25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tukio la ‘ugaidi’ latesa wafanyabiashara

Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

WAFANYABIASHARA wa mchele na nyanya waliopo wilaya za Kilombero na Kilosa mkoani Morogoro wamelalamikia kupotea kwa wateja wao kutokana na tukio la watu tisa kukamatwa na Jeshi la Polisi wakiwa na milipuko, silaha za jadi na sare za jeshi katika Msikiti wa Salah Al-Fajih, uliopo Kijiji cha Chikago, Kata ya Kidatu.

MTANZANIA Jumamosi lilitembelea katika vijiji vya Rauha, Kidodi, Ruhembe, Mkamba, Kidatu na Chikago kwa upande wa wilaya zote mbili na lilibaini hali hiyo ilitokana na wakulima na wafanyabiashara wenyeji katika maeneo hayo kulalamikia kushuka kabisa kwa mauzo yao.

Akizungumza kijijini hapa jana, mkulima Said Masuke alisema tukio la kukamatwa kwa watu hao wanaodhaniwa ni magaidi limeleta shida kwa wafanyabiashara katika maeneo hayo, hasa wa mazao na mbogamboga waliopo upande wa Ruaha na Kidatu.
Alisema tangu watu hao walipokamatwa na mwenyeji wao kuuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali, hakuna tena mfanyabiashara mgeni wa mchele, nyanya, matikiti maji na mchele aliyeingia katika maeneo hayo.

Alisema kijiji ama eneo lolote kuhusishwa na matukio ya ugaidi si jambo zuri katika maeneo mengi hapa nchini.

Alisema wateja wengi katika maeneo hayo ni wafanyabiashara kutoka maeneo ya Mombasa, Zanzibar na Tanga na wengi wao ni Waislamu wanaofuga ndevu nyingi.

“Cha ajabu sasa hivi ukifuga ndevu nyingi hapa kijiji cha Chikago na maeneo mengine unahusishwa moja kwa moja kuwa na unasaba na kundi la magaidi,” alisema Masuke.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuna baadhi ya watu wamenyoa ndevu zao kwa kuhofia kuhusishwa na matukio ya ugaidi.

Naye, mkazi wa Chikago, Zahara Mohamed, alisema amefunga mgahawa wake akihofu kuhusishwa na matukio ya ugaidi kwa madai wachuuzi wengi wa biashara kama ndizi, mpunga na mchele wanafika mgahawani kwake.

“Kama wanataka kufanya ugaidi wao waende wakakae porini ili wakumbane na mkono wa sheria na siyo kuja katika nyumba za ibada kujificha, sisi wenyewe tunachangia kuuchafua Uislamu,” alisema Zahara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles