kuajiri watu wachache wa kumsaidia kutoa huduma, lakini mara nyingi hahitaji watu wengi.

Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, uwekezaji huu wa mtu mmoja hutumiwa na familia nyingi zenye uwezo na mahitaji tofauti. Wapo wanaosaga debe moja kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na wapo wanaosaga magunia kwa magunia kwa ajili ya biashara. Wote hawa ni wateja na hawalazimiki kumiliki mashine au kuitunza. Katika kijiji kimoja mashine moja tu inaweza kutosheleza mahitaji ya wanakijiji wote na muda wote huendeshwa kwa faida kuliko ingetumika kusaga unga wa mwenye mashine pekee.

Mifano mingine ni mashine za kufyatua tofali, kumenya kahawa, kukamua mafuta ya alizeti na hata matrekta ya kulimia. Teknolojia hizi humilikiwa na mtu mmoja lakini hutumiwa na watu wengine wengi kwa malipo.

MAABARA BINAFSI

Katika sekta ya afya pia zipo maabara binafsi zinazomiliki vifaa vya gharama kubwa ambazo hutumiwa na hospitali nyingine kuchunguza sampuli. Katika sekta ya afya pia zipo maabara binafsi zinazomiliki vifaa vya gharama kubwa ambazo hutumiwa na hospitali nyingine kuchunguza sampuli. Mfano, kwa hapa Tanzania sampuli hupelekwa Kenya, India na Afrika Kusini ambako hufanyiwa uchunguzi na majibu kurejeshwa kwenye hospitali mgonjwa alipo. Utaratibu huu unazipunguzia hospitali mzigo mkubwa wa kumiliki mashine za gharama kubwa, na pia mzigo wa kuajiri wataalamu wa kila fani.

Utaratibu huu pia unatumiwa na wafanyabiashara kadhaa wa kitanzania wanaouza bidhaa toka Uchina. Wafanyabiashara hawa hutoa oda za bidhaa za viwandani ambapo wenye viwanda hufaya tathmini na kudai malipo ya kutengeneza bidhaa hizo. Bidhaa hizo hutengenezwa kulingana na mahitaji ya mnunuzi na kusafirishwa kuja Tanzania.

Mfano, kwa hapa Tanzania sampuli hupelekwa Kenya, India na Afrika Kusini ambako hufanyiwa uchunguzi na majibu kurejeshwa kwenye hospitali alipo mgonjwa. Utaratibu huu unazipunguzia hospitali mzigo mkubwa wa kumiliki mashine za gharama kubwa na pia mzigo wa kuajiri wataalamu wa kila fani.

WAZALISHAJI WASIOMILIKI VIWANDA

Katika sehemu nyingine duniani, wazalishaji wa magari, mfano Toyota, Nissan, Land Rover, Fiat n.k hawamiliki viwanda vya kutengeneza vifaa vyote vya magari. Badala yake makampuni hayo huingia mikataba na makampuni mengine yasiyo na ‘brands’ za magari, ili wawatengenezee vifaa vinavyohitajika kwa malipo. Kimsingi vifaa vyote hutengenezwa na makampuni tofauti duniani kisha wao huviunganisha kutengeneza gari (car assembling).

Mfano mwingine ni Kampuni ya Genmot ya Ujerumani ambayo imebobea kutengeneza ‘crankshaft’ za magari lakini hawatengenezi magari. Pia Kampuni ya Kayserberg ya Ufaransa imebobea kutengeneza madawa ya binadamu kwa mkataba bila kuwa na dawa zao wenyewe sokoni. Kayserberg hutengeneza kwa mkataba dawa za kampuni kubwa kama Norvatis ya Uswiss zenye thamani ya mpaka euro milioni 39.4 kwa mwaka. Kampuni ya Sony pia inazalisha kwa mkataba kamera za simu za mkononi za makampuni ya Apple, HTC, Samsung n.k.

Forsythe Lubrication kwa upande mwingine ni kiwanda binafsi kinachomilikiwa na familia moja nchini Canada toka mwaka 1911. Kampuni hii inatoa huduma za kuzalisha aina mbalimbali za vilainishi (Lubricants) na uchanganyaji wa vimininika kwa wateja wa aina mbalimbali kuanzia wanaohitaji mapipa 4 hadi kampuni makubwa ya mafuta yanayohitaji mamilioni ya galoni. Kwao, hakuna oda ndogo sana wala kubwa sana.

Kampuni hii pia inatoa huduma za maabara ya kutafiti kupata michanganyiko bora ya bidhaa, uchanganyaji, kutengeneza nembo kwa ajili ya vifungashio, huduma za maghala ya kuhifadhi bidhaa za vilainishi, usafirisaji na hata kutafuta malighafi. Pia hutoa huduma za ushauri wa kitaaluma kwa wateja walio katika biashara ya vilainishi.

Kampuni hii hufanya kazi hizi kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji na siri za kimikataba. Wateja wanaweza kupeleka bidhaa na wakataka watengenezewe bidhaa inayofanana nayo. Pia kampuni inaweza kubadilisha mchangayiko ili kupunguza gharama na kupata bidhaa ya bei nafuu zaidi.

Kampuni hii huwapunguzia wateja wake adha ya kuwekeza katika mitambo, adha ya kujua sheria, kanuni na taratibu za kuendesha biashara ya kuzalisha vilainishi, adha ya kujua au kuajiri wataalamu wanaofahamu kutengeneza vilainishi na pia kuwapa fursa ya kuzalisha bidhaa chache ili kujaribu soko bila kuwekeza kwenye mitambo ya gharama kubwa.

Hivyo kwa mtazamo wangu, viwanda vya aina hii ni fursa kubwa ya kukuza uchumi hasa kama vitaambatana na utaratibu wa kujenga uwezo wa wanaotaka kuzalisha bidhaa. Pia utawaondolea Watanzania adha ya kujua aina ya mashine zinazohitajika na wapi pa kuzinunua, adha ya kujua vibali vinavyohitajika na jinsi ya kuvitafuta na adha ya kutafuta ardhi na mikopo ya kujenga viwanda n.k.

Kwa sasa Watanzania wengi hasa vijana na wanawake tayari wana uzoefu wa kuuza bidhaa kupitia mfumo wa ‘network marketing’ kama ule wa kuuza bidhaa za GNLD (NeoLife International company) na Trevo toka Marekani. Hivyo, ni wazi kuwa wakijengewa uwezo wanaweza kutumia viwanda vya kukodisha kuzalisha bidhaa zao wenyewe zenye ubora wa kimataifa na kuziuza Afrika nzima.

Ninapenda kusisitiza kuwa uzalishaji wa viwandani unahitaji mtaji mkubwa sana wa kuwekeza kwenye mitambo na majengo. Pia uendeshaji wake unahitaji ujuzi mkubwa na rasilimali watu ya uhakika. Hali kadhalika, kutafuta soko la bidhaa na kuhakikisha bidhaa zinashindana sokoni kila siku kunahitaji fedha, maarifa na ubunifu mkubwa. Mahitaji haya si rahisi kwa Mtanzania wa kawaida kuyapata. Hivyo ni lazima tutafute jinsi ya kuwawezesha vijana wetu kushiriki katika ajira za viwanda bila kuzuiwa na ukosefu wa mitaji.

Katika kulitafakari pendekezo langu, nashauri tujikumbushe yafuatayo:

Kwanza, tofauti na nchi za Marekani, Ulaya na Asia zilizoendeleza viwanda kabla yetu, sisi tunafanya hivyo wakati dunia tayari imeshamiri viwanda vya aina mbalimbali vinavyotumia teknolojia ya hali juu kuzalisha bidhaa bora kwa wingi na kwa bei nafuu. Kwa mfano, sasa hvi China inatumia roboti kuzalisha bidhaa nyingi vikiwemo viatu tena kwa bei nafuu sana.Hivyo ushindani wetu ni mkubwa kuliko waliokutana nao wenzetu wakati wanaamua kuwekeza kwenye viwanda.

Pili, Tanzania inawekeza katika viwanda wakati ambao utandawazi, soko huria na teknolojia vinamwezesha mlaji kuchagua bidhaa toka mahali popote duniani. Pia walaji wa sasa wana uhitaji wa aina, viwango na ubora unaobadilika badilika. Hivyo, ubunifu unahitajika sana katika kuzalisha bidhaa zenye ushindani sokoni. Mahitaji ya ujuzi na maarifa miongoni mwa rasilimali watu pia ni makubwa sana sasa kuliko ilivyokuwa wakati nchi nyingine zinafanya mapinduzi ya viwanda. Teknolojia kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya walaji pia hubadilika sana. Hivyo, rasilimali yenye ujuzi sahihi na uwezo wa kupata teknolojia ni muhmu sana.

Tatu, tunawekeza kwenye viwanda wakati dunia iko makini sana katika kuyatunza mazingira na kuhakikisha afya ya mlaji na viumbe wengine inatunzwa. Hii inamaanisha kuwa mitaji mikubwa zaidi inahitajika kuwekeza kwenye teknolojia rafiki wa mazingira na kwenye kukidhi sheria, kanuni, viwango na masharti ya kibiashara ya ngazi ya kidunia, kikanda na nchi. Kama Taifa tumelazimika kuridhia mikataba mingi ya kidunia ambayo haikuwepo wakati China inajenga viwanda vyake.

Nne, tunaingia kwenye viwanda wakati Taifa bado lina changamoto kubwa ya upatikanaji wa mitaji, uwezo mdogo wa rasilimali watu wa kusimamia biashara kubwa, ukosefu wa nishati ya kutosha kuendesha viwanda vingi kwa ufanisi na gharama nafuu na miundombinu hafifu.

Hivyo, hatuwezi kuiga moja kwa moja sera na utaratibu waliopitia wengine kuendeleza viwanda vyao. Sisi kama Tanzania tunapaswa kuwa na utaratibu unaotufaa kulingana na muktadha wetu.

Utaratibu wa kukodisha huduma za viwanda (‘toll manufacturing’) unaweza kututengenezea ajira nyingi na kukuza uchumi wetu kama utapewa baraka na kuungwa mkono na Serikali pamoja na wananchi, sekta binafsi na ya mashirika yasiyo ya kiserikali hasa taasisi za fedha.

Tuwasiliane: +44 7818192320/ +255 784 272 596 au [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles